Serikali yatoa agizo Latra madai ya wahudumu wa mabasi kunyanyaswa

Dar es Salaam. Serikali imeagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kufuatilia kwa ukaribu madai ya wahudumu wa mabasi kushushwa porini na wamiliki wa vyombo hivyo vya moto.

Hali hiyo imeelezwa hutokana na wahudumu hao kutokuwa na mikataba ya ajira, hivyo huachishwa kazi muda wowote.

Gift Manega, mmoja wa wahitimu wa mafunzo kwa wahudumu wa mabasi amesema wamekuwa wakinyanyaswa, ikiwa ni pamoja na kushushwa kwenye basi pasipo sababu za msingi.

“Wasichana tunadhalilika, upo porini unaambiwa shuka kwenye basi niachie chombo changu, ningeomba Latra pamoja na uongozi kusimamia hilo tuweze kupata mikataba inayostahili tuweze kufanya kazi kwa kujiamini,” amesema.

Amesema mafunzo waliyopatiwa yatawasaidia kupata kipato hivyo kujikimu wao na familia zao.

Agosti 27, 2023 Mwananchi katika ripoti maalumu ilieleza changamoto wanazopitia wahudumu wa mabasi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni kukosekana mikataba ya ajira, unyanyasaji wa kingono na ujira mdogo wanaoupata katika kazi.

Akizungumza leo Novemba 12, 2024 katika hafla ya ugawaji wa kadi kwa wahitimu wa mafunzo ya huduma katika vyombo vya usafiri, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameagiza Latra kusimamia jambo hilo kuhakikisha wanazingatia utaratibu wa utumishi na ajira nchi.

“Lakini hili ninaweza kusema ni aibu kwetu kama Latra mnaweza kuwa na taarifa za mtu mwenye chombo akamshusha muhudumu njiani akaendelea kufanya shughuli zake nadhani inabidi tujitafakari,” amesema.

Kihenzile amewataka Latra kufuatilia na kukomesha vitendo vya namna hiyo kwani havikubaliki duniani wala mbinguni, akihoji mtu akishushwa njia na akidhurika inakuwaje.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mohamed Abdallah amesema hawajapata malalamiko ya manyanyaso ya wahudumu wa mabasi ambao hushushwa kwenye magari lakini yakiwafikia wana jukumu la kuwaita wahusika kuzungumza nao.

“Suala kama hilo halijafika kwetu lakini kama kuna vitendo hivyo, ni unyama mkubwa na haukubaliki, ikitokea tukapata malalamiko tutamwita mmiliki atueleze kwa nini anafanya hivyo,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Latra, Ahmed Mohamed Ame amesema hadi kufikia Oktoba, 2024 wahudumu 750 wamepatiwa mafunzo na wahudumu 174 wamekidhi vigezo na kusajiliwa Latra.

Amesema pamoja na matakwa ya kisheria na kanuni lakini kuna faida za wahudumu kuhudhuria mafunzo na kusajiliwa.

Kwa upande wa wamiliki wa mabasi, amesema wanapata faida ikiwamo wasimamizi mahiri na wenye weledi wa kazi, kuboresha huduma za usafiri ardhini na kurasimisha kazi ya wahudumu iheshimike kama ilivyo kazi nyingine.

Pia, kulinda mitaji ya wamiliki wa vyombo na vipato vya wahudumu, kuwezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazowawezesha kusimamaia masilahi ya wahudumu katika ajira na kuongeza nidhamu na uwajibikaji.

“Kuanzia sasa tutaanza kuchukua hatua dhidi ya wamiliki watakaotumia wahudumu ambao hawajasajiliwa kwani hawataruhusiwa kutoa huduma kwenye mabasi,” amesema.

Kauli hiyo inatolewa ikiwa zimebaki siku 49 za wamiliki kutumia wahudumu ambao hawajasajiliwa na Latra kwani Desemba 31 itakuwa mwisho wa kuwatumia.

Kwa mujibu wa kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413 ya mwaka 2019 Mamlaka ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara.

Kanuni ya 17 ya Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili Wahudumu wa Magari ya Biashara za Latra za mwaka 2020, zinamtaka mtu yeyote anayekusudia kufanya kazi ya uhudumu katika gari linalotoa huduma za usafiri kibiashara kusajiliwa.

Katika hatua nyingine, Kihenzile amesema pamoja na mafunzo mengine Latra, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Biashara na Chuo cha Ufundi cha Arusha waangalie kwa kina mitalaa inayotolewa ili ikiwezekana eneo la huduma ya kwanza lipewe uzito unaostahili.

“Nichukue nafasi hii kwa Jeshi la Polisi wanapofanya ukaguzi wajitahdi kuzingatia kuona kila chombo kina boksi la huduma ya kwanza, kwa sababu tunakagua sana kifaa cha kuzima moto.

“Watu wengi wamekufa kwa sababu ya kupata ajali na kukosa huduma ya kwanza na kwa sababu maarifa ya utoaji huduma ya kwanza si kila mtu anayo,” amesema.

Amesema takwimu ya hali ya ajali katika miaka mitatu tangu 2021 ajali 1,998 walifariki watu 1,245 na majeruhi 2,023.

Mwaka 2022 amesema ajali zilikuwa 1,720, walifariki dunia watu 1,545 na majeruhi 2,278, huku mwaka 2023 ajali zilikuwa 1,733 walifariki dunia 1,947 na majeruhi 2,716.

Kihenzile amesema mwaka 2024 katika ajali zilizotokea Januari hadi Juni ni 872, wamefariki dunia watu 816 na majeruhi 1,216.

Related Posts