Yafahamu masaibu wanayopitia walimu shule binafsi

Unatambua kuwa walimu shule binafsi wanafanya kazi katika mazingira magumu ikiwamo kukosa kinga na usalama wa ajira zao?

Mwananchi limezungumza na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Shule Binafsi Tanzania (TPTU), Julius Mabula, anayeelezea masaibu wanayopitia walimu wa shule hizo na masuala mengine mbalimbali kuhusu walimu na kada ya ya ualimu kwa jumla.

Swali; TPTU kilianzishwa lini na kwa madhumuni gani?

Jibu; Chama cha Walimu wa Shule Binafsi Tanzania (TPTU), kilianzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kusimamia, kulinda, kutetea haki na maslahi ya walimu wote wa shule za binafsi nchini kuanzia shule za awali, msingi na sekondari.

Swali: Chama chenu kinajitofautishaje na CWT ambacho kimechukua jina la walimu kitaifa?

Jibu: Walimu na waajiri wengi wamekuwa wakichanganya wakiuliza kwa nini kuwe na TPTU? na na sisi tunasema kwa nini kuwe na CWT?

Kwanza sheria inatoa uhuru wa kuanzisha vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi kuanzia wafanyakazi 20 wa kada moja. Vyama vinaanzishwa ili kuwapa fursa wafanyakazi kuchagua chama kitakachowatetea na kuwapigania haki zao.

Kuhusu tofauti, niseme ipo kubwa japo tumesajiliwa ofisi moja na tupo chini ya sheria moja. Sisi hatuhusiki na walimu wa umma bali tunahusika na walimu wa shule za binafsi.

Walimu wa umma hawatuhusu kwa sababu uzoefu unatuambia kwamba hatujui changamoto za walimu wa umma, kwa hiyo tumewaachia CWT ambao nao hawazijui changamoto zetu na hawawezi kutupigania.

Swali: Kuna maoni kuwa nyote ni walimu na pengine haki zenu zinafanana. Kulikuwa na haja gani ya kuwa na chama mbadala?

Jibu: Matatizo ya mwalimu wa shule binafsi na matatizo ya mwalimu wa umma, ni vitu viwili tofauti. Kwa mfano, kule umma wanapanda madaraja lakini binafsi hamna kupanda madaraja. Lakini pia wao wana mikataba ya moja kwa moja lakini huku binafsi wana mikataba naweza kuita ya ‘magumashi’ (ubabaishaji).

Sababu nyingine sisi tupo kwa waajiri wengi lakini kule umma wanamwajiri mmoja ambaye ni Serikali. Hi pia inawapa shida CWT hata namna ya kutuunganisha walimu kwa sababu huku binafsi hawaeleweki leo yupo hapa kesho utamkuta sehemu nyingine.

Kwa hiyo kwa vile sisi ni walimu wa muda mrefu na tunakutana na changamoto hizi, tukaona tuanzishe chama ambacho kitakuwa kinapigania haki na maslahi yetu.

Swali; Mwitiko wa walimu shule binaafsi kuwa wanachama ukoje?

Jibu; Kulingana na kazi ilivyo ngumu tuna wanachama 2,224 waliosajiliwa na matawi yasiyopungua 84. Tumebaini waajiri wengi hawana elimu ya vyama vya wafanyakazi na elimu ya sheria za wafanyakazi, kwa hiyo wao wana mtazamo hasi juu ya vyama hivi. Wanajua chama kikija kinakuja kurubuni wafanyakazi, kuendesha migomo na kuwafungua macho juu ya haki zao.

Tufahamu kwamba sekta binafsi wanatumia nguvu kubwa ili ile nguvu kazi iwazalishie faida kubwa, kwa hiyo ili mtu wa namna hiyo umbadilishe fikra zake inahitaji nguvu.

Tunaishukuru Serikali kwani pale waajiri wagumu na jeuri wanapokwamisha, tunampigia Kamishna wa Kazi anatusaidia.

Kwa hiyo kimsingi walimu na wafanyakazi wasio kuwa walimu huku sekta binafsi, wanahitaji chama lakini hofu yao ni kwamba je mwajiri wangu anasemaje, ndio maana na sisi tumewekeza nguvu kubwa huko.

