Rushwa ya ngono yamtupa mhadhiri jela miaka 20

Sumbawanga. “Siku ya kufa nyani, miti yote huteleza,” maelezo haya yanashabihiana na  aliyekuwa mhadhiri wa Chuo cha Paradise Business, Godfrey Mwakitalima ambaye ameshindwa kupangua kifungo cha miaka 20 jela alichohukumiwa kutokana na kosa la kuomba rushwa ya ngono.

Julai 23, 2018 mhadhiri huyo alikamatwa ‘red handed’ ndani ya chumba cha nyumba ya kulala wageni ya Ilembula iliyopo eneo la Chanji Wilaya ya Sumbawanga, alipokwenda kufanya mapenzi na mwanafunzi wake.

Hakufahamu kama mwanafunzi huyo ametoa malalamiko yake Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), iliyoandaa mtego na kumnasa mhadhiri huyo akiwa kitandani.

Takukuru ikamburuza mahakamani ikidai kuwa, Julai 23, 2018, mhadhiri huyo akiwa na mamlaka ya uhadhiri katika chuo hicho, aliomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake kama sharti la kumpa alama za juu katika somo la ujasiriamali.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa jamhuri na utetezi wa mhadhiri huyo wa zamani wa Paradise Business College kuwa mwanafunzi huyo alikuwa mpenzi wake wa muda mrefu, Mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka 20.

Hata hivyo, hakuridhika na hukumu hiyo na kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga iliyotupwa Agosti 31,2021 na Jaji John Nkwabi, lakini hakuridhika akakimbilia Mahakama ya Rufani lakini nako amekwaa kisiki.

Moja ya hoja ilikuwa, upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitishwa shitaka hilo na pia adhabu aliyopewa ilikuwa kinyume cha sheria kwa kuwa, alistahili kupigwa faini isiyozidi Sh5 milioni au kufungo cha miaka mitatu.

Hoja hiyo zote hizo zilipanguliwa na mawakili waandamizi wa Serikali, Safi Amani na Irene Godwin, wakisema hoja ya adhabu batili iliegemea kifungu tofauti na sheria aliyokuwa ameshitakiwa nayo ya kifungo cha miaka 20.

Katika hukumu waliyoitoa Novemba 7,2024 mjini Sumbawanga, Jopo la majaji watatu, Rehema Kerefu, Dk Paul Kihwelo na Gerson Mdemu wameitupilia mbali rufaa hiyo na kubariki kifungo cha miaka 20 jela.

Majaji hao walisema kifungu cha 25 cha sheria hiyo kiliwekwa ili maofisa wenye dhamana wasitumie vibaya mamlaka yao kwa manufaa binafsi kwa kutumia rushwa ya ngono kama mbadala wa rushwa ya fedha na kumlinda mwathirika.

Shahidi wa kwanza wa jamhuri, Daud Fransis ambaye ni mchunguzi kutoka Takukuru, aliiambia Mahakama kuwa Julai 23, 2018, alipokea malalamiko kutoka kwa mwanafunzi huyo aliyekuwa akisomea stashahada ya maendeleo ya jamii.

Kiini cha malalamiko yake ni kuwa alifanya mtihani wa somo la ujuzi wa ujasiriamali huku mwalimu wake huyo akamtua ujumbe mfupi wa simu, akimwambia matokeo yametoka lakini alikuwa amepata alama za chini sana.

Kulingana na ushahidi wake, mwanafunzi huyo aliyekuwa shahidi wa nne wa jamhuri, alimweleza kuwa ili aondokane na tatizo hilo la alama ambazo ni chini ya zile zinazokubalika na chuo, akubali kufanya naye mapenzi.

Baada ya kupokea malalamiko hayo alimjulisha Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Rukwa kisha mtego uliandaliwa na siku ya tukio saa 11 alasiri, timu ya maofisa wa Takukuru walikwenda katika nyumba ya kulala waliyokubaliana.

Shahidi huyo alisema walipofika katika nyumba hiyo waligonga chumba namba nane, mwanafunzi huyo alifungua mlango na kumkuta mwanafunzi akiwa amevua nguo ya juu tu, huku ‘mhadhiri’ akiwa amejifunika shuka tu.

Ushahidi wa shahidi wa nne ambaye ni mwathirika, hautofautiani na ushahidi wa shahidi wa kwanza na timu ya maofisa wengine wa Takukuru huku shahidi wa tano, akielezea ujumbe wa simu uliotumwa na mhadhiri huyo.

Katika utetezi wake, mrufani huyo (mhadhiri wa zamani) hakukanusha madai kuwa Julai 23, 2018 alikamatwa katika nyumba ya kulala wageni ya Ilembula akiwa na mwanafunzi wake wakijiandaa kufanya tendo la ndoa kinyume cha sheria.

Hata hivyo, alishikilia msimamo kuwa mwanafunzi huyo alikuwa ni mpenzi wake wa muda mrefu tangu tangu mwanafunzi huyo akiwa Chuo cha St Aggrey na penzi lao lilipamba moto baada ya mwanafunzi huyo kuhamia Paradise Business College.

Alieleza kuwa, mpenzi wake huyo hakuwa anazingatia masuala ya kitaaluma bali alijihusisha zaidi na anasa na ndio maana hata matokeo yake ya mitihani ya majaribio yalikuwa sio mazuri na kufanya mtihani akiwa na alama mitihani hiyo.

Hiyo ilimfanya afeli mitihani minne mbali na somo hilo la ujasiriamali alilokuwa akilifundisha, hivyo kukosa sifa hata ya kufanya mitihani ya marudio au Supplementary Examinations.

Ili kujiokoa katika hilo, mwanafunzi huyo alijaribu kuwaingia wakufunzi mbalimbali wakiwamo ili wamsaidie  ndipo alikwenda hadi kwa mkuu wa chuo lakini yeye (Mwakitilima) alisimama katika msimamo wake wa kukataa.

Aliieleza Mahakama kuwa, hiyo ndio sababu akamtungia kesi hiyo na kwamba siku alipokamatwa, haikuwa siku ya kwanza kwenda humo na kufanya mapenzi na mwanafunzi huyo ambaye alikuwa ni mpenzi wake wa siku nyingi.

Mahakama iliukataa utetezi wake huo na kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela, ambacho hakuridhidhwa nacho na kukata rufaa Mahakama Kuu ambayo ilitupilia mbali rufaa yake kama ilivyotokea pia Mahakama ya Rufani.

Related Posts