Hafidh: Mtibwa Sugar ni suala la muda Ligi Kuu

STRAIKA wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh amesema siri ya kung’ara kwake kwenye Championship ni ushindani wa namba kikosini huku akielezea kuwa timu hiyo kurejea Ligi Kuu ni suala la muda tu.

Hafidh aliyewahi kutamba na timu kadhaa za Ligi Kuu ikiwamo Coastal Union, Dodoma Jiji na Gwambina, ameonekana kuibeba zaidi Mtibwa Sugar akiipa matokeo mazuri kutokana na kasi aliyonayo kwenye kufunga mabao.

Nyota huyo hadi sasa ndiye kinara wa mabao Championship akitupia saba na kuiwezesha timu hiyo kuwa kileleni kwa pointi 19 wakiwaacha Geita Gold kwa alama mbili kwenye msimamo.

Staa huyo licha ya kuaminiwa na benchi la ufundi, anakabiliwa na upinzani wa namba dhidi ya mastaa wengine akiwamo Anuari Jabir, Juma Luizio, Amis Jogo, Omary Mlungu mwenye mabao mawili baada ya kupandishwa kutoka (U20).

Akizungumza na Mwanaspoti, Hafidh amesema vita ya namba kikosini inamuongezea presha kuhakikisha anapopewa jukumu uwanjani anaonyesha kitu cha ziada.

Amesema kwa mwanzo walionao hadi sasa inawapa matumaini ya kuweza kurejea Ligi Kuu, akieleza kuwa kushuka daraja kwa Mtibwa Sugar ni bahati mbaya kwani ni timu kubwana yenye historia.

“Kuondoka kwa Melis Medo tutamkumbuka kwa alichotufanyia, lakini kwakuwa amemuacha ambaye walikuwa wote haiwezi kutuathiri, kimsingi tunapambana kila mechi kutafuta ushindi,” amesema Hafidh.

Amefafanua kuwa ushindani wa ligi ulivyo, unaongeza nguvu na ari kwao kupambana kutafuta pointi tatu katika kila mechi akieleza kuwa Mtibwa Sugar kurudi Ligi Kuu ni suala la muda.

Related Posts