ELIMU ZAIDI MIKOPO YA 10% INAHITAJIKA- MBUNGE ZUNGU
Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Azzan Zungu amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya na timu yake kwa kuandaa kongamano la kuelimisha wajasiriamali juu ya upataji wa mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri na namna ya kuitumia.
Zungu ameyasema hayo wakati akizungumza kama mgeni rasmi katika siku ya pili na ya mwisho ya Kongamano la Uelimishaji na Uhamasishaji Jamii Juu ya Uwepo wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu Sambamba na Matumizi ya Nishati Safi, lililofanyika Uwanja wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Amesema ni vyema kwa wanufaika wa elimu hiyo kuitekeleza katika matendo kwani changamoto kubwa kwa makundi mengi yanayoomba mikopo hiyo ni ukosefu wa elimu.
“Nimepita kwenye vikundi mbalimbali, asilimia kubwa ya vikundi bado hamjapata elimu ya kutosha ya kuingia kwenye hii mikopo, kwa maana havijaanza utaratibu wa kujaza maombi ya kupata hii mikopo, mtamuangusha mama Samia kama hiyo kazi hamuwezi kuifanya kuanzia leo”, amesema Zungu.
Amewaomba maafisa maendeleo kuwasaidia wakazi wa maeneo yao juu namna ya kupata mikopo hiyo ikiwamo kutimiza masharti ya kuipata ili wawe katika nafasi nzuri ya kuongeza tija na ufanisi katika biashara zao.
Aidha amewaomba wale wanaokusudia kupata mikopo hiyo kuwa na dhamira ya kutumia pesa zake vizuri kwa kukopa na kuzirudisha ili ziweze kuwasaidia wengine wenye uhitaji huku akiipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Wilaya ya Ilala kwa kusimamia vyema mapato, kiasi cha kuiwezesha Halmashauri hiyo kupata Shilingi bilioni 14.85 kwa ajili mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu
“Mheshimiwa Mkurugenzi Mabelya bado hela zipo kwenye wilaya ya Ilala, tafuteni takwimu kamili za wafanyabiashara kwenye masoko yetu, kuna pesa nyingi zinavuja kwenye masoko, kwenye maegesho, kuna pesa nyingi zipo kwenye vyanzo mbalimbali ambazo wananchi wapo tayari kuzitoa, lakini sisi wenyewe tunakuwa nyuma sana”, ameeleza Zungu.
Aidha amewataka maafisa maendeleo kutenda haki kwenye mikopo, akisema kuwa baadhi yao wamekuwa hawatendi haki kwa kuleta vigezo ambavyo havipo kihalali.
“Kuna malalamiko mengi sana ya wananchi kunyanyasika na kukata tamaa na hizi pesa, niwaombe maafisa maendeleo mtimize wajibu wenu kwa kutenda haki”, amesema Zungu.