MANCHESTER, ENGLAND: NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes aligeuka shujaa baada ya kuokoa maisha ya mwanamume mmoja kwenye ndege akiwa anakwenda jijini Lisbon, Ureno kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha timu ya taifa hilo.
Kitendo hicho ambacho kilitokea baada ya mwanamume huyo aliyekuwa siti za nyuma ya ndege hiyo kuzidiwa na kuanguka chini, kimepokelewa kwa hisia tofauti na watu mbalimbali, huku mmoja wa viongozi wa juu wa miamba hiyo ya OIld Trafford akimsifia na kusema ni kawaida yake.
Fernandes ambaye alikuwa ameongozana na mchezaji mwenzake wa Man United na Ureno, Diogo Dalot, Jumatatu ya wiki hii, aligundua mwanamume huyo alianguka na kisha akamkimbilia huku akipiga kelele za kuomba msaada.
“Pole! Jamani, tunahitaji msaada! Pole! Tunahitaji msaada!”
Akisimulia tukio hilo, abiria mmoja aitwaye Susanna Lawson, alisema; “Bruno alikuwa aamemshikilia mwanamume huyo aliyeonekana kazimia, sijajua nini kilimkuta, lakini wafanyakazi walienda kumsaidia. Kulikuwa na kiti cha ziada na Bruno alikitumia kumsaidia mwanamume huyo kukaa.”
“Alibaki na wale wahudumu kuhakikisha mwanamume huyo anakuwa sawa na baada ya dakika tano hadi 10, alikuwa sawa na Bruno akarudi kwenye kiti chake, huku akionekana hataki ajulikane.”
Mmoja kati ya viongozi wa juu kutoka Man United alisema: “Hiyo ni tabia ya Bruno. Sio mtu anayekata tamaa au kugeuza uso katika hali kama hiyo. Ni kiongozi mzuri na anajali na kusaidia kwa njia yoyote anayoweza.
Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku moja tangu Bruno alipoiongoza Man United kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Leicester, kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Hadi sasa amefikisha mechi 250 kwa klabu hiyo tangu alipojiunga nayo akitokea Sporting Lisbon mwaka 2020 kwa ada ya Pauni 67 milioni.
Bruno amekuwa katika kiwango cha juu United wiki za hivi karibuni na amefunga mabao manne na kutoa pasi mbili katika mechi nne tangu Erik ten Hag aondolewe kazini.