China, Urusi lazima zipambane na udhibiti wa Marekani – DW – 12.11.2024

Moscow na Beijing zimeimarisha mahusiano yao ya kijeshi na ulinzi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine miaka mitatu iliyopita, huku Rais Xi Jinping akiwa mshirika muhimu wa Vladimir Putin kwenye jukwaa la kimataifa.

Hata hivyo, China imejikuta kati ya ushirikiano unaokua kati ya Urusi na Korea Kaskazini, ambayo pia imepeleka wanajeshi Ukraine na kuridhia mkataba wa ulinzi na Moscow wiki hii.

Akizungumza na Wang mjini Beijing, Shoigu, katibu wa Baraza la Usalama la Urusi, almesisitiza umuhimu wa China na Urusi kukabiliana na sera ya Marekani na washirika wake ya kuzidhibiti nchi hizo.

Ameutaja ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Urusi kuwa mfano wa ushirikiano kati ya madola makuu katika dunia ya leo.

“Sisi siyo muungano wa kijeshi na kisiasa kama ile iliyoundwa enzi za Vita Baridi – Mahusiano kati ya nchi zetu ni bora zaidi kuliko aina hizo za mahusiano baina ya mataifa,” alisema Shoigu.

“Mahusiano kati ya Urusi na China yanategemea misingi ya kuheshimiana, usawa, uaminifu, kutokujihusisha na mambo ya ndani ya kila mmoja, na kusaidiana katika masuala muhimu,” aliongeza.

Soma pia: Putin aonya dhidi ya majaribio ya kuishinda Urusi

Shoigu alikuwa waziri wa ulinzi wa Urusi katika miaka miwili ya kwanza ya vita dhidi ya Ukraine, lakini alihamishiwa kwenye Baraza la Usalama baada ya kushindwa kijeshi mara kadhaa na kukosolewa na waandishi wa habari wa kijeshi nchini Urusi.

Anatarajiwa kuhudhuria maonyesho ya anga ya China wiki hii, ambapo ndege ya kisasa zaidi ya Urusi, Su-57, itafanya maonyesho ya kuruka.

Urusi | Sergei Shoigu
Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa la Urusi Sergei Shoigu yuko Beijing kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi.Picha: Mikhail Klimentyev/Russian President Press Office/dpa/picture alliance

China imejitangaza kama mshirika asiyeegemea upande wowote katika vita vya Ukraine na inadai haijatoa msaada wa kivita kwa upande wowote, tofauti na Marekani na mataifa ya Magharibi.

Hata hivyo, imeendelea kuwa mshirika wa karibu wa kisiasa na kiuchumi wa Urusi, na mwezi uliopita mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo waliahidi kuimarisha ushirikiano wao wa kijeshi.

Uhusiano kati ya Urusi na China unalenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kisiasa, huku maonyesho ya anga ya China yakiwa fursa muhimu kwa nchi hizo kuonyesha uwezo wao wa kijeshi.

Ushirikiano huu unaendelea wakati China ikijaribu kudumisha msimamo wake wa kutoegemea upande wowote kwenye mgogoro wa Ukraine.

Dmitry Medvedev, rais wa zamani wa Urusi, amewashutumu viongozi wa Ulaya kwa kuchochea mzozo wa Ukraine baada ya Donald Trump kuchaguliwa tena.

Medvedev ameonya dhidi ya kuruhusu Kyiv kutumia makombora ya masafa marefu ya Magharibi kulenga maeneo ndani ya Urusi.

Mkuu ajaye wa sera ya kigeni EU asisitiza kuisaidia Ukraine

Kaja Kallas, aliyeteuliwa kuwa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, aliwaambia wabunge wa Umoja huo kuwa Umoja wa Ulaya lazima uunge mkono Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi “kwa muda wote utakaohitajika.”

Akisisitiza hali ngumu kwenye uwanja wa vita, Kallas alisema Umoja wa Ulaya unapaswa kuendelea kutoa msaada wa kijeshi, kifedha, na kibinadamu ili kusaidia Ukraine kupambana na Urusi.

Soma pia: Mkuu wa sera za Kigeni ajae EU anamtazamo upi kuhusu Israel

Kallas, ambaye alikuwa waziri mkuu wa Estonia, anatarajiwa kuthibitishwa kuwa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, akimrithi Josep Borrell.

Kallas, mkosoaji mkali wa Urusi, alieleza kuwa msaada wa Umoja wa Ulaya kwa Ukraine lazima uwe na njia wazi kwa Ukraine kujiunga na Umoja huo.

Alionya kuwa mgogoro huo unahusu usalama wa Ulaya na kanuni za Ulaya, na hivyo ni muhimu kusaidia Ukraine kupata njia ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Kaja Kallas
Mkuu ajaye wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas ni mkosoaji mkubwa wa Urusi na rais Vladmir Putin.Picha: European Council

Mnamo Juni, Brussels ilifungua mazungumzo ya kujiunga kwa Ukraine, jambo ambalo Urusi imekuwa ikijaribu kuzuia.

Uteuzi wa Kallas umekuja wakati ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakabiliwa na ukaguzi wa wabunge, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa wiki moja wa kusikilizwa.

Kallas ni mmoja wa makamu sita walioteuliwa kwenye Tume mpya ya Ulaya chini ya uongozi wa Ursula von der Leyen.

Ikiwa atathibitishwa, Kallas atakuwa na jukumu muhimu la kuendelea kuimarisha sera za kigeni za Umoja wa Ulaya, hususan kuhusu mzozo wa Ukraine.

Umoja wa Ulaya tayari umetoa karibu dola bilioni 125 kusaidia Ukraine tangu uvamizi wa Urusi mwaka 2022, wakati Marekani imetoa karibu dola bilioni 90, kulingana na taarifa kutoka Kiel Institute.

Soma pia: Waziri Mkuu wa Estonia asema hatonyamazishwa na Urusi

Katika kuendelea kwa uungwaji mkono huo, Josep Borrell, mkuu wa sasa wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, alisisitiza msaada “usioyumba” wa Umoja wa Ulaya kwa Ukraine kwenye ziara yake ya kwanza nchini Ukraine tangu Donald Trump kushinda uchaguzi wa Marekani.

Hata hivyo, uchaguzi wa Trump umewatia wasiwasi baadhi ya viongozi wa Ukraine na Ulaya, kwani wanasubiri kuona kama atadumisha msaada wa Marekani kwa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya Urusi.

Hofu ni kwamba Trump anaweza kusitisha msaada wa kijeshi na kifedha kwa Ukraine, jambo ambalo linaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa nchi hiyo kupambana na uvamizi wa Urusi.

Chanzo: Mashirika

 

Related Posts