Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema dhamira imara ya kisiasa katika ngazi zote za kitaifa na kikanda ni muhimu katika kuondoa matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
Kufanya hivyo, amesema kutaendeleza sera, mikakati, mipango na malengo ya kufikia matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Taarifa iliyotolewa Novemba 13, 2024 na Ofisi ya Makamu wa Rais, imesema Dk Mpango ameeleza hayo alipofungua mkutano kuhusu nishati safi ya kupikia, ulioandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) na Tume ya Nishati Afrika (AFREC).
Mkutano huo umefanyika kando ya ule wa 29 wa wakuu wa nchi na serikali wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29), unaofanyika mjini Baku, nchini Azerbaijan.
Dk Mpango amesema usambazaji wa nishati safi ya kupikia ni nguzo muhimu katika ustawi wa jamii, hivyo ni muhimu kuongeza jitihada kuwezesha upatikanaji wake kwa gharama nafuu, ili kuikomboa jamii hususani wanawake.
Amesema upatikanaji wa nishati hiyo utachochea usawa wa kijinsia kwa kuwa utawawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika elimu, kuepushwa na athari za kiafya zinazosababishwa na nishati chafu na kushiriki shughuli za kiuchumi na kiuongozi.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi wa Afrika na jumuiya ya kimataifa kuongeza ushirikiano ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia.
Amesema mchakato wa utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ni muhimu kuzingatia mazingira ya nchi husika, ikiwemo rasilimali zilizopo, changamoto, mahitaji ya jamii na teknolojia za asili.
Amesema mchakato huo unapaswa kufanyika kwa hatua kwa kukizingatia kuwa idadi kubwa ya Waafrika inategemea nishati ya kuni na mkaa.
Amesema viongozi wa Afrika wanapaswa kutoa kipaumbele cha pekee katika suala hilo kwa ushirikiano na wabia kutoka taasisi za kimataifa na sekta binafsi.
“Kutokana na Afrika kuwa na idadi kubwa ya vijana, ni muhimu kutumia ubunifu wao katika kuendeleza teknolojia sahihi ya nishati safi ya kupikia,” amesema.
Amesema ni muhimu kutoa msisitizo katika vyuo vya ufundi na ujuzi katika masuala ya teknolojia za nishati safi ya kupikia ili kuongeza rasilimali watu muhimu katika uvumbuzi wa teknolojia za kupika za kisasa na matengenezo ya vifaa vinavyotumika.
Amesisitiza matumizi ya teknolojia ya kidijitali ikiwemo utaratibu wa malipo ya kabla ili kuhakikisha uwazi na haki katika matumizi ya nishati safi.
Katika uunganishaji wa huduma hiyo, amesema ni vyema kuwe na chaguo la malipo kidogo-kidogo ili kuwezesha watu wengi wa kipato cha chini hususani vijijini kufikiwa na huduma hiyo.
Dk Mpango amesema kuzinduliwa kwa programu ya nishati safi ya kupikia ili kuwasaidia wanawake barani Afrika katika mkutano wa COP28, Dubai na Kuzinduliwa kwa Mkakati wa Tanzania wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia 2024 – 2034 ni jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuonyesha njia na kuhimiza viongozi wa Afrika kulipa kipaumbele suala hilo.