Yanga, Mualgeria kuna kitu | Mwanaspoti

YANGA haitanii, kwani kwa sasa inadaiwa ilikuwa hatua ya mwisho ya kumtema aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi na hivi unavyosoma tayari imeanza mchakato wa kumnasa kocha kutoka Algeria, Kheireddine Madoui wa CS Constantine ambao ni wapinzani wa Simba katika michuano ya CAF msimu huu

Yanga inamtaka kocha huyo aliyewahi kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2013-2014 akiwa na ES Setif ya Algeria na kubeba pia Caf Super Cup msimu uliofuata, wakiamini ni mdadala sahihi wa Gamondi ambaye walikuwa katika mazungumzo ya mwisho ya kila mmoja ashike lake baada ya Yanga kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara na sababu nyingine zinazoelezwa ni za ndani ya klabu baina ya pande hizo mbili.

Licha ya uongozi kuto kuweka wazi ndoa yao na Gamondi imevunjika, mwenyewe tayari ameondoa utambulisho wa kuwa kocha mkuu wa Yanga katika akaunti zake za mitandao ya kijamii ikiwamo wa Instagram na inaelezwa ameondoshwa kutokana na vitu vingi lakini mwenendo mbaya wa timu yake kwenye mechi mbili za mwisho umetajwa kuwa sehemu ya sababu za kuondolewa.

Mbali na Gamondi, taarifa za ndani zinasema hata Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine Mzambia aliyetokea TP Mazembe misimu miwili iliyopita huenda naye akaonyeshwa mlango wa kutokea ndani ya timu hiyo kutokana na uwepo wake kushindwa kuongeza kitu ndani ya klabu hiyo, inaelezwa.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kimeliambia Mwanaspoti, ni kweli wamemalizana na Gamondi na taarifa kuhusu kocha mpya mchakato unaendelea na bado hawajamalizana naye lakini kuna asilimia kubwa ya kumnasa kutokana na mafanikio aliyonayo.

“Ishu ya kocha Gamondi imemalizika na tayari mchakato wa mbadala wake upo kwenye hatua nzuri za kumalizana naye, muda wowote kuanzia sasa mambo yakiwa tayari taarifa zitatolewa na timu itaendelea na maandalizi kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kipindi hiki mambo mengi yatazungumzwa kuhusu kuondolewa kwa Gamondi lakini uamuzi uliofanyika ni sahihi na utaleta afya ndani ya timu kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wetu kuziweka wazi, tunaheshimu makubwa aliyoyafanya na amekuwa kocha ambaye ameandika rekodi nzuri.”

Akizungumzia suala la Mtendaji Mkuu alisema pia lipo kwenye mchakato linajadiliwa haitaji kuliweka wazi zaidi, lakini mchakato wa kuzungumza naye unaendelea na wakimalizana wataweka wazi kama ataendelea kuwepo au ataondoka na kupisha mwingine.

Madoui ni kocha wa kisasa anayependelea zaidi kutumia mfumo wa mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji watatu na mshambuliaji mmoja (4-2-3-1) ambao kwa sasa Yanga umetumika na makocha walioipa mafanikio timu hiyo misimu mitatu mfululizo.

Kocha huyo anatarajia kutua Yanga akitokea CS Constantine, inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Algeria ikicheza mechi nane na kukusanya pointi 15, ikishinda nne sare tatu na kipigo kimoja, huku kwa mechi za kimataifa za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu amecheza zote nne na kuitinga makundi ikipangwa Kundi A pamoja na Simba, Bravos do Maquis ya Angola na CS Sfaxien ya Tunisia.

Madoui kwenye rekodi ya mataji ameshinda kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja, Super Cup kachukua mara moja, ametwaa mataji mawili Ligi Kuu ya Algeria na Algeria Super Cup pia mara mbili, kuonyesha kuwa sio kocha mwenye Cv ndogo hasa akiungana na Yanga ilipopo Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na Al Hilal ya Sudan, MC Alger ya Algeria na TP Mazembe.

Related Posts