Leseni za Madini zaidi ya 50,000 zatolewa

• Maeneo zaidi ya wachimbaji wadogo kutengwa

TUME ya Madini imetoa jumla ya leseni za uchimbaji madini 54,626 katika kipindi cha miaka saba.

Kaimu Mkurugenzi wa Leseni na Tehama Mhandisi Aziza Swedi amesema katika kipindi cha kuanzia 2018/2019 hadi Septemba 30, 2024, Tume ya Madini imetoa jumla ya leseni 54,626 kati ya leseni hizo, leseni za utafutaji wa Madini (Prospecting Licence-PLs) 1,683, leseni za uchimbaji wa kati (Mining Licences-MLs) 144 na leseni za uchimbaji mkubwa (Special Mining Licences-SMLs) tano.

Aidha amesema, leseni za uchimbaji mdogo (Primary Mining Licences-PMLs) zilizotolewa ni 35,536 leseni za uchenjuaji (Processing Licences-PCLs) 216, leseni za usafishaji Madini (Refinery Licences-RFLs) saba, leseni za uyeyushaji Madini (Smelting License’s-SLs) sita, leseni ndogo za biashara ya Madini (Brokers Licences-BLs) 12,273 na leseni kubwa za biashara ya Madini (Dealers Licences-DLs) 4,756.

Amesema, Tume imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo ikiwemo kuwatengenezea mazingira rafiki kwa ajili ya kupata Leseni za uchimbaji pamoja na kuwaunganisha na Taasisi za kifedha ili wapate Mikopo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji

“Hadi kufikia Oktoba, 2024 Tume imefanikiwa kutenga maeneo 65 kwa ajili ya Wachimbaji wadogo katika mikoa mbalimbali yenye shughuli za uchimbaji madini,”amesema Mhandisi Aziza.

Asema, Tume ya Madini imeendelea kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) katika kuyafanyia utafiti maeneo mbalimbali ili kuwawezesha Wachimbaji kupata taarifa za uwepo wa rasilimali madini na kufanya uchimbaji wenye tija.

Mhandisi Aziza amesema ili kuimarisha mfumo wa usimamizi wa utoaji wa leseni, Tume ya Madini imejenga mfumo mpya wa kuboresha uchakataji,usimamizi na utoaji wa leseni za madini.

“Baada ya maboresho yote kukamilika itafuata hatua ya uunganishwaji wa mifumo mingine ya Serikali na uhamishaji wa data kutoka mfumo wa zamani kwenda mfumo mpya pamoja na kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo,”amesema Mhandisi Aziza.

Related Posts