Upinzani walia mapingamizi kukwama | Mwananchi

Dar/mikoani. Vilio vya vyama vya upinzani vimeendelea kusikika vikidai kuenguliwa kwa wagombea wao kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Baadhi ya wagombea wa vyama hivyo

wamewasilisha mapingamizi na kuenguliwa tena huku wengine wakidai kushindwa kufanya hivyo baada ya ofisi za wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo kufungwa.

Hatua hiyo, imelalamikiwa na vyama vya siasa vya upinzani huku vikiitaka Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuwatendea haki ili kuhakikisha mchakato mzima wa uchaguzi kabla na baada unakuwa huru na wa haki.

Tayari vyama vya upinzani vimemuangukia barua Rais Samia Suluhu Hassan, vikimuomba kuingilia kati kuhusu kuenguliwa wagombea wao. Uchaguzi huo utahusisha vijiji 12,333,  vitongiji 64,274 na mitaa 4,269.

Awali, kilio cha wapinzani kilisikika Novemba 8, 2024 siku ya uteuzi baada ya  maeneo mbalimbali hawakuteuliwa.

Hata hivyo, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliitisha mkutano na waandishi wa habari, Dodoma na kutoa maelekezo.

Mchengerwa alisema kuna siku mbili za kupokea changamoto na malalamiko (pingamizi za uteuzi) mbalimbali kupitia taratibu ambazo wagombea wanatakiwa kuzifuata endapo hawajaridhika.

Siku hizo kwa mujibu wa Tangazo la Uchaguzi huo ni Novemba 8-9, 2024 na Novemba 8-10 ni uamuzi wa pingamizi kuhusu uteuzi.

Novemba 10-13 ni kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa pingamizi la uteuzi.

Hata hivyo, vyama vya upinzani vimelalamikia maeneo mbalimbali kushindwa kuwasilisha pingamizi hizo.

Vimedai sababu ya kushindwa ni ofisi za wasimamizi wasaidizi kufunga ofisi na hata yale waliyosiwasilisha bado wagombea wao wameenguliwa.

Baada ya malalamiko hayo ya ofisi kufungwa na mengine, Mwananchi imezungumza na Katibu Mkuu Tamisemi, Adolf Ndunguru ambaye amesema ofisi zikifungwa changamoto hiyo inatakiwa kutatuliwa ndani ya mfumo wa uchaguzi (ngazi ya juu) na kutoa majibu.

“Ukikuta ofisi imefungwa, kwenye mtaa kuna msimamizi juu yake anaitwa mtendaji kata na anamsimamizi juu yake, mkurugenzi na kuna mkurugezi mkuu juu yake Ras na wanakuja kwa katibu mkuu, kwa hiyo wanatakiwa kuzingatia mchakato tu,” amesema.

Amesema kupitia mfumo huo wametatua mapingamizi mengi kama ofisi zimefungwa na mtu hapatikani na mifumo iko wazi huku akiwataka watu kukaa ofisini.

“Hakuna michakato na kama inashindikana wanatakiwa kupiga simu si lazima waandike barua tuko tayari kujibu changamoto zao masaa 24 na wenye shida wanawasiliana na mtendaji mkuu wa Tamisemi na hao unaowataja namba za mtendaji wanazo,” amesema.

Wakati Tamisemi ikieleza hayo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla naye amesema ni muhimu vyama vya upinzani kutambua mapingamizi yanahusu vyama vyote hata CCM imewekewa mapingamizi.

“Mapingamizi ni kwa vyama vyote hata CCM imewekewa mapingamizi, tusiangalie upande mmoja. Rai yetu Tamisemi itende haki kwa vyama vyote,” amesema Makalla, alipozungumza na Mwananchi.

Vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo Mkoa wa Kilimanjaro, vimesema wagombea wao zaidi ya 1,000 wasioteuliwa wameshindwa kuwasilisha mapingamizi yao.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema ni muhimu Tamisemi wafungue njia mbadala ya kuwasilisha mapingamizi yao kwa njia ya kidijitali ili waweze kuteuliwa.

“Iwapo Tamisemi wanataka uchaguzi huru na wa haki, kama Waziri Mchengerwa alivyosema, wafungue njia mbadala ya kuwasilisha pingamizi zetu kwa njia ya kidijitali, ambazo zinaweza kuwasilishwa kwa wasimamizi husika,” amesema Mrema.

“Vinginevyo, itaonekana kuna mpango wa makusudi wa kuzuia rufaa zetu. Pia, tumetuma barua kwa makatibu tawala katika maeneo yote ambayo wagombea wetu waliondolewa. Kama hawawezi kusaidia, tunaweza kutafuta njia nyingine,” amesisitiza Mrema.

Alitolea mfano Manispaa ya Iringa, akisema wagombea wao wote waliopitishwa wameenguliwa.

“Inashangaza wameenguliwa kutokana na pingamizi zilizowekwa na wagombea wa CCM,” amesema.

Mrema amesema wasimamizi wa uchaguzi wameshindwa kubandika fomu za wagombea hadharani, kama kanuni zinavyotaka, hivyo kuwaacha wakihoji ni kwa namna gani wagombea wa CCM waliweza kupata na kuwasilisha pingamizi dhidi ya wateule wa chama chao.

“Hii inatuma ujumbe kwetu kwamba CCM ina mkakati wa makusudi unaofanya kazi kwa karibu na wasimamizi wa uchaguzi kupata fomu za wagombea wa vyama vingine na kuweka pingamizi dhidi yao,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la vijana Chadema Mkoa wa Kilimanjaro (Bavicha), Lemburus Mchome amesema majimbo mawili ya Same Mashariki na Magharibi  wagombea  900 wameshindwa kupeleka mapingamizi yao tangu jana kwenye ofisi za wasimamizi wasaidizi baada ya kukuta ofisi zimefungwa.

