Dar/mikoani. Malalamiko ya wapinzani kuhusu uadilifu wa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa baada ya maelfu ya wagombea wao kuenguliwa yamekiibua Chama tawala, CCM kikiiomba Wizara ya Tamisemi inayousimamia, “kupuuza makosa madogo kwa wagombea na kuwarejesha kuleta ushindani ma kukuza demokrasia”.
CCM imesema demokrasia ya Tanzania bado ni changa inayohitaji muda wa wananchi kujifunza na hivyo wagombea walioenguliwa kwa kasoro ndogondogo kupewe fursa ya kugombea na kuendelea kujifunza.
CCM imetoa maombi hayo iliyosema yana baraka za Mwenyekiti wa Chama, Rais Samia Suluhu Hassan, kipindi ambacho maelfu ya wagombea wa upinzani nchini wakiwa wameenguliwa kutokana na sababu mbalimbali, baadhi yake CCM ikidai ni ndogo zinazozungumzika huku wapinzani wakidai hazina msingi na zimelenga kukipendelea chama tawala.
Miongoni mwa sababu ambazo wapinzani wamezibainisha na kuzikatia rufaa ni baadhi ya fomu kuchezewa kwa kuongezwa herufi au tarakimu, madai ya kukosa kipato halali, kushindwa kujaza fomu, kukosea majina au tarehe na mwaka wa kuzaliwa.
Pia zimetajwa sababu kama kutokuwa wakazi wa eneo wanalogombea, kukosekana mihuri na wagombea kutoandika majina matatu au ya wadhamini wao.
Mathalan, ACT-Wazalendo imedai wagombea wake 51,423 wameenguliwa kwa kigezo cha kukosa udhamini wa chama ngazi ya kata. CUF nayo imedai ilisimamisha wagombea 56,816 nchi nzima lakini walioenguliwa ni zaidi ya 48,000.
Chadema imedai karibia nusu ya wagombea wake nchi nzima wameenguliwa, ingawa haikuwa na takwimu za kitaifa.
Baadhi ya walioenguliwa wamekata rufaa na kuangukia pua, huku wengine wakipata vikwanzo mbalimbali vikiwemo vya ofisi za wasimamizi kufungwa na wengine kutakiwa wawasilishe rufaa wenyewe badala ya vyama vyao.
Katikati ya vilio hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amejitokeza mbele ya waandishi wa habari kuwasilisha maombi ya chama hicho aliyosema yana Baraka za Mwenyekiti, Rais Samia Suluhu Hassan kwa Ofisi Rais, Tamisemi.
Dk Nchimbi akizungumza kwenye mkutano na wanahabari Dar es Salaam, Novemba 12, amesema baadhi ya mambo yaliyowekewa mapingamizi ni madogo madogo yanayohitaji kupuuzwa.
Amesema kwa kuyaona hayo, wanamuomba “Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa atumie mamlaka yake kuangalia suala hilo ili wananchi wawe na mawanda mapana ya uchaguzi.”
Dk Nchimbi ametaja baadhi ya makosa yaliyojitokeza ni pamoja na wagombea kukosea tarehe yake ya kuzaliwa, kukosea herufi ya jina, mgombea kuruka vipengele, ambayo kwa mujibu wa utaratibu makosa hayo yanamuondolea mtu sifa za kuteuliwa.
“Katika maelekezo ya mwenyekiti wa CCM (Rais Samia Suluhu Hassan), tumeelewana kimsingi katika demokrasia hii changa ya nchi yetu, lazima upate nafasi ya kujifunza.
“Nitoe wito kwa Waziri wa Tamisemi, tunajua watendaji wamefuata sheria lakini ni muhimu kukumbuka demokrasia yetu bado ni changa, wanahitaji kukua. Tutachukua muda kujifunza, lakini watu wetu hawajazoea vitu hivi na tutachukua muda kujifunza kidogo katika uchaguzi huu.
“Tunaziomba mamalaka zinazohusika, hasa Tamisemi, katika hatua za mwisho za rufaa kuyapuuza makosa madogo madogo ili watu wengi wapate nafasi ya kugombea. Serikali itazame makosa madogo yasipewe uzito kwenye rufaa, japo ya kisheria. Kwa sababu sheria imewekwa kwa ajili ya kuwasaidia watu, sio kuleta tafrani kwenye jamii,” amesema Dk Nchimbi.
