Benki ya TCB kujenga uchumi kupitia mikopo ya Bilioni 300 kwa wafanyabiashara wadogo na wakati

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imetangaza azma yake ya kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi kwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 300 kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini. Mikopo hii inatarajiwa kusaidia wafanyabiashara hao kuongeza mitaji na kuinuka kiuchumi.

Akizungumza leo Novemba 13, 2024, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Biashara kwa Wateja Wadogo na Wakati wa TCB, Lilian Mtali, alisema benki hiyo, inayomilikiwa na serikali, ina nia thabiti ya kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini. “Tukiwa kama benki ya serikali, tumeona tuwe vinara katika kuleta suluhisho kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kukua kibiashara kwa kurahisisha malipo popote walipo,” alisema.

Mtali alifafanua kuwa TCB, iliyohudumu nchini kwa miaka 99, inalenga kutoa huduma za kisasa na suluhisho la malipo kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ili kuwasaidia kufanya biashara kwa urahisi zaidi. Hadi sasa, benki hiyo imetoa shilingi bilioni 300 kwa wajasiriamali wa kati na wadogo, pamoja na shilingi bilioni 250 kwa wafanyabiashara binafsi.

Huduma Mpya ya Malipo ya Kidijitali – ‘Lipa Popote’

Katika hatua nyingine, Mtali alitangaza kuzinduliwa kwa huduma ya ‘Lipa Popote,’ inayolenga kurahisisha miamala kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) pamoja na wamiliki wa biashara. Huduma hii mpya inawawezesha wateja wa TCB kupokea malipo moja kwa moja kwenye akaunti zao kupitia namba maalum ya Lipa Popote.

Alisema huduma hii inalenga kuwa suluhisho la malipo la haraka na salama kwa wafanyabiashara hao, ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa. “Lipa Popote inatarajiwa kubadilisha namna biashara ndogo zinavyofanya kazi kwa kurahisisha miamala ya kifedha na kuimarisha usalama wa malipo kwa wateja wetu,” alisema Mtali.

Kuchochea Ubunifu na Ujumuishi wa Kifedha

Ofisa Mkuu wa Huduma za Kidijitali na Ubunifu wa TCB, Jesse Jackson, alibainisha kuwa TCB imejikita katika kukuza ubunifu ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kufanikisha malipo bora, rahisi, na salama. “Kwa kuanzisha huduma ya kidijitali kama Lipa Popote, tunachangia kwa kiasi kikubwa malengo ya Tanzania katika kukuza ujumuishi wa kifedha, hasa kwa wajasiriamali wadogo, jamii, na watu binafsi ambao hawajafikiwa na huduma hizi,” alisema Jackson.

Huduma ya Lipa Popote ni sehemu ya mkakati wa TCB wa kuwaendeleza wajasiriamali nchini na kuwawezesha kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa kwa njia ya usasa wa kidijitali.

Related Posts