Dar/Dodoma. Wakati Polisi Mkoa wa Dodoma ikieleza imewakamata watu sita kwa tuhuma za kuharibu miundombinu ya reli ya kisasa (SGR) na wanne wameshafikishwa mahakamani, wadau wameshauri hatua za kuchukua kudhibiti uharibifu huo.
Akizungumzia uharibifu wa miundombinu ya SGR, wakili Dk Onesmo Kyauke ameeleza kupungua uzalendo miongoni mwa Watanzania ni chanzo cha kuhujumu miundombinu hiyo.
“Tulitarajia raia wangekuwa walinzi wa maendeleo haya,” amesema akisisitiza umuhimu wa elimu ya umma kuhusu umuhimu wa kulinda mali za kitaifa.
Kwa mujibu wa Dk Kyauke, wananchi, hasa wale wanaoishi karibu na njia za SGR, wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda mradi huo kwa kuwa wanachangia kufadhili miradi hiyo kupitia kodi.
Amependekeza adhabu kali itolewe kwa yeyote atakayepatikana na hatia ya kuharibu miundombinu ya kitaifa, akitaka serikali za mitaa kuanzisha programu za usalama zinazolenga jamii kwa ajili ya kulinda miradi muhimu kama SGR.
“Wanapaswa kuhisi maumivu ya uharibifu wanaousababisha kwa Taifa,” amesema Dk Kyauke alipozungumza na gazeti dada la Citizen mwishoni mwa wiki.
Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Wilhelm Ngasamiaku amependekeza sehemu ndogo ya ada za tiketi itumike kufadhili juhudi za kiusalama kando mwa njia za reli.
“Fedha hizi zinaweza kusaidia juhudi za polisi jamii kufuatilia na kuripoti shughuli zozote za kutiliwa shaka kando ya njia.
“Nchi imewekeza rasilimali nyingi, tunapaswa kuchukua hatua madhubuti kulinda uwekezaji huu. Wanaojihusisha na uharibifu wanachelewesha maendeleo yetu,” amesema.
Mwanasosholojia kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania, Linah Kabula amependekeza kupelekwa polisi kando mwa reli ya SGR.
Amesema polisi walinde maeneo yenye hatari kubwa, huku polisi jamii wasimamie sehemu zenye hatari ndogo.
Novemba 9, 2024 Shirika la Reli Tanzania (TRC), liliagizwa na wabunge kufunga kamera za ulinzi maeneo yote ya reli, ili kukabiliana na watu wanaohujumu miundombinu ya SGR.
Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Miundombinu na Bajeti waliotembelea na kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa SGR walitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Selemani Kakoso alisema kufungwa kamera za ulinzi (CCTV) kutawezesha kukabiliana na hujuma kwa mradi huo.
Walitoa kauli hizo ikiwa zimepita siku nne tangu TRC kupitia mkurugenzi wake mkuu, Masanja Kadogosa kueleza kuna njama zinazofanywa kuhujumu mradi huo ili kuonyesha haufai.
Treni ya SGR kwa nyakati tofauti safari zake zimekuwa zikipata hitilafu za mara kwa mara, jambo linalosababisha watu kukwama wakiwa katikati au kuchelewa kuanza safari wanapokuwa stesheni.
Akizungumza na Mwananchi Novemba 5, mwaka huu Kadogosa alisema kuna njama zinazofanywa kwa lengo la kuhujumu mradi huo.
Alisema hujuma hizo si za hivi karibuni, bali zimeanza muda mrefu akieleza baadhi ya wahusika wamekamatwa ambao wako mbioni kuchukuliwa hatua.
“Hatua dhidi yao zinaendelea, watakapohukumiwa wananchi watawafahamu,” alisema.
Safari ya kwanza ya treni ya umeme ilianza Juni 14, 2024 kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro, ikiwa na mabehewa 14 yaliyojaa. Julai 25, 2024 treni hiyo ilianza safari za Dar es Salaam hadi Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye aliyeizindua.
Kamanda wa Polisi MKoa wa Dodoma, George Katabazi akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Novemba 12, 2024 amesema kati ya watu sita, wanne wameshafikishwa mahakamani.
Amewataja wanaoshikiliwa mpaka sasa ni Said Sempinga (39) na Michael Robert (44), wakazi wa Kilosa mkoani Morogoro, akieleza uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Amesema Oktoba 10, 2024 saa 5.00 usiku katika Kijiji cha Msagali wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma watuhumiwa wanadaiwa kukata na kuiba waya wa shaba kutoka katika madaraja matatu ya reli ya SGR.
“Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilipata taarifa na kuanza uchunguzi wa tukio mara moja kwa kushirikiana na wananchi na kuwakamata watuhumiwa kwa nyakati tofauti wakiwa na nyaya za shaba walizoiba kutoka kwenye reli ya umeme (SGR)” amesema.
Kamanda Katabazi amesema uchunguzi wa tukio hilo bado unakamilishwa, ili taratibu nyingine za kisheria zifuatwe.