“Lakini yapo maeneo mgombea amerudi sehemu na kwa maana ya utaratibu wa kisheria, makosa haya hayampi nafasi ya kuteuliwa, lakini kwa maelekezo ya mwenyekiti, ni msingi watu wapewe nafasi ya kusikilizwa.”
Amesema wao kama CCM, wangependa kuona ushindani unakuwepo kutokana na wagombea wengi, hivyo, amesisitiza kuwepo uvumilivu kwa mustakabali wa Taifa.
Hata hivyo, Dk Nchimbi amesema kuna yale makosa makubwa, akitolea mfano sehemu inayotakiwa kugombea mwanamke, basi anapogombea mwanaume hilo ni kosa halivumiliki.
Akisisitiza hoja hiyo, Dk Nchimbi amesema: “Msimamo huu wa chama una baraka zote za mwenyekiti wa chama.”
Akijibu swali kwa nini Rais Samia amemwagiza yeye kueleza hayo badala kumwambia moja kwa moja Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, Dk Nchimbi amesema:
“Labda niseme, mimi ni katibu mkuu wa chama, nimezungumza na mwenyekiti wa CCM kama chama cha siasa, kwa kutazamana masilahi ya nchi yetu na nafasi ya chama,” amesema Dk Nchimbi.
Awali, Kabla ya mkutano wa Dk Nchimbi, Waziri wa Tamisemi amekutana na wahariri kwenye semina juu ya kanuni za uchaguzi huo na kuvitaka vyama vya siasa kuacha kulalamika mitandaoni, bali viwahimize wagombea wao kukata rufaa kwa kuzingatia kanuni.
Wagombea wasikae nyumbani na kuviacha vyama vyao vikilalamika kupitia mitandao ya kijamii, rufaa inakatwa na mgombea mwenyewe, kwa hiyo wale wanaoona hawajatendewa haki wajitokeze sasa watumie muda huu uliobaki wakakate rufaa,” amesema Waziri Mchengerwa.
Amesema mgombea ambaye hajaridhika na mchakato, njia ya kwanza ya kutafuta haki ni kukata rufaa kupitia kwa wasimamizi wasaidizi.
Amesema wagombea walioenguliwa bado wana siku moja ya Jumatano na haki ya pili ya kukata rufaa inapatikana kwenye kamati ya wilaya kupinga uamuzi wa msimamizi.
“Tujiepushe na mitandao ofisi ziko wazi hadi hivi sasa nazungumza ni saa 8:19 mchana, nawaambia wale wote walioenguliwa kama hawajaridhika wapeleke rufaa zao muda bado, kwa kuwa mchakato bado kanuni zinanibana kuzungumza zaidi,” amesema.
Amesema uchaguzi wa serikali za mitaa ni kalenda ya mwaka mzima na kila siku kuna tukio lake na kanuni zinazotumika, vyama vyote 19 vinavyotarajia kushiriki uchaguzi huo, vilikaa na vikakubaliana kwa pamoja kuzipitisha.
“Waambieni wanasiasa wafuate utaratibu, hatuwezi kuwa na taifa ambalo halifuati misingi ya Katiba, sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea wenyewe, tutakuwa taifa la ovyo kabisa,” amesema Mchengerwa.
Amesema hoja nyingi zinazoelezwa na vyama vya siasa, hususan vya upinzani, ni propaganda na kuwa huenda vyama hivyo havikujipanga na uchaguzi huo.
Waziri huyo amesema Novemba 14 mwaka huu, atatoa tathimini na takwimu za kila mkoa kwa ushahidi zaidi.
Akijibu kuhusu ofisi za wasimamizi na wasimamizi wasaidizi kufungwa, Mchengerwa amesema taarifa zilizorekodiwa kwa baadhi ya vyama vya upinzani, kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), zinadhibitisha kuwa hakuna ofisi iliyokuwa imefungwa ndani ya muda wa kazi uliowekwa kisheria.
“Isipokuwa kuna changamoto ilijitokeza katika Mkoa wa Arusha, kuna watu wasiokuwa na nia njema walivamia maeneo hayo na kutoa vitisho kwa watendaji, lakini maeneo mengi vituo vilikuwa wazi,” amesema waziri huyo.
