Sababu 10 zatajwa changamoto afya ya akili kwa wanaume

Dar es Salaam. Wataalamu wa saikolojia tiba wamesema ongezeko la matukio ya kuua, kujiua na changamoto ya afya ya akili miongoni mwa wanaume, inachangiwa na ukimya miongoni mwa jinsia hiyo.

Wameeleza umuhimu wa jamii kuwapa wanaume mazingira salama ya afya zao za akili, ikiwemo ‘kufunguka’ bila kuhukumiwa, ili kuwalinda na matokeo hasi ya msongo wa mawazo. Wataalamu hao wamebainisha sababu 10 zinazochangia afya ya akili kwa wanaume.

Hata hivyo, mwanawake wametajwa kuchagiza ongezeko hilo na nafasi yao katika kuleta suluhisho, ikiwemo kutafuta msaada wa awali kwa kundi hilo.

Maoni hayo yametolewa leo Jumapili Novemba 10, 2024 ikiwa ni sehemu ya mazungumzo katika maadhimisho ya mwezi wa afya ya akili kwa wanaume kupitia kampeni ya ‘Movember.’

Mtaalamu wa saikolojia, Saldin Kimangale amesema mara nyingi, wanaume hukosa fursa ya kuzungumza waziwazi kuhusu afya ya akili kutokana na mitazamo ya kijamii inayowafanya wahisi kuwa dhaifu wanapohitaji msaada wa kihisia.

“’Funguka’ iwe ndio neno la kuwahamasisha wanaume kuzungumzia afya zao za akili, ni muhimu kwa jamii kuwapa wanaume mazingira salama ya kufunguka bila kumhukumu.

“Pengine iko haja kwa akina mama, akina dada na wenza wa wanaume kuchukuwa juhudi ya kuwahamasisha wanaume kwenye familia zao kupata msaada wa kisaikolojia kwa wakati,” amesema Kimangale.

Amesema wanaume wana tabia ya kujijengea ukuta na si wepesi kutafuta msaada mapema ukilinganisha na wanawake na hilo huchochea kundi hilo kupata magonjwa mengine kama Bipolar, Schizophrenia na magonjwa ya wasiwasi.

Kimangale amesema wanaume wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa ya akili kwa sababu ya malezi na jinsi ambavyo jamii inawachukulia.

Visababishi wanaume kuongoza

Hata hivyo, wataalamu wa afya ya akili na wanasaikolojia wametaja sababu 10 zinazochangia wanaume kuongoza kuugua magonjwa ya afya ya akili, ikilinganishwa na wanawake.

Sababu hizo ni kuzongwa na majukumu, ugumu wa maisha, utafutaji, malezi, usiri, kukua kwa teknolojia, matarajio ya maisha, sonona, matukio ya nyuma, matumizi ya mihadarati na pombe kupindukia.

Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili zinaonyesha kati ya wagonjwa wa nje 24,014 walioonwa, wanaume walikuwa 15,205 ikilinganishwa na wanawake 8,809 kwa kipindi cha mwaka 2020/21.

Mtaalamu wa afya ya akili na mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Mental Health Tanzania, Dk Philimina Scarion ametaja vyanzo vingine vinavyosababisha wanaume wapate msongo wa mawazo ambao mwishowe hufikia sonona na kujikuta wakipata tatizo la afya ya akili.

“Wanaume wanaoishi katika nchi za uchumi mdogo na kati kama Tanzania, wengi huwa na msongo wa mawazo mara nyingi ikilinganishwa na wanawake,” amesema Dk Scarion.

Ametaja sababu nyingine kuwa wengi wao ni wazito kuzungumza ya sirini mwao, hivyo hujikuta wakikaa na matatizo moyoni baadaye yanafika hatua ya juu na kuchanganyikiwa.

“Pia, jamii yetu imekuwa na dhana kuwa mwanamume ni mtu mwenye nguvu, hivyo hapaswi kuonyesha udhaifu wa kuumizwa hivyo wanabaki na maswali mengi wakijiuliza na kujijibu wenyewe,” amesema Dk Philimina.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mwaka 2023 inaonyesha hali ya afya ya akili kwa mwaka 2020, ilikadiria mzigo wa magonjwa ya akili umechangia kiwango cha vifo vya kujinyonga cha asilimia 8.15 kwa kila watu 100,000.

Vivyo hivyo, mwaka 2022 ripoti ya Wizara ya Afya ilieleza mzigo wa maradhi ya akili umepanda kutoka wagonjwa 386,358 mwaka 2012 hadi 2,102,726 kufikia mwaka 2021 mtawalia, likiwa ni ongezeko la asilimia 82.

Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi 2024 waliohudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa shida ya magonjwa ya afya ya akili walikuwa 293,952 ikilinganishwa na 246,544 kwa kipindi cha mwaka 2022/23.

Katika kipindi hicho waliolazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya wenye magonjwa ya afya ya akili walikuwa 19,506 ikilinganishwa na 13,262 mwaka 2022/23.

Related Posts