Hakimu adaiwa kubaka na kulawiti, RPC, Waziri Gwajima watoa neno

Dar es Salaam.  Polisi Mkoa wa Mara inafanya uchunguzi kuhusu tuhuma za hakimu kudaiwa kumbaka na kumlawiti binti ambaye jina lake linahifadhiwa mkazi wa Manispaa ya Musoma mkoani humo.

Tukio hilo linadaiwa kutokea mjini Musoma usiku wa Novemba 9, 2024  Mtaa wa Kenedi ndani ya Manispaa ya Musoma wakati binti huyo mwenye miaka 25 alipokwenda nyumbani kwa hakimu huyo aliyemuahidi kumpatia kazi.

Akizungumza na Mwananchi  jana Jumanne Novemba12, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara (RCP), Pius Lutumo amesema kwa sasa jeshi hilo linaendelea na uchuguzi wa tukio hilo baada ya kuripotiwa.

“Tukio lipo ni kweli wala siyo siri, ila kwa sasa sina taarifa za kina hivyo siwezi kulizungumia labda kesho (Jumatano) nitakapokuwa na faili nitaweza kukueleza kwa undani,” amesema.

Wakati Kamanda akisema hayo, Mwananchi limezungumza na binti huyo ambaye amekiri kutokea kwa tukio hilo ingawa amekataa kuzungumza kwa undani huku akiahidi kufanya hivyo baadaye.

“Ni kweli tukio limetokea na sasa tunafuatilia kujua mwisho wake, naomba nikupigie simu baadaye siyo kwa sasa,” amedai binti huyo na kukata simu.

Mwananchi limemtafuta hakimu huyokwa simu kuhusu tukio hilo ambapo  amesema,“Sifahamu chochote kuhusu madai hayo.”

Taarifa zinadai hakimu aliyehusika na tukio hilo ni wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na kwamba baada ya tukio hilo alikamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Musoma.

Taarifa hizo zinadai baada ya kukaa kituoni kwa saa kadhaa hakimu huyo aliweza kudhaminiwa na hakimu mwenzake.

Inadaiwa binti huyo alikuwa akitafuta kazi na baada ya hakimu huyo kupata taarifa hizo alimuahidi kumpa kazi ya kuuza duka ambapo alimtaka binti kufika nyumbani kwake kwa mazungumzo na maelekezo zaidi ya kazi hiyo.

Baada ya binti kufika nyumbani ndipo hakimu huyo alipomtaka binti huyo kufanya naye mapenzi lakini binti huyo alikataa kufanya hivyo.

Inadaiwa baada ya binti kukataa hakimu huyo alimshika kwa nguvu kisha kumbaka na kumlawiti na kufuatia tukio hilo binti huyo aliamua kutoa taarifa polisi kwa hatua zaidi.

Kupitia mtandao wake wa X (zamani twitter) Meya mstaafu wa Ubungo, Boniface Jacob maarufu Boni Yai ameandika kuhusiana na tukio hilo huku akimtaka Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kufuatilia suala hilo.

Boni amesema tukio hilo la kubakwa na kulawitiwa kwa binti huyo limeripotiwa na kufunguliwa kesi  lakini zipo dalili za kuzimwa kwa kesi hiyo.

“Mheshimiwa fuatilia haraka taarifa za kubakwa na kulawitiwa kwa binti huyo, alibakwa na kulawitiwa na hakimu, wanataka kuhonga wazazi,” ameandika Boni ambaye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chadema.

Kutokana na taarifa hiyo, Waziri Gwajima kupitia mtandao wake wa X amejibu na kusema tayari amewasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Mara hivyo anasubiri kupata mrejesho.

Related Posts