Sonko awataka wafuasi wake kulipiza kisasi – DW – 12.11.2024

Kabla ya uchaguzi uliopita wa rais nchini humo, wafuasi wa Sonko ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Pastef, walipambana na polisi mnamo mwezi Machi katika baadhi ya machafuko mabaya zaidi katika historia ya Senegal.

Lakini nchi hiyo imekuwa na utulivu tangu rais mshirika wa Sonko Bassirou Diomaye Faye aliposhinda kura hiyo dhidi ya rais wa wakati huo Macky Sall kwa kishindo. Hata hivyo hivi sasa machafuko yamekuwa yakijitokeza kati ya wafuasi wa vyama vya kisiasa nchini humo katika kipindi cha wiki za hivi karibuni,wakati Senegal ikijiandaa Jumaapili kuingia kwenye uchaguzi wa bunge utakaoamuwa hatma ya viongozi hao,Faye na Sonko katika utekelezaaji wa sera zao.

Soma pia: Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye atangaza kulivunja bunge

Sall afuatilia siasa za Senegal kutoka nje ya nchi

Senegal, Dakar | Rais wa zamani Macky Sall
Rais wa zamani Macky Sall anaongoza muungano mpya wa upinzani kutoka nje ya nchi.Picha: Sylvain Cherkaoui/AP/picture alliance

Kiongozi wa zamani wa Senegal Macky Sall, anaongoza muungano mpya wa upinzani kutoka nje ya nchi, na kuzua maswali juu ya nia ya kurejea kwake katika uwanja  wa kisiasa na inaweza kuwa na maana gani kwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Chama cha Pastef kinashindana na vyama tawala vya zamani ambavyo vimeunda muungano unaowaunganisha marais wa zamani Macky Sall na Abdoulaye Wade. Sall aliondoka madarakani mwezi Aprili baada ya miaka 12 madarakani, akikabidhi mikoba kwa Faye na kuondoka Senegal kuelekea Morocco.

Soma pia: Rais mpya wa Senegal kuanza na mageuzi ya kiuchumi

Mpinzani wa muda mrefu wa kisiasa wa Sall , Waziri Mkuu wa sasa Ousmane Sonko, amependekeza mara kwa mara kwamba wanachama wa utawala wa zamani, ikiwa ni pamoja na Sall, wanaweza kufikishwa mbele ya mahakama.

Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii, Sonko alikashifu mashambulizi dhidi ya wafuasi wa Pastef katika mji mkuu wa Dakar na miji mingine tangu kampeni zilipoanza.

Athari za ghasia

Senegal | Wafuasi wa wanasiasa Sonko na Faye.
Shangwe miongoni mwa wafuasi wa wanasiasa wa chama tawala cha Pastef.Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Kundi moja la kiraia la nchini Senegal limeripoti kuongezeka kwa ghasia katika wiki ya kwanza ya kampeni, ikiwa ni pamoja na makao makuu ya chama cha upinzani kilichochomwa moto huko Dakar na mapigano kati ya wafuasi katikati mwa Senegal.

Aidha kiongozi huyo, amewashutumu wafuasi wa Meya wa Dakar Barthelemy Dias anayeongoza muungano pinzani wa Samm Sa Kaddu kwa kuwashambulia wafuasi wa chama chake.

Muungano wa Samm Sa Kaddu umesema Sonko anawajibika kwa lolote litakalowatokea wanachama wake, wanaharakati, wafuasi na wapiga kura.

Senegal inatarajia kufanya uchaguzi wa bunge jipya siku ya Jumapili, baada ya rais Bassirou Diomaye Faye kuvunja bunge lililokuwa likidhibitiwa na upinzani.

 

Related Posts