Longido. Changamoto ya upatikanaji wa maji katika Kijiji cha Oltepes kilichopo Kata ya Orbomba, wilayani Longido huwalazimu wasichana na wanawake wa eneo hilo kutumia siagi ya ng’ombe ili kudhibiti damu ya hedhi na mkojo wa ng’ombe kujisafisha.
Wanawake hao hulazimika kutumia siagi hiyo (mafuta ya ng’ombe) kujipaka maeneo ya sirini, sambamba na vipande vya nguo za zamani ili kuifanya damu hiyo isishike katika nguo zao.
Eneo hilo lenye wakazi wapatao 4,000, hutembea umbali wa kilomita tano kutafuta maji, lakini nyakati za kiangazi wanapolazimika kutumia mkojo wa ng’ombe hutembea mpaka kilomita 10 kutafuta tu maji ya kunywa na kupikia kwenye mabwawa.
Hiyo ni sehemu ya adha wanayoipata wakazi wa maeneo kadhaa wilayani humo, licha ya sera ya maji kuelekeza majisafi na salama yapatikane umbali usiozidi mita 400 kutoka makazi ya watu yalipo.
Elizabeth Olodo (40) ni miongoni mwa wanawake wanaopitia changamoto hiyo kijijini hapo. Katika maisha yake yote, amekuwa akitegemea nguo za zamani na siagi ya ng’ombe ili kudhibiti hedhi yake.
Ingawa ni njia isiyo salama na kawaida, hii imekuwa ni chaguo lake pekee katika eneo ambalo taulo za hedhi ni anasa.
Elizabeth hujipaka siagi hii sehemu za siri ili kuepuka madoa kwenye nguo zake. Wakati wa kiangazi, ambapo maji ni haba, anakutana na changamoto kubwa zaidi kukusanya mkojo wa ng’ombe na kuuweka kwenye ndoo.
Baada ya mzunguko wake wa hedhi kumalizika, hutumia mkojo huo kujisafisha, kusafisha nguo zake na kuzianika kabla ya kuzivaa tena mzunguko unaofuata.
“Maisha hapa ni magumu. Hatuna uwezo wa kununua taulo za hedhi, kwa hiyo tunategemea nguo na mkojo wa ng’ombe,” anasema Elizabeth.
“Mzunguko wa hedhi ukiisha, natumia mkojo wa ng’ombe kujisafisha na kusafisha nguo zangu. Kisha naviweka vikauke na kusubiri kabla ya kuvivaa tena.”
Lakini matatizo ya Elizabeth hayaishii hapo. Anaendelea na majukumu yake ya kila siku ya kukusanya kuni, kutunza mifugo na kupika chakula, huku akishughulika na usumbufu wa nguo inayoshikilia mwili wake.
Majukumu yake ya kila siku hayamwachii nafasi ya kukaa nyumbani, kwani uhai wa familia yake unategemea mabega yake. Kila hatua anapochukua, anapata nguvu kutoka kwa vizazi vya wanawake waliovumilia changamoto kama hizo.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Longido, Dk Mathew Majani, anasisitiza hatari za kiafya zinazotokana na matumizi ya vifaa visivyo salama.
“Wanapoitumia nguo badala ya taulo za hedhi, hatuwezi kuhakikisha usalama wao. Vifaa hivi vinaweza kusababisha maambukizi na matatizo mengine ya kiafya,” anaeleza.
Dk Majani pia anataja kuwa, licha ya changamoto hizo, eneo hilo linapata manufaa kutokana na michango ya taulo za hedhi. Hata hivyo, usambazaji wake unahitaji kufuatiliwa kwa karibu ili kuhakikisha unakidhi viwango vya afya.
Hali inayokumbwa na wengi
Christina Denis (24), mkazi wa Longido na mama wa watoto watatu, naye ana hadithi inayofanana. “Maisha ni magumu, hatuwezi kumudu kununua taulo za hedhi,” anasema na kuongeza; “Hedhi ikija, hutumia nguo yoyote niliyopata, iwe safi au la.”
Christina anakumbuka alivyokosa shule wakati wa mzunguko wa hedhi kwa sababu aliona aibu kugundulika na damu iliyovuja, jambo ambalo lilimletea aibu na kupoteza heshima.
Anasema leo hii, ingawa baadhi ya wanawake kijijini hapo wana uwezo wa kununua taulo za hedhi, wengi bado wanategemea njia za kitamaduni.
Kama Elizabeth, Christina mara nyingi hutumia mkojo wa ng’ombe kusafisha nguo zake za hedhi pale ambapo hakuna maji.
“Ikiwa kuna maji mtoni, nitasafisha nguo yangu huko. Ikiwa hakuna, nitatumia mkojo wa ng’ombe kuioshea,” anasema.
Licha ya shida hii, Christina anasema anapata nguvu katika ustahimilivu wa wanawake katika jamii yake. “Kila wakati ninaposafisha nguo ile, najikumbusha jinsi nilivyo na nguvu. Mimi ni sehemu ya mstari mrefu wa wanawake waliovumilia na hali hii,” anasema.
Kisa cha Christina huwakumba wasichana wale waishio pembezoni, wapo ambao hujihifadhi katika mazizi ya ng’ombe hasa maeneo ya wafugaji mpaka siku zao zikome na wapo ambao hukatisha masomo kwa kuwa hata vitambaa vya nguo chakavu vimekosekana.
