Kwenye hili la mauaji, Tume huru itueleze ukweli

Watu wa Zanzibar walipata mshituko mwishoni mwa wiki kwa kusikia taarifa za kuuawa kwa watu wawili na wengine kujeruhiwa katika Kijiji cha Kidoti, kilichopo kaskazini Unguja.

Tukio hilo limekuwa na taarifa za kila aina katika vijiwe, vyombo vya habari, mitandaoni na kutoka Jeshi la Polisi Zanzibar.

Huyu anasema hili, yule anasema lile, yaani kwa muhtasari ukweli hasa haueleweki ni upi. Lakini lisilokuwa na utata ni kwamba watu wawili walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa katika tukio ambalo Jeshi la Polisi lilifyatua risasi.

Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Upelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Zuberi Chembera, ni kwamba askari polisi na vyombo vyingine vya usalama waliokuwa katika operesheni maalumu walikutana na gari la mizigo.

Askari hao walilisimamisha gari ili kulifanyia ukaguzi, lakini dereva hakutii hiyo amri halali na akaongeza mwendo na kupiga honi ovyo. Hapo tena watu waliokuwa wamepakiwa nyuma wakalirushia mawe gari liliokuwa na askari polisi na wa vikosi vyingine vya ulinzi.

Chembera alieleza kwamba hali hiyo ndiyo iliyosababisha askari kufyatua risasi juu (haikuelezwa ni ngapi) ili kumtaka dereva asimame, lakini hakutii amri na watu wengine wakajiunga kuwapopoa askari kwa mawe.

Katika purukushani hiyo gari la mizigo lilipoteza mwelekeo na kugonga mkungu uliokuwa pembezoni mwa barabara. Hapo ndipo yalipomalizika maisha ya dereva Msina Sharif (29) na mwenzake Abdulla Bakari (28), wote wakazi wa Kijiji cha Kidoti.

Vilevile, tumeambiwa na Jeshi la Polisi kuwa hilo gari halikuwa na namba ya usajili.

Kutokana na hali hiyo, Chembera alisema Jeshi la Polisi litaunda Tume huru ili kujua kiini cha tukio hilo lililosabisha watu wawili kuuawa na wengine waliokuwa wanatembea barabarani kujeruhiwa.

Hatua ya Polisi ya kuunda Tume huru kuchunguza tukio zito kama hilo lililosababisha maafa, inafaa kupongezwa, lakini ingekuwa vizuri kwa umma kuelezwa hao wajumbe wa tume watatoka wapi.

Katika jamii, watu wana wasiwasi kwamba hao wajumbe wasije kuwa wanatoka Jeshi la Polisi na vikosi vyingine vya ulinzi au wastaafu wa vikosi hivyo. Hili linafaa kuwekwa wazi.

Jingine ni Polisi ingekuwa imefanya vema kama ingeonyesha picha za hilo gari ili kuwa na uhakika kwamba kweli halikuwa na namba ya usajili na kueleza kilichokuweo katika hilo gari, yaani ni mzigo wa aina gani.

Polisi wameeleza kuwa sababu ya kifo ilikuwa gari kugonga mti. Ni vema maelezo ya uchunguzi wa sababu za kifo yaliyotolewa na madaktari yangewekwa wazi polisi ili umma ufahamu ni yapi, kwa risasi au kwa athari zilizotokana na gari kugonga mti.

 Vilevile, hao waliopata majeraha walipata athari hizo kwa mawe, kuanguka au kwa risasi.

 Suala la risasi kufyatuliwa hewani na Polisi lina historia mbaya Zanzibar, kwani imekuwa kawaida kusikia risasi kupigwa hewani, lakini kwa bahati mbaya zikasababisha vifo.

Mfano ni tukio la kule Micheweni Pemba wakati wa harakati za kuanzisha kwa vyama vingi vya siasa ambapo mtu mmoja aliuawa na wengine kujeruhiwa, mmojawao alipelekwa Hospitali ya Muhimbili na kutolewa risasi mwilini.

Wakati ule, watu waliuliza inakuwaje risasi iliyopigwa hewani ikarudi ardhini na kumpiga mtu? Hakuna maelezo yaliyotolewa juu ya tukio lile mpaka leo.

Sasa kinachosubiriwa na wananchi wa Zanzibar ni maelezo ya kina na Jeshi la Polisi limetoa ahadi ya kufanya hivyo na kuwataka wanachi wawe watulivu.

Polisi imesema itatoa taarifa kamili mapema itavyowezekana juu ya tukio hili la watu wawili kuuawa na wengine, wakiwemo watoto wa shule, kujeruhiwa.

Lakini kubwa zaidi ni kuwepo sio ukweli tu bali na uwazi na hasa katika muundo wa hiyo Tume huru.

Ni vizuri hiyo Tume isiwe na sura ya ule msemo wa Waswahili wa mlalamiakaji Msomali, mwendesha mashitaka Msomali na hakimu ni Msomali.

Kwa mtazamo wangu, itakuwa jambo la busara kwa taasisi za kiraia kama za jumuiya za wanasheria, vyombo vya habari au tasisi yoyote ile ya kiraia isiyokuwa na uhusiano wa kisiasa zikajumuishwa katika uundaji wa hiyo Tume.

Kwa sasa kinachosubiriwa ni kujua nini hasa kiini cha tukio hili la kusikitisha na kutisha. Ni Tume huru ya kweli ndiyo inaweza kutupa ukweli na wao kuendelea kuwa imani na Jeshi la Polisi ama mlinzi imara na muaminifu wa usalama wa raia na mali zao.

Related Posts