Mtoto mchanga auawa, anyofolewa viungo, ‘bibi wa kambo’ ahusishwa

Bukoba. Mtoto mchanga, Antidius Avitus (miezi minne) amekutwa amefariki dunia na baadhi ya viungo vya mkono wake vikiwa vimenyofolewa huku bibi yake wa kambo akihusishwa.

Mauaji hayo yametokea Nkindo, Kijiji cha Itahwa, Kata ya Karabagaine, Manispaa ya Bukoba.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Novemba 11, 2024, mama wa mtoto huyo, Dorice Avitusi amesema tukio hilo lililotokea Jumamosi Novemba 9, 2024.

Dorice Avitusi Mama mzazi wa marehemu mtoto anayesadikiwa kuuwawa chumbani na kunyofolewa baadhi ya viungo kwenye mkono mmoja.

Amesema jana asubuhi alikuwa na mwanawe akiwa mzima na alimwandalia uji kabla ya kwenda naye kanisani kufanya usafi.

Anasema alirejea nyumbani mchana akiwa amembeba mgongoni akiwa amelala na akapitiliza kwenda kumlaza chumbani.

Akisimulia huku akibubujikwa machozi, Dorice amesema alienda dukani na aliporudi akaendelea kupika chakula cha mchana huku mtoto akiwa kalala.

“Nilipomaliza kupika tukala na ilipofika saa tisa nikasikia mtoto analia nikaenda kumchungulia  dirishani, nikaona bado amesinzia, nikaendelea na shughuli zangu,” anasimulia Dorice.

Anasema alipomaliza shughuli zake alienda kumuangalia tena ndipo akakuta chandarua na mashuka yakiwa na madoa ya damu, alipomfunua mtoto alikuwa anatokwa na povu puani na mdomoni na mkono ulikuwa umechunwa ngozi na baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa.

“Niliogopa sana nilipoona mwanangu yupo katika hali hiyo; mapovu yalikuwa mengi puani na mdomoni, na mwili wake ulikuwa kama umepakwa dawa za kienyeji. Nilianza kumtafuta mume wangu kwa simu na alifika na kuanza kuwasiliana na majirani,” amesimulia mama huyo.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Avitus Ponsiani amesema alipofika nyumba alikuta mwili wa mwanawe umelazwa kifudifudi ukitokwa na povu huku baadhi ya viungo kwenye mkono mmoja vikiwa vimenyofolewa.

Amesema alitoa taarifu kwa viongozi wa kitongoji na majirani zake.

Ndani ya nyumba hiyo, amesema wanaishi na mama yake wa kambo baada ya baba yao mzazi kufariki dunia.

Amesema yeye, ndugu zake na mama huyo hawana maelewano mazuri kutokana na kugombea mirathi ya baba yao.

“Mama yetu wa kambo alikuwa na ugomvi na sisi… Na wakati tukio linatokea, alikuwepo ndani chumbani amelala na wala hakushtuka wakati tukio hili limetokea,” amedai baba huyo wa mtoto.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Itahwa, Kilego Magoli amesema alipokea taarifa za mauaji ya mtoto huyo saa 11 jioni baada ya kupigiwa simu na wananchi.

“Nikatoa taarifa kwa viongozi wa kata na Jeshi la Polisi ambao walifika eneo la tukio na kukuta mtoto ameuawa katika mazingira ya kutatanisha.

Alikuwa amelazwa chumbani, mkono wake ukiwa umechanwa na alikuwa amepakwa kitu kama dawa usoni,” amesema.

Amesema familia hiyo ina migogoro ya mara kwa mara kati ya mama na watoto wa marehemu baba yao.

“Na hata hiki kilichotokea, wanamtuhumu mama huyo ambaye hivi sasa anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi,” amesema mwenyekiti huyo.

Jirani wa family hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake amedai wanandoa hao wanamtuhumu mama huyo kwa mambo mengi, na hata hilo wanamuhusisha.

“Wanasema huenda mama yao anahusika kwa kushirikiana na jirani yake mmoja ambaye naye nyumba yake imechomwa moto na kubomolewa usiku wa kuamkia leo (jana),” amedai jirani huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amesema tayari amefika nyumbani kwa familia hiyo na kuzungumza nao na kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi na baadhi ya watu tayari wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo akiwamo mama huyo wa kambo.

“Nilifika na kuliagiza Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi zaidi. Wakimaliza taarifa kamili nitawajulisha au polisi wenyewe watatoa taarifa kwenu,” amesema Sima.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

Related Posts