Tafsiri ya uchaguzi iliyopo CCM, si ya Chadema wala ACT

Kitu chenye mvuto kuhusu kitabu “Uncivilized Civilization” ni kuwa mwandishi Morris Schwartzberg, alifafanua vema dhana ya “Ustaarabu” – “Civilization”. Aliandika kwamba unachoona wewe ni ustaarabu, mwenzio anatafsiri ni kutostaarabika, vivyo hivyo kinyume chake.

“Uncivilized Civilization” – “Ustaarabu wa Kutostaarabika”, ni kitabu kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1920. Zaidi ya karne moja baadaye, maarifa ndani yake bado yanakidhi kuzifundisha jamii za kiulimwengu.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 una sura inayofanana na hali ilivyokuwa mwaka 2019. Ni dalili mbaya zaidi, kwani kilichofanyika 2019 kilipalilia njia Uchaguzi Mkuu 2020 ambao ni wa hovyo zaidi katika historia ya Tanzania. Kama imetokea hivi 2024, itakuwaje Uchaguzi Mkuu 2025?

Ni malalamiko kila pembe ya nchi. Vyama vya upinzani, hasa Chadema na ACT-Wazalendo, wanalalamika na kutoa matamko mfululizo. Hoja kubwa ni wagombea wao kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuenguliwa kwa sababu ambazo wanasema si za haki.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohammed Mchengerwa, aliagiza wenye malalamiko wakate rufaa. Wakata rufaa wakasema walikuta ofisi zimefungwa. Bila shaka hili halikuwa la nchi nzima. Yapo maeneo rufaa zilipokelewa.

Binafsi nimeona baadhi ya barua za majibu ya rufaa. Ukisoma vizuri, unajionea jinsi usikilizaji wa rufaa ulivyo tatizo lingine. Rufani zimeongeza malalamiko badala ya kupunguza. Ukipitia kila kitu unaona dhahiri kuna kitu kikubwa hakipo sawa.

Je, ni uchaguzi? Kama ndivyo kwa nini kuna mvutano? Mazingira ya uchaguzi ya sasa ni sawa na mpira wa miguu kwenye uwanja wenye mwinuko. CCM wamejichagulia goli lao ni mlimani, wapinzani wapo bondeni. Sheria ya mchezo inasema hakuna kubadili goli. Kisha, refa, waamuzi wasaidizi hadi kamishna wa mchezo ni watu wenye vinasaba vya ukada.

Mchengerwa, mbunge wa CCM, ni waziri katika Baraza la Mawaziri, ambalo bosi wake, Rais Samia Suluhu Hassan ni Mwenyekiti wa CCM. Mfumo wa wagombea kuteuliwa na hadi kutangazwa baada ya kushinda, upo kwenye utii wa Waziri Mchengerwa, kwa maana hiyo wanamheshimu Rais Samia.

Hata kama Mchengerwa anataka haki itendeke, Rais Samia anahitaji chama chake (CCM), kishindane kwa uwazi na ukweli ili ajue nguvu yake, kuna wasimamizi wa uchaguzi, kwa kudhani kuminya wapinzani ni kuwafurahisha wakuu wao, si ajabu kukutana na manung’uniko yanayoendelea.

Uchaguzi ni nini? Swali hili linaweza kusaidia kutibu malalamiko mengi kuhusu uchaguzi kama litajibiwa kwa usahihi. Na pengine, tafsiri ndiyo inayogomba. CCM wanaamini katika mantiki tofauti kuhusu uchaguzi. Wapinzani nao wanayo tafsiri yao. Sawa na hekima za Schwartzberg katika Uncivilized Civilization.

Migogoro ya kila wakati kwenye uchaguzi inatoa ishara kwamba CCM na vyama vya upinzani, havikutani kwenye tafsiri moja. Pengine, CCM wanaamini uchaguzi ni mzani wa kupima nguvu yao na kukubali kwao ili wajue jinsi ya kuendelea kuongoza. Wapinzani wenyewe wanaamini uchaguzi ni kuishinda CCM.

Uchaguzi ni mchakato wa kuchagua viongozi kwa mujibu wa Katiba au sheria zilizotungwa na kukubaliwa. Kisiasa, uchaguzi ni tendo la kukasimisha mamlaka. Yaani, wananchi ambao ndio wenye mamlaka, wanakasimisha kwa wachache kwa kipindi fulani. Tanzania ukasimishaji huwa wa miaka mitano.

Kwa mantiki hiyo, uchaguzi ni mali ya wananchi. Wao ndio wanapaswa kuachwa waweze kukasimisha mamlaka yao kwa wanaowaona wanafaa. Uchaguzi siyo mali ya CCM, kwamba waamue kanuni za kimchezo zenye kuwapendelea. Wala uchaguzi siyo tafsiri ya upinzani kwamba lazima CCM wang’oke.

Huwezi kucheza mechi ya soka, kikapu, pete au mchezo mwingine wowote, mwamuzi na wasaidizi wake wote unawaweka wewe, matokeo yake, badala ya kuchezesha kwa haki. Ndivyo ilivyo kwenye uchaguzi Tanzania.

Wizara ya Tamisemi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni kishawishi cha kuharibu uchaguzi. Kuna wasimamizi watadhani kuacha kila kitu kiende kwa haki na usawa, halafu CCM ishindwe vibaya, itamkwaza Rais Samia, bosi wao, kwamba chama chake hakikubaliki chini ya uongozi wake.

Ndiyo matokeo ya kuwa na wagombea wengi wenye kupita bila kupingwa. Mapambano ya kugombea kura na wapinzani hayatakiwi, yanaweza kuivua nguo CCM. Ikitokea hivyo, wataweza kumtazama vipi usoni Rais Samia, ambaye anaambiwa kila siku wapinzani hawana watu?

Haijasahaulika hii; mwishoni mwa Agosti na mwanzoni mwa Septemba 2024, kuna video ilisambaa mitandaoni, ikimwonesha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marko Ng’umbi, akitamba jinsi Serikali ilivyohusika kufanya uhalifu wa uchaguzi. Marko alijiweka katikati ya muktadha, maana alisema yeye alishiriki.

Marko alisema, madiwani waliopita bila kupingwa ulikuwa mpango wa Serikali. Hata kwenye majimbo, Serikali ilihusika, naye alishiriki. Hadi maporini, yaliyotendeka, ulikuwa mpango wa Serikali, naye alishiriki. Hii ni bila kumwongezea maneno.

Rais Samia, alimfuta kazi Marko mara moja. Ni jambo jema. Hata hivyo, ukweli dhahiri ni kwamba kifuani kwake inaonekana kuna mengi, ndiyo maana anashindwa kujizuia, kwa hiyo anajikuta anadondosha vingine hadharani.

Ukitafsiri maneno ya Marko kwa utaratibu wa kupita katikati ya mstari (between the line), utayaona majigambo ndani yake, jinsi ambavyo mambo yasiyofaa hufanywa kwa masilahi ya wachache kwenye mfumo wa dola. Kwake hiyo ni fahari. Ni fahari ya uhalifu.

Watu kama Marko na wasimamizi wengi wa uchaguzi, hudhani kuwa kuengua wagombea wa upinzani kwa hila ni matumizi mazuri ya kanuni za kimchezo. Hawajui kuwa uchaguzi ni mali ya wananchi. Kuuharibu ni kutenda uhalifu wa kidola kama alivyosema mwanazuoni wa Ujerumani, Friedrich Nietzsche.

Related Posts