KAMA usingizi ambao mashabiki wa Simba wanaupata, basi ni hivi sasa ambapo mambo ndani ya chama lao yanaonekana kuanza kuwaendea vyema, huku kwa watani zao, Yanga kukiwa hakujatulia kufuatia kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Tabora United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Lakini, wakati mambo yakiwa hivyo, nyota mpya wa Wekundu wa Msimbazi, Jean Charles Ahoua ameingia katika anga za kiungo mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzengeli ambapo utamu wote upo katika namba na maisha ya uwanjani.
Iko hivi, kiungo huyo wa Simba ameifikia rekodi iliyowekwa na nyota wa Yanga, Maxi Mpia Nzengeli katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwenye michezo 10 ya mwanzo, huku wakitoka kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu ‘MVP’ katika timu walizotoka.
Ahoua aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Stella Club Adjame ya kwao Ivory Coast, katika michezo 10 ya Ligi Kuu Bara na kikosi hicho, amefunga mabao matano na kuchangia manne ‘asisti’, sawa na Maxi aliyefanya hivyo msimu wa 2023-2024 ukiwa ni kwanza kwake akiwa na Yanga.
Nyota huyo aliyewahi kuzitumikia timu za LYS Sassandra na Sewe Sports kabla ya kukipiga Stella, alikuwa mchezaji bora wa Ligi ya Ivory Coast msimu uliopita baada ya kuhusika na mabao 21 ya timu hiyo, akifunga 12 na kuchangia tisa ‘asisti’.
Kwa upande wa Maxi ambaye pia alikuwa mchezaji bora wa msimu ‘MVP’ wa Ligi ya DR Congo msimu wa 2020-2021, msimu wake wa kwanza na Yanga akitokea AS Maniema Union, katika michezo 10 za mwanzo za Ligi Kuu Bara alihusika na mabao tisa sawa na Ahoua.
Msimu wake wa kwanza wa 2023-2024 akiichezea Yanga, Maxi anayemudu kucheza kwa ufasaha nafasi ya kiungo mshambuliaji akitokea upande wa kushoto, kulia au hata katikati, katika michezo 10 ya mwanzo na kikosi hicho alifunga mabao saba na kuchangia mawili yaani asisti kuonyesha kuwa namba zake zimelingana na Ahoua ambaye ana moto mkali kwa sasa akiwa na Simba.
Katika msimu huo, Maxi alimaliza na mabao 11 ya Ligi Kuu Bara akiwa katika kiwango bora na kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na hadi sasa ukiwa ni msimu wake wa pili na kikosi hicho amefunga mabao matatu kwenye michezo 10, iliyocheza akiachwa mbali na Ahoua.
Nyota mwingine ambaye alipotoka alikuwa MVP ni kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki aliyejiunga na Yanga akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast msimu wa 2021-2022 ambapo yeye msimu wake wa kwanza hakuwa na makali yoyote.
Katika msimu wa 2022-2023, mechi zake 10 za kwanza akiwa na Yanga alifunga mabao mawili tu ya Ligi Kuu Bara akiwa hana ‘asisti’ na safari yake iliendelea vyema kwani alimaliza na mabao tisa na kukiwezesha kikosi hicho kutetea tena ubingwa msimu huo.
Msimu uliofuata wa 2023-2024, kwa maana uliopita, ndio ulikuwa mzuri zaidi kwa nyota huyo raia wa Burkina Faso kwa sababu alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 21 na kutoa asisti nane na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu yaani ‘MVP’.
Tuzo nyingine alizochukua ni ya kiungo bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kuwashinda, Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC na Kipre Junior aliyejiunga na MC Alger ya Algeria, huku nyota huyo akiingia katika kikosi bora cha msimu.
Nyota mwingine anayeingia katika kundi hili ambaye alikuja Tanzania akitokea kuwa MVP ni Pacome Zouzoua wa Yanga ambaye naye alijiunga na timu hiyo msimu wa 2023-2024, akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, ambapo msimu mmoja nyuma alikuwa mchezaji bora na kikosi hicho.
Nyota huyo aliyeanza maisha yake ya soka katika timu ya vijana ya Williamsville Athletic Club ya kwao Ivory Coast kisha kujiunga na AC Sparta Prague B ya Jamhuri ya Czech, akiwa na ASEC alifunga mabao saba na kuchangia manne kwa msimu huo.
Msimu huo Pacome aliyechezea timu mbalimbali za, SC Gagnoa, Daugavpils, Africa Sports kabla ya kutua ASEC msimu wa 2021-2022, aliwashinda Aubin Kramo aliyewahi kuichezea Simba na Mohamed Zougrana anayeichezea kwa sasa MC Alger ya Algeria.
Katika michezo 10 ya mwanzo ya Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga, Pacome alifunga mabao manne na kuchangia moja tu ‘asisti’, akionekana kushuka, ambapo kwa msimu wa 2023-2024 alimaliza na mabao saba baada ya kuandamwa na majeraha huku msimu huu akifunga mawili tu hadi sasa.
Beki wa Simba, Che Malone Fondoh ‘Ukuta wa Yericko’ alishinda pia tuzo ya mchezaji bora wa msimu (MVP) akiwa na Cotton Sports FC ya kwao Cameroon iliyochukua ubingwa msimu wa 2022-2023 na kuwavutia mabosi wa Msimbazi waliomsajili msimu wa 2023-2024.
Licha ya Malone kucheza beki wa kati, ila msimu wake wa kwanza alifunga bao moja la Ligi Kuu Bara na hadi sasa amefunga mawili na kukiwezesha kikosi hicho chini ya Kocha, Fadlu Davids kuongoza msimamo kwa pointi 25, baada ya kucheza michezo 10.
Akizungumzia kiwango cha Ahoua msimu huu Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema hadi sasa ameonyesha uwezo mkubwa ambao umesaidia timu hiyo kufika ilipo, ingawa bado anapaswa kuongeza juhudi ili kwa pamoja watimize malengo waliyojiwekea.
“Naamini katika ushirikiano katika timu ndio maana licha ya kufanya vizuri ila kuna wengine waliosababisha yeye kufanya hivyo, tupo katika mstari mzuri na siwezi kumpa sifa peke yake bali ni wachezaji wote kutokana na mchango wao kikosini.”
Nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ alisema ubora wa wachezaji wa nje umesaidia kuongeza thamani ya Ligi yetu na kama haitoshi umeongeza pia ushindani wa nafasi na kuwaamsha nyota wazawa waliokuwa wamebweteka.
“Ukiangalia wachezaji wengi wa kigeni sio kwamba wameleta tu manufaa katika timu zao bali hata kukuza uchumi wa nchi kwa sababu wanalipia vitu vingi vinavyosaidia kuongeza pato la taifa, pia imeongeza sana mvuto wa Ligi yetu kutazamwa nje.”