Mwenyekiti wa Bavicha, Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya amesema licha ya Mbeya Mjini wagombea wao kupita, lakini maeneo mengine wameenguliwa bila sababu za msingi kulingana na kanuni za uchaguzi.

Amesema Wilaya za Kyela, Chunya, Busokelo na Mbeya Vijijini, wagombea wao waliengulia na tayari Chadema imewasilisha mapingamizi ili warejeshwe na iwapo hawatatendewa haki, watakata rufaa.

Kilio kama hicho kimetolewa na Mjumbe wa Halmashauri ya ACT Wazalendo Taifa, kupitia Kanda ya Kaskazini, Ally Mdimu ambaye amesema wamejitahidi kupeleka mapingamizi lakini wamekutana na changamoto ikiwamo wasimamizi wasaidizi kutokuwepo ofisini na maeneo mengine.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema wagombea wao wengi wameenguliwa, hivyo kumtaka Waziri Mchengerwa kuhakikisha wanarejeshwa.

“Agosti 8 na 9, ACT-Wazalendo tuliwasilisha pingamizi kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi. Mapingamizi yetu kwa kiasi kikubwa yametupiliwa mbali,” amesema Ado.

“Tumefanikiwa katika kesi mbili tu za Kanda ya Kaskazini na chache za Kigoma Mjini, lakini kila mahali pingamizi zetu zilitupiliwa mbali,” amesema na kuongeza hatua yao inayofuata ni kuwasilisha rufaa kwa Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS).

Pia, amemtaja kiongozi wa chama chao, Dorothy Semu kumjulisha Rais Samia kuwa wagombea wao hawakuenguliwa kwa sababu za kisheria, bali kwa sababu za kisiasa, kwa kuwa wizara inayosimamia Serikali za mitaa iko chini ya Ofisi ya Rais.

Ado amesema bado hawana hesabu kamili ya wagombea walioenguliwa nchi nzima, ikizingatiwa mchakato unaendelea,”tunatarajia kuwa na nambari sahihi kufikia kesho.”

CUF: Tunaendelea kupambana

Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya amesema licha ya kuwasilisha mapingamizi yao lakini wameenguliwa tena kwa mara ya pili kwa madai hawajui lugha ya Kiingereza na wanaendelea kupambana ngazi inayofuata.

“Wagombea wetu hawajui lugha ya Kiingereza mbona inakizana na sheria yetu kwanza si lugha yetu inakuwaje mgombea anaenguliwa hajui Kiingereza, wagombea wetu wengi wameenguliwa kwa sababu hiyo,” amesema.

Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi huo, kifungu cha 15(c) kinachoelezea sifa za mgombea, miongoni mwa sifa hizo awe ana uwezo wa kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.

Sakaya amesema wamewaeleza tena wagombea wao kuandika barua kupinga uamuzi huo kwakuwa kanuni haisemi lazima ujue lugha ya Kingereza uweze kuchaguliwa au kuwa mgombea.

“Nimepigiwa simu kutoka Chemba na Kondoa mkoani Dodoma kwenye kata ya Soya na zingine tatu ambazo wagombea walienguliwa wote hawajarudishwa baada ya kupeleka mapingamizi yao yao mara ya pili jana (juzi) lakini leo (Jana) majina yao yameenguliwa tena,” amesema.

Sakaya hadi muda huo anazungumza na Mwananchi leo Jumapili 12:06 mchana amedai anafuatilia kujua na maeneo mengine nchini kujua hali ikoje huku akieleza asilimia 70 ya wagombea wao walienguliwa.

“Mfano Mtwara Mjini tuliweka wagombea vitongoji 57, tulienguliwa vitongoji 28,Mtwara Vijijini tuliweka wagombea vitongoji na vijiji vyote tumeenguliwa na kubaki vitongoji 12 ni asilimia 70 tumeenguliwa,” amesema.

Amesema baada ya kuenguliwa kwa mara ya pili wamewaelekeza wakate rufaa kwenda kwa kamati ya wilaya ambayo mwenyekiti wake ni katibu tawala wilaya huku akieleza kama wataenguliwa tena watakuja na maamuzi mazito.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi (Bara), Joseph Selasini ametaja maeneo ambayo wagombea wao waliwekewa mapingamizi kuwa ni Kigoma  Vijijini, Buhigwe, Mwambwe, Buyungu, Bihalamulo, Muleba, Ukerewe, Magu, Morogoro na Ruvuma.

Amesema katika maeneo hayo sehemu waliyohangaika kuwasilisha rufaa zao ni Kibamba kumtafuta mtendaji walitumia muda mrefu hadi kuja kumpata na kufanikiwa kuwasilisha.

“Dar es Salaam tuliwekewa pingamizi Kibamba, Ubungo na tumekata rufaa tunasubiri zijibiwe wakienguliwa tutachukua hatua nyingine kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi,” amesema.

Naye Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo amesema wagombea wa chama hicho waliteuliwa na wasimamizi wa uchaguzi isipokuwa mapingamizi wamewekewa na wagombea wa CCM.

“Tunapambana kukata rufaa lakini kwenye uteuzi wameteuliwa wote kwa upande wetu, tunajitahidi kujibu rufaa za wagombea wenzetu kutoka CCM,” amesema.

Imeandikwa na Tuzo Mapunda (Dar), Janeth Joseph (Kilimanjaro), Saadam Sadick (Mbeya).

Related Posts