Utafiti wa shirika lisilo la kiserikali la usawa wa wanawake na wasichana (FOEPA) umeonyesha Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wasichana hasa wa jamii ya wafugaji wamekuwa wakiacha masomo na wengine kukosa vipindi kwa siku kadhaa wanapopata hedhi.
Utafiti uliofanywa na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef), ulionyesha wasichana hukosa masomo siku nne hadi tano kwa mwezi kutokana na hedhi ambapo msichana mmoja kati ya kumi huacha shule kila mwaka kutokana na kukosa vifaa vya kujihifadhi wakati wa hedhi.
Wasichana waishio maeneo yasiyofikika wanakosa namna ya kujihifadhi wawapo katika siku zao za hedhi, hivyo kukabiliwa na changamoto ya kukosa masomo kwa siku tano hadi saba za mwezi.
Baadhi ya maeneo yaliyotajwa kuwa na changamoto hiyo ni Nchinga Lindi vijijini, Ntuntu Singida, Izimbia Bukoba, Ngarenaro, Longido na Serioni mkoani Kilimanjaro, huku maji na sabuni vikitajwa kuwa changamoto licha ya kuwa msaada kwa wasichana hao.
Licha ya changamoto hii kuonekana vijijini, Mtafiti katika Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Angela Shija anasema utafiti umeonyesha kuwa asilimia 80 ya wanafunzi waliopo mijini wanatumia taulo za kike mchana wakiwa shuleni na usiku wanatumia vitambaa kutokana na sababu za kiuchumi.
Hadithi za Elizabeth na Christina si changamoto yao pekee. Kwa mujibu wa UN Women, mamilioni ya wanawake na wasichana duniani kote bado hawawezi kumudu bidhaa za hedhi au kupata huduma za usafi bora za kudhibiti afya zao za hedhi.
Tatizo hili, linalojulikana kama umasikini wa hedhi, husababisha kukosa shule na kazi na linaweza kusababisha changamoto kubwa za kiafya.
Umasikini wa hedhi unahusiana na ukosefu wa uwezo wa kupata au kumudu bidhaa za hedhi, maji safi, usafi na huduma za usafi. Pia, unatoa mwanga kwa ukosefu wa elimu kuhusu afya ya hedhi.
Kwa wanawake na wasichana wengi, hedhi sio tu mchakato wa kimaumbile bali ni kikwazo cha elimu, fursa za kiuchumi na afya.
Hili ni tatizo linaloenea sio tu Longido bali kote Tanzania, wasichana wengi wanajaribu kutumia mbadala zisizo salama, kama vile vipande vya nguo, kwa sababu wanakosa bidhaa za hedhi salama na zenye usafi.
Athari za changamoto hizi ni zaidi ya usumbufu wa kimwili. Kwa kuwa asilimia 60 ya wanawake wa Tanzania wanaishi katika umaskini, upatikanaji wa bidhaa za hedhi ni anasa ambayo wachache wanaweza kumudu.
Bila maji ya kutosha kwa ajili ya usafi binafsi, wasichana wengi wanakosa shule au kuacha kabisa. Athari hii kwa elimu yao ni kubwa, na inazidi kudumaza mizunguko ya ukosefu wa usawa kijinsia.
Ingawa wengi wa Watanzania wanakutana na changamoto za maji, usafi na afya, wanawake hasa wanakutana na ugumu unaojitokeza katika usafi wa hedhi.
Katika maeneo ya vijijini, hedhi mara nyingi ni suala linalozungumziwa kidogo na hii inachangia ukosefu wa elimu na rasilimali. Wasichana wengi hukua wakiwa hawana ufahamu kuhusu miili yao au jinsi ya kudhibiti mzunguko wao wa hedhi kwa usahihi.
Bidhaa za hedhi ni ghali kwa mamilioni ya wanawake duniani kote. Sera zisizo na mtazamo wa kijinsia na ushuru mkubwa juu ya bidhaa za usafi wa wanawake ni baadhi ya sababu zinazochangia hili na pia kuimarisha unyanyapaa unaozunguka hedhi.
Hitaji la bidhaa za hedhi zinazoweza kumudu na zinazopatikana ni dharura, hasa katika maeneo ya mbali kama Longido.
Changamoto ya maji Longido
Kuhusu mgogoro wa maji, Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido Dk Steven Kiruswa amethibitisha kuwa upatikanaji wa maji katika eneo hili umeongezeka hadi asilimia 56, kutoka asilimia 36 miaka saba iliyopita.
“Mikakati inaendelea ya kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2025, ikiwa ni pamoja na miradi ya kuchimba visima vya maji, vyanzo katika baadhi ya milima ikiwa ni pamoja na Longido na kuchimba visima vipya vitano,” anasema.
Kampeni ya bidhaa za hedhi
Mratibu wa Baraza la Wanawake wa Kimaasai (PWC), Jackson Maole, anasema wana kampeni ya kutoa taulo za hedhi bure kwa watoto wa shule na kuondoa ushuru kwa bidhaa za hedhi.
“Tunaisihi Serikali ije na mpango wa kutoa taulo za hedhi bure kwa watoto wa shule wote,” anasema Maole.
“Katika jamii za Wamasai, wanawake na wasichana wengi wanakalibiwa kutumia vifaa visivyo salama ambavyo vinaweza kuathiri afya zao. Lengo letu ni kuhakikisha afya ya hedhi haihitaji kuwa kikwazo kwa elimu au heshima.”
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation