Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imepokea udongo wenye masalia ya mafuta ya marehemu Naomi Orest Marijan, anayedaiwa kuuawa na mumewe Hamisi Luwongo kisha kuuchoma moto mwili wake, kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 44/2023, mshtakiwa Hamisi, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe Naomi, kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Hamisi anadaiwa kumuua mkewe Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili wake kwa moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda na akaenda kuyazika masalia ya mwili huo na majivu shambani kwake na kupanda migomba.
Upande wa mashitaka leo Jumanne, Novemba 12, 2023 umewasilisha mahakamani mchanga wenye masalia ya mafuta ya marehemu Naomi, kupitia kwa shahidi wake wa 12, Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Ofisi ya Makemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Kanda ya Kusini (Mtwara) Hadija Mwema.
Mahakama hiyo imepokea mchanga huo wenye masalia ya mafuta ya marehemu na kuyaorodhesha kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashitaka baada ya kutupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi.
Awali, jopo la mawakili wa utetezi wanaomtetea mshtakiwa hiyo linaloongozwa na Wakili Mohamed Majaliwa limeweka pingamizi furushi hilo la mchanga lisipokewe na kuwa kielelezo cha upande wa mashitaka kwa madai kuwa haikuwa limeorodheshwa katika orodha ya vielelezo vya upande mashitaka.
Mwendesha mashtaka aliyemuongoza shahidi huyo kutoa ushahidi wake, Wakili wa Serikali, Mwasiti Ally amepinga hoja za pingamizi hilo akidai kielelezo hicho kiliorodheshwa kwenye orodha wakati wa usikilizwaji wa awali ( mshtakiwa aliposomewa maelezo ya kesi).
Hata hivyo, Wakili Majaliwa amepinga kuwa kilichotajwa kwenye orodha hiyo na kile shahidi alichoomba kipokewe ni viwili tofauti.
Amefafanua kilichoandikwa kwenye orodha ya vielelezo ni masalia ya mwili wa marehemu lakini shahidi akiwa kizimbani ameomba kutoa mchanga wenye mafuta.
Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi hiyo katika uamuzi wake amesema kuwa masalia ya mwili wa marehemu haina tafsiri nyingine, alifafanua kuwa, masalia ya mwili sio mpaka iwe mifupa tu bali hata mafuta hayo ni sehemu ya masalia ya mwili.
“Kwa hiyo natupilia mbali pingamizi na huo udongo wenye masalia ya mafuta unapokewa,” amesema Jaji Mwanga.
Awali, katika ushahidi wake, Hadija amesema mwaka 2019 alikuwa Meneja Kitengo cha Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dar es Salaam.
Amesema, Julai 24, 2019 alipokea vielelezo na barua kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) iliyomtaka afanye uchunguzi wa vinasaba katika sampuli za vielelezo mbalimbali alivyokabidhiwa.
Vielelezo hivyo matone ya damu yaliyochukuliwa chumbani kwa marehemu, kwenye banda ambamo inadaiwa ndimo mwili wake ulimochomwa moto na kuuteketeza, mchanga uliodhaniwa kuwa na masalia ya mafuta ya binadamu (ya mwilini) na mabaki ya mifupa.
Vingine ni nguo za marehemu, viatu vyake, chanuo vitana alivyokuwa akivitumia, nyembe na mashine za kunyolea kutoka chumbani kwa marehemu mpanguso wa mate wa mtoto wake na wa mshitakiwa na matone ya damu yaliyodhaniwa kuwa ya mshitakiwa.
Amesema baada ya uchunguzi aliandaa ripoti ya uchunguzi wa uhusiano wa chembechembe asili za urithi (DAN) ya Julai 26, 2019 ambayo pia imepokewa na kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka.
Akizungumzia matokeo ya uchunguzi Hadija amesema damu na vielelezo vingine vilionesha kuwa ni mtu wa jinsia ya kike na kingine kilioneaha kuwa kulikuwa na damu ya mtu wa jinsia ya kiume na kwamba udongo ule wenye masalia ya mafuta pia ulionesha kuwa ni mafuta ya binadamu wa jinsia ya kike.
Hata hivyo, amesema vielelezo vingine havikuweza kutoa mpangilio wa uhusiano wa vinasaba kutokana na sababu mbalimbali za kitaalamu.
Hata hivyo, akihojiwa maswali ya dodoso na Wakili Majaliwa, shahidi huyo amesema hakuweza kuwasilisha mahakamani masalia ya mifupa kwa kuwa yalitumika na kuisha yote katika uchunguzi wa mpangilio wa vinasaba.
Pia, amekiri kuwa hawezi kujua kama vielelezo hivyo kweli vilikuwa ni Naomi kwa kuwa wakati vinachukuliwa yeye hakuwepo lakini akasema kuwa alifahamu hivyo kutokana na taarifa zilizokuwa kwenye barua iliyomtaka afanye uchunguzi wa vielelezo hivyo.