Warundi wamo, sasa ni nchi tano Guru Nanak

DEREVA kutoka Burundi, Imtiaz Din na msoma ramani wake Allen Rukundo ndiyo ingizo jipya katika mbio za magari za Guru Nanak zitakazofanyika Arusha Novemba 16 na 17 mwaka huu.

Uthibitisho wa madereva hawa kutoka Burundi unaifanya Guru Nanak Rally kuwa ni mashindano yatakayoshirikisha nchi tano za Afrika Mashariki wakiwemo wenyeji Tanzania.

Kwa mujibu afisa mawasilkiano wa klabu ya mbio za magari Arusha, Janeth Lyatuu, nchi ambazo madereva wake wamekwishathibitisha kushiriki ni Kenya na madereva wanne, Uganda wawili na Zambia ambayo itakuwa na mwakilishi mmoja.

 Hadi kufikia mwishoni mwa juma, majina makubwa yaliyothibitisha kushiriki ni pamoja na Yassin Nasser na Ally Katumba kutoka Uganda, Ian  Duncan, Azhar Anwar na Ravi Chana kutoka Kenya wakati kutoka Zambia atakuwepo Dave Sihoka.

Timu ya madereva wanne kutoka timu ya Harri Singh ya Moshi ambayo itaongozwa na Guljit Dhani, pia  ni miongoni mwa majina makubwa yanayotegemewea kuzing’arisha mbio za Guru Nanak, ambazo pia ni raundi ya nne na ya mwisho ya ubingwa mbio za magari kitaifa.

Lyatuu anaamini kuwepo kwa zaidi ya magari 25 kutoka ndani na nje ya Tanzania kunafaifanya raundi ya nne kuwa bora kuliko zote zilizowahi kufanyika nchini kwa mwaka huu.

Kutoka magari saba katika mchezo wa ufunguzi wa msimu mjini Tanga  hadi kufikia zaidi ya magari 25 ni hatua kubwa na kwa mujibu wa waandaji klabu ya mbio za magari ya Arusha (AMSC) raundi ya nne siyo tu  imeshirikisha idadi kubwa ya madereva bingwa bali pia inakuja na magari mengi ya kisasa yaliyopasishwa  kwa mchezo wa mbio za magari  na chama cha kimataifa cha mchezo huo, FIA.

Madereva mahiri kutoka Dar es Salaam kama Randeep Birdi, Manveer Birdi na Harinder Deere  waliofanya vizuri raundi tatu za awali Tanga, Iringa na Morogoro pia wamethibitisha kushiriki.

Wengine waliothibitisha  ni timu ya Amapiano kutoka Dar es Salaam inayoundwa na Ethan Taylor, Isack Taylor, Charles Bicco na David Matete.

Mbio za magari za Guru Nanak  zitakimbiwa katika umbali wa kilometa 217 wakianza na kilomita 67 siku ya kwanza na kumaliza na kilomita 150 siku ya pili, Novemba 17.

Related Posts