MAHAKAMA ya Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi imemtia hatiani Omari Ntauka kwa makosa ya uhujumu uchumi na kusababishia hasara ya Shs. 5,602,100/- kwa kuiba kilogramu 1,855 za ufuta alizokabidhiwa na wakulima katika Tawi la Chilonji kwa msimu wa ufuta 2021/2022 kwa Chama cha Msingi cha Ushirika( AMCOS) cha Rweje .
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba mshtakiwa akiwa Karani wa Rweje AMCOS kwa makusudi alikisababishia hasara Chama hicho cha Msingi.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi Na. 21147/2024 ya Jamhuri dhidi ya Ntauka iliongozwa na Mhe. Neema Mhelela Hakimu Mkazi Mkuu na kusimamiwa na Wakili wa Serikali
Haruna Mchande wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Lindi.
Katika kesi hiyo iliyotolewa hukumu Novemba 11, 2024, Kosa la kwanza ni kuisababishia Hasara Mamlaka kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) ya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 marejeo ya mwaka 2022 .
Kosa la pili ni wizi kinyume na kifungu cha 271 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022,
Mshtakiwa amehukumiwa kwenda jela miaka 22 ambapo katika kosa la kwanza adhabu yake ni miaka 20 na katika kosa la pili mshtakiwa amehukumiwa kwenda jela miaka miwili.
Adhabu hizo zinaenda sambamba na mshtakiwa kulipa hasara ya Sh. 5,602,100/- aliyoisababisha kwa Chama hicho cha Msingi.