Amesema Oktoba 8, katika maeneo ya Bahi Sokoni wilayani Bahi, mkoani Dodoma waliwakamata watuhumiwa wanne kwa nyakati tofauti wakidaiwa kuharibu na kuiba miundombinu ya serikali kwa kukata nyaya za shaba katika mradi wa SGR wilayani Bahi.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Kipambwe (38), Petro Yassi (22) Michael Leyaseki (27) na Issa Misami (42) ambao wameshafikishwa mahakamani.
Wakati polisi wakieleza hayo, Novemba 10, zilisambaa picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha baadhi ya watu wakiwa wamekamatwa na nyaya za umeme, nyavu za uzio na betri za kuongeza umeme katika reli hiyo.
Picha hizo pia zilionyesha nyaya zinazopitisha umeme wa kuendeshea treni ya SGR zikiwa zimekatwa.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam leo Novemba 12, Ofisa Habari wa Wizara ya Uchukuzi, Jacob Kipara amesema picha hizo wanazifahamu.
“Picha mnazoziona mtandaoni ni kweli hao watu tuliwakamata na tuliwaonyesha wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge za Miundombinu na Bajeti kutokana na jitihada tulizofanya za ukamatwaji wa watu hao na tuliamua kuziachia kwa jamii,” amesema.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na reli ya SGR wamelalamika kubadilishiwa sehemu za vivuko walivyokuwa wakipita baada ya ujenzi wa reli.
Katika eneo la Chekeleni, mwandishi ameshuhudia baadhi ya maeneo nyavu za uzio wa reli hiyo yakiwa wazi na sehemu nyingine zikiwa zimekatwa, kisha kufanyiwa matengenezo, huku mvua ikiathiri maeneo mengine.
Wamesema kuna wakati hulazimika kukatiza kwenye reli ili kuwahi maeneo ya karibu, ikiwemo shule na maeneo ya kazi wakiwamo wanaotoka Kijiji cha Kikongo kwenda Nungu.
Mwajuma Bakari, mkazi wa Chekeleni amesema eneo la uzio lililokatwa uzio huwawezesha kufika maeneo ya huduma kwa haraka.
“Kutoka hapa Chekeleni hadi upande wa pili ni umbali mrefu ukitumia njia rasmi, lakini tunapovuka kupitia hapa kwenye reli tunaokoa muda. Inasaidia sana hasa kwa wazee na wanafunzi ambao wangetembea mwendo mrefu kufika shuleni,” amesema Mwajuma.
Amedai ni vigumu kwao kuendelea kufuata njia rasmi, kwani zinahitaji kupita njia za mbali zinazoongeza muda wa safari zao.
“Tunajua kuwa reli ni muhimu, lakini Serikali itafute namna nyingine ya kuzuia uhalifu bila kutulazimisha kuzurula mbali kwa njia zisizo za moja kwa moja,” amesema.
Masoud Shoka, mfanyabiashara wa mkaa amesema awali walikuwa wanatumia njia za mkato kufikisha bidhaa zao kutoka kijiji kimoja kwenda kingine na wakati mwingine kupeleka Mlandizi, lakini tangu kuweka kwa uzio wanajikuta wanazunguka barabara ya Mzenga.
“Hapa tunatumia njia tatu, aidha uzunguke hadi kutokea stesheni ya Pugu ambako inabidi kupita jirani na hospitali ya wilaya ya Kibaha, lakini mvua ikinyesha hatuwezi kutumia huko kwa sababu ya utelezi,” amesema.
Dereva wa gari la mchanga, Zawadi Seif amesema malalamiko yanayotolewa ya kuhujumiwa inawezekana, kwa sababu si sehemu zote zimezibwa kwa ajili ya kuzuia watu kupita.
“Kama hapa tunapopita upande wa kushoto na kulia kupo wazi na hakuna ulinzi wa kuzuia watu wasiingie huku juu, hata wanapolalamika uwepo wa watu wanaokata nyaya waangalie na njia zao zipo salama?
“Hatuwezi kutumia fedha kila siku kufika upande wa pili wakati tunaweza kuvuka kwa dakika chache kupitia reli,” amesema mwananchi ambaye hakuwa tayari kutajwa jina.
Jumatatu ya Novemba 3, 2024, usafiri wa SGR ulipata hitilafu katika mfumo wa uendeshaji, hali iliyosababisha ratiba kuvurugika na abiria kukwama katika stesheni tofauti za SGR.
TRC kupitia taarifa kwa umma iliomba radhi kwa abiria wa treni ya mchongoko walioanza safari Dar es Salaam kwenda Dodoma saa 2:00 asubuhi na kusimama ghafla saa 2:20 kati ya Pugu na Soga.
Novemba mosi, 2024, TRC pia iliomba radhi kwa abiria wa treni ya saa 11:15 alfajiri kutoka Dodoma na treni ya saa 3:30 kutoka Dar es Salaam ikijumuisha safari nyingine za siku hiyo.
Novemba 4, 2024 treni iliyotoka Dodoma saa 11:15 asubuhi ilikwama kwa dakika 20 kati ya Pugu na Soga.