Hili suala linafanikiwa japo kuwa sio la siku mbili au tatu kwamba tutalimaliza, ndio maana tumeanza kwanza na walimu wa shule za baadhi ya madehebu ya kidini. Baadaye tunaamini madhehebu mengine na hata shule za majeshi zitaiga.

Swali; Mnajitofautishaje kuepuka malalamiko kama ilivyo kwa CWT kiasi kwamba baadhi ya walimu huko walijitenga na kuanzisha chama kingine?

Jibu; Vyama vimesajiliwa kwa sababu kilichopo hakijakidhi matakwa ya wanachama na wanachama nao wanahitaji huduma.

Sisi kazi kubwa ni kutoa huduma inayostahili kwa wanachama wetu, tutahakikisha tunawapigania ili wafanye kazi katika mazingira mazuri yenye ustawi mzuri, kwa maana ya maslahi mazuri na mkataba mzuri na siku mwalimu akiachishwa kazi, taratibu na sheria zifuatwe.

Kwa mfano, kulikuwa na malalamiko mengi pindi wakiachishwa kazi, kuna ugumu mkubwa kupata mafao yao, kwa hiyo tumesaini mkataba na NSSF miongoni mwa makubaliano tuliyoingia, mwanachama wetu akiachishwa kazi leo au kesho apate stahiki zake bila usumbufu.

Swali: Changamoto gani wanapitia walimu wa shule binafsi nchini?

Jibu: Changamoto ya kwanza ni ajira. Huku kwetu, ajira za walimu binafsi hazina kinga kama ilivyo kwa walimu wa Serikali, kwa sababu ili umfukuze mwalimu ukutane na vyombo vitano, ambavyo ni Wizara ya Elimu, Utumishi wa Umma, Tamisemi, CWT na Utumishi wa Walimu.

Lakini huku sekta binafsi, mwajiri akikohoa kidogo tu umeshafukuzwa, kwa hiyo hiyo ndio inafanya watu kuona hiyo sio kazi.

Changamoto ya pili ni mikataba sio tu kwa walimu wa shule za binafsi, lakini hata kazi nyingine.Tunaomba sekta binafsi isimamiwe mbona kwenye sekta ya michezo tumeweza, mchezaji anapewa mkataba lakini sekta zingine kama ya walimu hawana mikataba huku Wizara ya Kazi ikiwapo na hiyo ndio kazi yake.

Changamoto ya tatu watu wetu hawakopesheki sasa dunia ya leo mataifa makubwa yanakopa, wabunge na wafanyakazi wengine wanakopa. Sasa kwa nini walimu wasikope? Kukopa ni sehemu ya maisha, lakini watu wetu hawaaminiki kwenye mazingira hayo.

Kwenye taaluma ya ualimu walimu wetu wanajisikia vibaya sana wanapotengwa. Kwa mfano kwenye semina, mafunzo, posho, usimamizi wa mitihani ya taifa wanatengwa. Sasa unamwamini vipi mtu afundishe miaka saba halafu humwamini kwenye kusimamia?

Binafsi huwa nahisi kwamba labda maofisa kazi wamezidiwa kwa sababu mazingira ya kazi ni magumu, hivyo kushindwa kufuatilia huku sekta binafsi.

Swali: Kwa kiwango gani unaridhika na namna Serikali inavyowatambua walimu wa shule binafsi?

Jibu: Ni kweli kwamba walimu binafsi hawatambuliwi kuwa ni walimu na ni kundi kubwa ndio maana mipango mikubwa ya Serikali inayozungumzia walimu wanakuwa wanamaanisha wa Serikali.

Ndio maana programu zote ambazo zinalenga walimu mfano vishikwambi, usimamizi wa mitihani, uandikishaji, wanaoguswa ni walimu wa Serikali.

Sisi tumeshakaa vikao vingi na Serikali juu haya mambo wanayajua tumewaomba na kuwaambia umefika muda wa kulitambua hili kundi kwa sababu kazi wanayofanya walimu wa taasisi binafsi ni sawa na kazi zinazofanywa na walimu wa Serikali.

Swali: Una maoni gani kuhusu sheria inayotaka kuwapo kwa bodi ya kitaalamu ya walimu?

Jibu: Bodi hii ipo na hivi sasa inatungiwa kanuni. Ni bodi inayokuja kwa ajili ya walimu wote. Ila sisi tumeiomba Serikali, tuliposoma zile kanuni za hiyo bodi, tuliona ilikuwa na adhabu kali sana.

