Necta yatoa onyo mtihani kidato cha nne kesho

Dar es Salaam. Wakati watahiniwa 557,731 kesho Jumatatu Novemba 11, 2024 wataanza mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limeonya watakaohujumu mtihani huo, kuwa litawachukulia hatua za kisheria.

Necta imesema hayo wakati matukio ya watu kujihusisha na udanganyifu katika mitihani ya taifa yakiripotiwa kila mwaka.

Januari 2024, Baraza hilo lilitangaza kufuta matokeo kwa wanafunzi 178 wa darasa la nne na 28 wa kidato cha pili, waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani yao ya upimaji kwa mwaka 2023.

Baraza hilo pia mwaka 2023 lilifuta matokeo ya watahiniwa 337 wa kidato cha nne waliofanya mtihani mwaka 2022 huku likizichukulia hatua baadhi ya shule na vituo vilivyojihusisha na matukio hayo.

Akizungumza leo Jumapili, Novemba 10, 2024 na waandishi wa habari Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed amesema baraza linaamini walimu wamewaandaa watahiniwa vizuri katika kipindi chote cha miaka minne ya elimu ya sekondari, hivyo halitarajii kuona vitendo hivyo vikitokea.

“Ni matarajio ya Necta, watahiniwa wote watafanya mtihani wao kwa kuzingatia kanuni za mitihani. Baraza halitarajii mtahiniwa yeyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu, atakayebainika kufanya hivyo, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.

“Baraza halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayesababisha udanganyifu kufanyika na kuhujumu mitihani hiyo. Watahiniwa watafutiwa matokeo, kituo cha mtihani kitafutiwa usajili na mashauri ya kinidhamu na ya jinai yatafunguliwa kwa watumishi,” ameonya.

Aidha, Dk Mohamed amewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mtihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wake.

“Baraza linatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha mtihani unafanyika kwa amani na utulivu. Wananchi wanaombwa kuhakikisha hakuna mtu yeyote asiyehusika na mtihani anaingia kwenye maeneo ya shule katika kipindi chote cha mtihani,” amesema.

Katika mtihani huo kati ya watahiniwa wa shule 529,321 waliosajiliwa mwaka 2024, wavulana ni 250,562 sawa na asilimia 47.34 na wasichana ni 278,759 sawa na asilimia 52.66.

Aidha, wapo watahiniwa wa shule 1,088 wenye mahitaji maalumu, kati yao wenye uoni hafifu ni 601, wasioona 56, wasiosikia 209, wenye ulemavu wa akili 39 na wenye ulemavu wa viungo 183.

Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 28,410 waliosajiliwa, wavulana ni 11,167 sawa na asilimia 39.31 na wasichana ni 17,243 sawa na asilimia 60.69. Aidha, kwenye kundi hilo wamo wenye mahitaji maalumu 18 kati yao, mwenye uoni hafifu mmoja, wasioona 16 na mwenye ulemavu wa viungo mmoja.

Dk Mohamed amesema mwaka huu kuna upotevu wa wanafunzi zaidi ya laki moja ambao walipaswa kufanya mtihani huo tangu walipokuwa kidato cha pili wakiwa 690,341.

Mwarobaini wa udanganyifu

Akizingumza na Mwananchi kuhusu onyola Mecta, mchambuzi wa masuala ya elimu, Dk Thomas Jabir amesema changamoto kubwa ya kuendelea kwa udanganyifu katika baadhi ya shule, ni kupambania madaraja ya ufaulu na shule kuutumia kama njia ya kuvutia wanafunzi zaidi.

Ameshauri elimu kuondokana na mfumo wa mitihani, ambao inaonekana kuogopwa.

“Elimu inapaswa kuwa ya ukombozi wa kifikra na sio kukariri ambako kunawafanya wanafunzi pamoja na makundi yenye nia ovu kuhujumu mitihani kwa kutaka kuwapa wananfunzi ufaulu usio wa kwao,” amesema Dk Jabir.

Kuhusu hilo, Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko amesema suala la udanganyifu lina upande wa mwanafunzi mwenyewe na upande wa shule.

“Kwa upande wa shule, amesema inaweza ikafanya hivyo ili ipate wanafunzi wengi na ili kuondokana na hilo, amesema:

“Zitungwe sheria kali zitakazositisha moja kwa moja huduma ya mmiliki wa shule atakayefanya udanganyifu, ili wengine wakiona hivyo waogope,” ameshauri.

Kwa upande wa mwanafunzi, amesema anaweza akafanya udanganyifu kutokana na presha ya ufaulu anayoipata kutoka kwa jamii yake, ambayo inamfanya atafute mbinu mbadala ya kufaulu, hivyo jamii iondokane na dhana kwamba kufaulu ndio kila kitu.

“Kingine, ufundishaji uimarishwe kwani mwanafunzi akifundishwa vyema atatumia maarifa aliyoyapata na hataweza kufanya udanganyifu,” ameshauri Nkoronko.

Related Posts