Amesema kinachomshangaza ni kuona vyama vya siasa vinalalamikia wagombea wao kuenguliwa wakati wagombea wenyewe wamebaki nyumbani hawapeleki rufaa.
“Wanadhani malalamiko wanayotoa kupitia viongozi yanaweza kusaidia kutibu wanacholalamikia, ukweli ni kwamba kanuni zetu ziko wazi, ni nani anapaswa kwenda kukata rufaa, nawakumbusha kukata rufaa,” amesisitiza hilo.
Kwa upande wake, mwanasheria wa Tamisemi, Mihayo Kadete akizungumzia malalamiko ya wagombea kuenguliwa kwa kujaza kuwa kazi yake ni mjasiriamali, amesema hilo si sahihi kwa kuwa hiyo kazi halali inayotambulika kiserikali.
“Si sahihi kwa mgombea wa chama chochote kuenguliwa kwa kigezo kama amejaza tu kazi yake ni ujasiriamali, hii ni kazi halali na yule aliyeenguliwa kwa kigezo hicho anapaswa kukata rufaa kutafuta haki yake,” amesema mwanasheria huyo.
Lissu: Uchaguzi umevurugwa, umekwisha
Akiwa mkoani Singida, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu alikutana na waandishi wa habari akisema kutokana na idadi kubwa ya wagombea wao kuenguliwa, uchaguzi huo ni kama umekwisha hivyo wanachama wa chama hicho wanapaswa kujipanga upya.
“Ukiniuliza mimi nikwambie ukweli wa Mungu, nisizungumze siasa siasa, kama kuna namna ya kuuokoa, nitasema hauna namna. Labda tuanze upya mchakato wa uchaguzi upya,” amesema Lissu.
“Kwa hiyo uchaguzi wa mwaka huu umekwisha, hao waliosalia watakwenda, lakini uchaguzi huu umekwisha, umevurugwa, umechafuliwa. Huo ndio ukweli wa Mungu, tuache maneno maneno.
“Ukimya wetu una mwangwi mkuu, tumenyamaza sana kwenye mambo ya msingi na kwenye mambo ya hovyo haya, kwa nini,” amehoji.
Lissu amesema pamoja na ahadi za Serikali kwamba uchaguzi ungekuwa huru na wa haki, bado mambo waliyoyalalamikia katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020 yamerudiwa.
“Kile kilichotokea mwaka 2019 kwa wagombea wa upinzani kuenguliwa kila mahali nchi nzima, ndicho kinachoendelea sasa hivi,” amesema.
Amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa chama chao wameenguliwa zaidi ya asilimia 95 ya wagombea.
Amegusia pia jimbo analotoka la Singida Mashariki kuwa: “Tulilkuwa tumeweka wagombea 1,225, kati ya wagombea 1,250 wanaotakiwa kwa jimbo zima, wameenguliwa zaidi ya 500 na bado wanaendelea kuenguliwa,” amesema.
Akifafanua kuhusu mapingamizi waliyowekewa, Lissu amesema kuwa barua walizoletewa zinafanana kwa wagombea wote.
“Kwa mfano fomu inasema mgombea ni mkulima, barua inasema hajaonyesha kazi yake, fomu inasema amedhaminiwa, lakini barua inasema hajadhaminiwa na chama chake,” amesema.
Akieleza sifa za wagombea kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Lissu amesema sababu zilizotajwa hazipo kwenye kanuni.
“Hizo ndizo sababu zinazompotezea mtu sifa ya kuwa mgombea, sio mhuri, sio umekosea kuandika jina, sio umeandika kwa kifupi sio hivi visababu vyote vilivyotumika kuengua maelfu wagombea wa upinzani,” amesema.
Akieleza ukataji wa rufaa, Lissu amesema pamoja na kuwepo kwa haki hiyo, ni ngumu kukata rufaa.
”Sasa fikiria watu walienguliwa ni zaidi ya 100,000, hao wanaweza kuata rufaa? Wakate rufaa ndani ya siku nne na zisikilizwe na kuamuliwa ndani ya siku nne? Hilo jambo linawezekana?
“Mimi tangu juzi sijalala natengeneza rufaa za kajimbo kamoja tu na sijamaliza, hao Watanzania na vielimu vyao, unategemea wakate rufaa zaidi ya 100,000 zikasikilizwe na makatibu tawala, ndani ya siku nne inawezekana? Haiwezekani.”
