Fountain yaanza na mshambuliaji | Mwanaspoti

TAARIFA zinadai kwamba uongozi wa Fountain Gate, umemalizana na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Yusuph Athuman kwa kumpa mkataba wa mwaka mmoja.

Mshambuliaji huyo anatua Fountaine Gate akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na timu ya West Armenia inayoshiriki Ligi Kuu Armenia ambayo alijiunga nayo Julai 2023.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Fountain Gate kimeliambia Mwanaspoti kuwa tayari uongozi umemalizana na mchezaji huyo na ataanza kuitumikia baada ya usajili wa dirisha dogo litakalofunguliwa Desemba 15, mwaka huu.

“Ni kweli tumekamilisha usajili wa mchezaji huyo (Yusuph Athuman) ikiwa ni sehemu ya kuongeza nguvu kikosini na tunaamini ataongeza kitu ndani ya timu kutokana na uzoefu alionao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Uwepo wa kinara wa upajikaji mabao, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ hakuzuii sisi kufanya usajili. Tulimkosa mechi mbili akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa tumeona mapungufu ndio sababu ya kuongeza nguvu.”

Chanzo hicho kilisema wanaheshimu ubora wa washambuliaji walionao kikosini kwa sasa na wanatambua kazi kubwa wanayofanya lakini wameamua kuongeza nguvu ili kutoa changamoto ya ushindani huku pia wakiangalia namna wanavyokabiliana na mechi nyingi.

Athuman anaenda kuungana na Gomez ambaye hadi sasa amefunga mabao sita akiwa kinara wa ufungaji ndani ya Ligi Kuu Bara, lakini pia William Edgar naye ana mabao manne katika nafasi ya tatu ya ufungaji.

Mwanaspoti lilimtafuta Yusuph ambapo alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia dili hilo lakini lolote linaweza kutokea kwani ni mchezaji huru ambaye anaweza kuzungumza na timu yoyote.

“Siwezi kuzungumzia tetesi, mambo yakiwa tayari kila kitu kitawekwa wazi kwasabubu mimi ni mchezaji naweza kucheza timu yoyote, hivyo naamini kama suala la mimi kutua huko likiwa na ukweli klabu itatoa taarifa,” alisema mchezaji huyo wakati akizungumza na gazeti hili.

Mbali na Yanga ambayo mshambuliaji huyo alijiunga nayo Agosti 2021 akitokea Biashara United, pia Athuman ameichezea Coastal Union kwa mkopo msimu wa 2022/23.

Related Posts