Dar es Salaam. Wakati watu tisa kati ya 100 wakiathirika na kisukari nchini, wataalamu wa afya wametaja magonjwa yanayosababishwa na kisukari kisipodhibitiwa.
Hatua hiyo imekuja wakati watu wawili kati ya tisa wanaoishi na ugonjwa huo, hawagunduliki mapema mpaka kufikia hatua ya kupata madhara zaidi za kiafya.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 13, 2024 Mkurugenzi wa Hospitali ya Hindu Mandal, Profesa Kaushik Ramaiya amesema takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha asilimia 9.6 ya watu waliozidi umri wa miaka 25 wanaathiriwa na ugonjwa huo, na kwamba utafiti mpya wa Steps Survey unatarajiwa kuonyesha hali halisi kwa sasa.
“Nguvu kubwa imewekwa katika kutoa elimu kwa umma kwani zaidi ya asilimia 80 mpaka 90 ipo kwenye mtindo wa maisha, vituo vya afya kubaini mapema wenye changamoto na kuwafundisha wataalamu wa afya kufanya tiba mapema kwani kati ya tisa wawili hugundulika wameshapata madhara zaidi,” amesema Profesa Kaushik.
Ugonjwa kisukari unaweza kuwa chanzo cha magonjwa mengine endapo mgonjwa hatofuata maelekezo anayopewa na wataalamu wa afya.
Dk Asha Rajab kutoka Amref Health Africa ameelezea wagonjwa wa kisukari wapo hatarini kupata magonjwa mengine ikiwamo figo.
Dk Asha amesema mgonjwa wa kisukari ana uwezekano mkubwa wa kushambuliwa na magonjwa mengine kwa sababu kadhaa zinazohusiana na mabadiliko ya kinga ya mwili, mzunguko wa damu na kupona kwa vidonda.
Amesema kisukari hudhoofisha mfumo wa kinga ya mwili kwa sababu ya viwango vya juu vya sukari katika damu, sukari nyingi huzuia seli za kinga kufanya kazi vizuri, hivyo kuifanya iwe vigumu kwa mwili kupambana na maambukizi na vimelea vya magonjwa.
“Kwa wagonjwa wa kisukari mishipa ya damu inaweza kuharibiwa na viwango vya sukari vilivyo juu kwa muda mrefu, hii huzuia damu kufikia baadhi ya maeneo ya mwili na kupunguza utoaji wa virutubisho na seli za kinga kwenye tishu na sehemu zilizo na maambukizi,” amesema.
Dk Asha amesema wagonjwa wa sukari huchukua muda mrefu kupona kidonda kutokana na kuathirika kwa mishipa ya damu na kinga za mwili hivyo kutoa nafasi kwa maambukizi kushamiri, hivyo wanahitaji umakini zaidi wanapopata majeraha au vidonda.
“Ni muhimu kwao kufuatilia viwango vyao vya sukari, kudumisha lishe bora na kufanya mazoezi ili kuboresha afya yao ya jumla na kupunguza hatari ya maambukizi,” amesisitiza.
Dk Shabani Kiungulio kutoka Hospitali ya Rufaa mkoani Tanga amesema kisukari kinaweza kuathiri mfumo wa damu, figo, macho na neva na kusababisha athari kiafya kama upofu, shinikizo la damu na hata magonjwa ya moyo.
Dk Kiungulio amesema viwango vya juu vya sukari vinaweza kusababisha uharibifu wa mishipa ya damu mikubwa na midogo, hii husababisha shinikizo la damu kuwa juu, kujaa kwa mafuta kwenye mishipa na hatari ya mshtuko wa moyo au kiharusi kuongezeka.
“Magonjwa ya figo, viwango vya sukari vilivyo juu kwa muda mrefu vinaweza kuharibu vyumba vya nephrons, ambavyo ni sehemu za figo zinazosaidia kuchuja uchafu kwenye damu, hii inaweza kusababisha figo kushindwa kufanya kazi ipasavyo,” amesema.
Ametaja sukari nyingi kwenye damu huathiri mishipa ya damu kwenye retina na kwamba hiyo inaweza kusababisha kuvuja kwa damu au tishu kupasuka, bila kupata matibabu ya haraka inaweza kusababisha upofu.
Dk Kiungulio ametaja athari nyingine kuwa ni uharibifu wa mishipa ya fahamu kutokana na sukari nyingi kwenye damu husababisha maumivu, ganzi na kupoteza hisia, hasa kwenye miguu na mikono.
Pia, inaweza kuathiri viungo vingine, kama moyo na mfumo wa mmeng’enyo.
Amedokeza viwango vya juu vya sukari hutoa mazingira mazuri kwa bakteria kukua, pia kinga dhaifu ya mwili kwa wagonjwa wa kisukari hufanya maambukizi hayo kuwa rahisi kutokea.
“Watu wengi walio na kisukari wanaweza kuishi maisha marefu na yenye afya kwa kufuata kanuni za afya zinazopendekezwa na madaktari kama vile kudhibiti mlo, kwa watu wenye kisukari kudhibiti aina ya chakula wanachokula.
“Mlo wa afya unapaswa kuwa na viwango vya chini vya sukari na wanga pia, usambazaji mzuri wa protini na mafuta yenye afya, anapaswa kutumia mboga za majani, matunda yenye nyuzi nyingi, nafaka zisizokobolewa, pia wanashauriwa kuepuka vinywaji vyenye sukari na bidhaa za unga uliokobolewa,” amesema.
Dk Kiungulio amesisitiza watu kufanya mazoezi mara kwa mara, kwani yanaweza kusaidia kudhibiti sukari kwenye damu na kuboresha afya ya moyo na huruhusu mwili kutumia sukari kwa ufanisi na kusaidia kudhibiti uzito, ambao ni hatari kuu kwa watu wenye kisukari cha aina ya pili.
Amesisitiza upimaji wa kiwango cha sukari mara kwa mara, kupitia kifaa maalumu kinachotumika kupima kiwango cha sukari mwilini (glucometer), kujua viwango hivi humsaidia mtu kufanya uamuzi wa lishe, dawa na mazoezi ili kudhibiti kisukari vizuri.