VIDEO: Saa 4 za mapokezi ya mwili wa Mafuru Dar

Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru umewasili nchini na kuhifadhiwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo.

Mapokezi ya mwili huo yamefanyika kwa takribani saa nne tangu ndege ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Mafuru mtaalamu wa fedha na uchumi aliyehudumu katika sekta binafsi na sekta ya umma alifariki dunia Novemba 9, 2024 akiwa anapatiwa matibabu nchini India.

Mwili wa Mafuru umewasili saa 7.45 mchana ukisindikizwa na baadhi ya wanafamilia akiwamo mkewe, Noela Mafuru.


VIDEO: Mwili wa mafuru ulivyowasili Dar

Saa 10.15 jioni msafara wa magari zaidi ya 50 ulianza safari kuelekea Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo kwa ajili ya kuuhifadhi ukiongozwa na gari la Mkuu wa Trafiki Kanda ya Dar es Salaam.

Tukio la kupokea mwili liliongozwa na baba mzazi wa marehemu, Gamba Mafuru aliyeingia jengo la mizigo (Terminal Cargo) saa 9.11 alasiri kupokea mwili wa mwanaye.

Ilipofika saa 9.50 alasiri geti la jengo hilo lilifunguliwa kuwezesha gari maalumu la kubeba jeneza lenye mwili wa Mafuru kuingia.

Dakika nane baadaye lilitoka likiwa limebeba jeneza, kiti cha mbele akiwa amekaa mdogo wa marehemu Maira Mafuru, na ndugu mwingine aliyeketi kiti cha nyuma.

Gari hilo lilipotoka ndani ya jengo la mizigo lilisimama kwa dakika 15 kuwawezesha ndugu, jamaa na waombolezaji wengine kumuombea kabla ya kuanza safari ya Lugalo.

Msafara ulipita katika barabara za Nyerere, Mandela, Sam Nujoma na Bagamoyo iliko Hospitali ya Lugalo. Waombolezaji wachache na wanafamilia walikwenda kuuhifadhi mwili wa Mafuru saa 11.10 jioni.

Ratiba ya maombolezo, mazishi

Msemaji wa familia, Ephraim Mafuru amesema mazishi yatafanyika Ijumaa, Novemba 15 katika makaburi ya Kondo, Tegeta jijini Dar es Salaam.

Kesho Jumatano, Novemba 13 maombolezo yataendelea nyumbani kwa marehemu Bunju A na Alhamisi Novemba 14, mwili wa Mafuru utaagwa katika ukumbi wa Karimjee kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 8.00 mchana kisha utapelekwa nyumbani kwake utakapolala kabla ya shughuli za mazishi Ijumaa.

Ratiba ya mazishi itaanza saa 2.00 asubuhi kwa chai kwa waombolezaji nyumbani kwa marehemu na saa 4.30 hadi saa 5.30 asubuhi msafara utaelekea Kanisa la Waadventista Wasabato  Magomeni ambako itafanyika ibada ya faraja kuanzia saa 6.00 hadi saa 8.00 mchana. Msafara utaelekea makaburi ya Kwa Kondo, Tegeta kwa mazishi kuanzia saa 9.00 alasiri.

Amesema Mafuru aliyeacha mke na mabinti wawili alikaa India mwezi mmoja kwa matibabu hadi mauti ilipomfika Novemba 9, 2024.

Viongozi mbalimbali wampokea

Wakimzungumzia Mafuru, baadhi ya waombolezaji waliojitokeza kupokea mwili wake wamesema alikuwa mkarimu, aliyeipenda nchi yake.

Mwanzilishi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa BSM Washauri Tanzania, Bakari Machumu amesema alimfahamu Mafuru akiwa mwanahabari wa biashara katika gazeti la Business Times na alikuwa chanzo chake cha habari.

“Tulikuwa na ukaribu huo hadi nilipohamia Mwananchi, alikuja nikiwa Mkurugenzi Mtendaji (Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd) akataka tufanye ushirikiano na taarifa wanazozichakata ziwe zinatumika The Citizen, tukafanya naye kazi,” amesema Machumu.

“Taarifa za kifo chake nilizipata Jumamosi nikiwa natoka kanisani, kuna mtu akanipa pole, nilisikitika mno, lakini ndiyo hivyo ametangulia, tumuombee,” amesema.

Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema: “Nilitegemea tungeendelea kuwa naye, ni kijana wa kizazi chetu sisi tuliozaliwa miaka ya 1970, tulitegemea tutaendelea kuwa pamoja kwenye harakati za kuimarisha nchi,” amesema Zito.

“Mara ya mwisho nilikuwa naye kwenye mjadala wa dira yeye (Mafuru) akiwa moderator (muongozaji),” amesema akieleza alikuwa mkarimu.

“Hatuna namna ni kuendelea kumshukuru Mungu kwa maisha yake, Mafuru ametangulia akiwa ameacha legacy (kumbukumbu) ambayo ni wajibu wetu kuendeleza mema yake.”

Waombolezaji wengine waliokuwapo ni Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

Related Posts