Tukasema hizi adhabu zipunguzwe kwa sababu mwalimu akikosea kidogo ananyang’anywa leseni, sasa kwa mtu ambaye amesoma kwa miaka 17 inakuwa ngumu tukawaomba wapunguze masharti.

Taaluma ya ualimu na uwakili ni tofauti sana ndio maana mawakili wapo wachache sana nchini lakini walimu ukichukua wa binafsi na Serikali wapo zaidi ya 400,000 ambao wameajiriwa. Sasa ukiweka sheria kali na kunyang’anya leseni zao tunaenda kuchukua taaluma za watu wengi sana.

Hata hivyo, tumeomba mchakato wa bodi hii uharakishwe ili tuondoe walimu makanjanja mtaani na mwishowe taaluma iheshimiwe.

Swali: Hivi kuna usawa kati yenu na shule za umma?

Jibu: Ili mimi nizungumze vizuri katika sekta ya elimu, ni hadi pale nitakapoona walimu wa umma na binafsi wanahudumiwa na kupewa stahiki sawa.

Kwa sababu sekta binafsi zinatozwa gharama kubwa zaidi ya kodi 20 lakini shule za umma hawana kodi yoyote. Ibara ya 11 ya Katiba inasema Serikali ndio atawajibika kuwaelimisha wananchi wake, sasa mtu amekuja kukusaidia kuwekeza kwenye elimu, kwa nini unamuumiza na kodi nyingi ndio maana shule nyingi zinakufa. Lakini pia hizi kodi zinaathiri mishahara ya watu.

Lipo suala la vitendea kazi kama vitabu. Kwa upande wa walimu wa umma, wanapelekewa bure lakini kwetu tunanunua hata ile miongozo na vitabu ambavyo havipo kwa ajili ya kuuzwa.

Swali: Hivi sasa kuna mabadiliko ya mitalaa, je, mlishirikishwa kwenye mchakato na kupatiwa mafunzo?

Jibu: Nakiri kwamba mafunzo ya kuboresha ufahamu wa walimu waweze kuumudu huu mtalaa, bado hayajaeleweka. Hii ni kwa sababu waliokuja kuwawezesha waliwawezesha siku mbili ambazo kiuhalisia hazitoshi wakatuambia tukawafundishe walimu wengine.

Yaani mabadiliko ya mitalaa ya elimu yanakuja, unatupa mafunzo ya siku mbili na kuagiza kuwa tukawafundishe walimu wengine, hili eneo liwekewe nguvu kubwa ili walimu waweze kulimudu.

Swali: Kuna madai kuwa walimu wengi wa shule binafsi hawana sifa za kuwa walimu. Unalisemeaje hilo?

Jibu; Kuanzia mwaka 2015 kushuka chini kweli naunga mkono kwamba shule za binafsi zilikuwa na walimu ambao hawakuwa na sifa kwa sababu Serikali ilikuwa ikiajiri wahitimu wote wa ualimu.

Baada ya hapo, Serikali ilianza kuajiri kidogo kidogo, ndio maana mpaka sasa mtaani kuna watu wengi ambao hawana ajira.

Kwa hiyo kama hivi sasa kuna mwajiri mwenye mwalimu asiye na sifa, atakuwa amependa yeye kwa sababu kuna walimu wengi huko mtaani ambao wana sifa na hawana kazi.

Swali: Kwa vipi hadhi na heshima ya mwalimu nchini inaweza kurudi kama ilivyokuwa zamani?

Jibu: Miaka ya nyuma mwalimu aliheshimika na kuonekana ni mtu mstasrabu mitaani mpaka kufikia hatua ya kuwa mtatuzi wa migogoro mbalimbali katika jamii.

Ni kweli walimu wanaongezeka sana na kinachosababisha ualimu kushuka heshima na kudharaulika ni maslahi. Ndio maana mtu akikwambia nataka kuwa daktari au rubani amechungulia fursa.

Kuna walimu walistaafu 2018 mpaka sasa hawajalipwa stahiki zao sasa huyo mwalimu ataheshimika vipi? Mbunge akistaafu leo kesho anapewa stahiki zake, kuna mahali kama nchi hatujatoa kipaumbele kwa mwalimu.

Related Posts