Kutokana na hali hiyo, Lissu amewataka wanachama wa chama hicho kujipanga upya.
“Tunapozungumza kujipanga, ni kurudi kwenye hoja za msingi, Katiba mpya, mfumo huru wa uchaguzi, tusichekeane na watu walioonyesha kuwa hawako tayari kuachia hata kitongoji kimoja.
“Tuache kuota ndoto za mchana, kwamba kuna umoja wa kitaifa. Njia itakuwa ngumu sana, lakini ndio njia pekee. Hii longolongo haitupeleki popote,” amesema akisisitiza huo ni mtazamo wake lakini atakishawishi chama kukubaliana nao.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Lissu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema huo ni mtazamo wake.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema karibu asilimia 60 ya wagombea wao 150,000 wameenguliwa.
“Tulipokata rufaa kupinga wagombea wetu kuenguliwa, ni wagombea wachache sana wamerejeshwa, hasa Kigoma, Tunduru na maeneo machache, mengi msimamo wa wasimsmizi umebaki vilevile.
“Novemba 11, kuna mapingamizi mengi yaliwekwa na CCM sehemu mbalimbali za nchi na yameleta madhara kwa sababu wasimamizi waliyakubali karibu yote hasa kwa Dar es Salaam,” amesema.
Amesema pia walijaribu kufuata ushauri wa Waziri wa Tamisemi kwamba tufuate sheria, lakini sheria haionekani kuleta suluhisho.
“Waziri Mchengerwa aliiandikia ACT Wazalendo na makatibu wa vyama vyote ikiwemo CCM, akieleza kwamba vyama vina uhuru wa kuchagua ngazi ya chini ya kumdhamini wagombea.
“Sisi ACT Wazalendo tuliiandikia Tamisemi tukiambatanisha barua hiyo kwamba ngazi tuliyochagua ni ya kata, lakini yapo maeneo wamekiuka maagizo hayo wakisema hawayatambui na wamewaengua wagombea wetu,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo watakuwa na kikao Novemba 12, 2024 usiku kujadili mkwamo huo.
“Sisi wapinzani tusiishie tu kukutana, ni vizuri kuanzisha grand coalition (muungano mkubwa) kwa ajili ya matamko na shinikizo na yasitoke kwenye chama kimoja tu,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ADA Tadea, Juma Ali Khatib amesema wamesimamisha wagombea zaidi ya 560 na wamewekewa mapingamizi na wanaendelea kupambana nayo.
“Kufanya hivyo ni kwenda kinyume na agizo la mheshimiwa Rais, kwa sababu tunakwenda na 4R zake, alisema kila mwenye sifa ya kugombea agombee na uchaguzi uwe huru na wa haki, sasa tusimchafulie sifa zake,” amesema.
Katibu mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema wamesimamisha wagombea zaidi ya 600 nchi nzima na waliowekewa mapingamizi ni zaidi ya 30.
“Kwa sababu tuko kwenye rufaa tunasubiri zikamilike ndio tutoe tamko,” amesema.
Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amesema, “hakuna dalili njema katika uchaguzi huu, kwa sababu watu wanaosimamia uchaguzi ndio walewale tunaogombea nao.
“Tumeingia kwenye uchaguzi ndio tunayaona, watu wanakatwa, wanaondolewa sababu zinazotolewa hazina msingi, ilimradi fujo tu. Tutakata rufaa lakini hatujui kama watatukubalia au vipi,” amesema.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano cha CUF, Mohamed Ngulangwa amesema kutokana na enguaengua hiyo uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mbaya kuliko wa 2019.
“Maana uchaguzi ule japo wagombea walienguliwa lakini waliondolewa bila usumbufu, lakini mwaka huu kuna kuchezeana shere, maana watu wanaondolewa katika kuchukua fomu na wengine katika uteuzi na hata wakiteuliwa wanaenguliwa, kwa hiyo hatuelewi uchaguzi utakuwa katika hali gani.
“Tuliweka wagombea 56,816 nchi nzima, walioenguliwa ni zaidi ya 48,000 maana yake waliobaki ni zaidi ya 8,000 tu,” amesema.