Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikitarajiwa kushiriki mkutano wa G20, wanazuoni wamesema ni nafasi ya nchi kujipambanua juu ya mwelekeo wake wa uchumi wa kujitegemea ili kunufaika na fursa zitakazokuwepo.
Wasomi hao waliobobea katika uchumi na biashara ya kimataifa, wamesema ni vema nchi ikaweka wazi msimamo wake wa kujitenga na utegemezi, badala yake ionyeshe utayari wa kujifunza kutoka kwa mataifa hayo ya G20.
Kauli za wanazuoni hao zinakuja muda mchache baada ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kuelezea mwaliko uliotolewa kwa Tanzania kushiriki mkutano wa G20.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva amemwalika Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki mkutano huo utakaofanyika Novemba 18 na 19, 2024.
Hata hivyo, Rais Samia anakuwa mkuu wa nchi wa kwanza kushiriki mkutano wa nchi hizo za G20 zinazochangia asilimia 85 ya pato la jumla la dunia na asilimia 75 ya biashara ya kimataifa.
Awali, Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa na wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete walishiriki mikutano wakati umoja huo ukiitwa G8, kabla ya mabadiliko ya mwaka 2008.
Mwanazuoni wa Uchumi na Biashara ya Kimataifa, Profesa Francis Matambalya amesema ushiriki wa Tanzania katika G20 ni fursa adhimu.
Lakini, ameeleza ushiriki huo huo unaweza usiwe fursa iwapo nchi haijajiandaa kuvuna kutoka katika mkutano huo.
Kwa mujibu wa Profesa Matambalya, mavuno ya fursa hizo yatatokana na Tanzania kujiamini kiasi cha kumudu kueleza uhalisia wake.
Sambamba na hilo, amesema fursa hizo zitavunwa iwapo wanaokwenda watakumbuka wajibu wa Tanzania katika kuisemea Afrika na mataifa mengine ya Kusini.
“Ushiriki wa Tanzania katika G20 ni fursa, iwapo atakayeshiriki atahakikisha anasema uhalisia wa nchi na kuzisemea nyingine za Afrika kama ambavyo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliweka msingi huo,” ameeleza.
Mwanazuoni huyo aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, amesema katika mkutano huo Tanzania inapaswa kujifunza kutoka kwenye nchi zenye nguvu ya kiuchumi na majeshi.
“Katika mkutano huo itawezekana kujua mambo mengi hasa namna nchi kama zetu (zinazoendelea) zinavyoweza kupewa nafasi ya kujitegemea badala ya kuwa wategemezi,” amesema.
Ameshauri msafara utakaokwenda kushiriki unapaswa kujikita katika kuielezea Tanzania kama nchi inayolenga kujitegemea na sio kujijenga kwa utegemezi.
“Twende kule tukiwa tunajiamini tutarudi na kitu, tukienda bila kujiamini tutarudi bila kunufaika na chochote. Hatupaswi kuishia kushiriki kwa sababu ya kuwepo, bali tusimame kuwa kama msemaji wa nchi za Afrika na nchi za kusini,” ameeleza Profesa Matambalya.
Kwa kuwa mkutano huo unayakutanisha mataifa yenye nguvu kiuchumi, ushiriki wa Tanzania utatoa fursa ya kujitangaza kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benedict Mongula.
Profesa Mongula amesema wataokwenda wanapaswa kuhakikisha wanatumia nafasi hiyo kutangaza fursa za uwekezaji na utalii zinazopatikana nchini.
“Kampuni, mashirika na viongozi wa nchi za G20 wataijua Tanzania kupitia ushiriki wake. Sio kila mtu anaijua Tanzania, tunapokwenda kujieleza vizuri tutajulikana na kuvuna fursa,” amesema.
Profesa Mongula ameeleza msingi wa uchumi wa Taifa lolote ni uwekezaji, hivyo kuna fursa ya kuwavutia wawekezaji kutoka G20.
Mwanazuoni huyo, aliuhusisha ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo na nafasi ya nchi kuepuka matendo yasiyofaa ulimwenguni.
“Tusiende kienyeji tujiandae ili kuonyesha fursa zetu, waende watu wanaotakiwa watakaotumia vema fursa zitakazopatikana,”amesema Profesa Mongula.
Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika katika Jiji la Rio de Janeiro, nchini Brazil umebeba kaulimbiu ya ‘Kujenga Ulimwengu wa Haki na Sayari Endelevu.’
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ushiriki wa Tanzania unadhihirisha ushawishi wake katika medani ya kimataifa, ukiakisi juhudi za kidiplomasia za Rais Samia zinazolenga kuwawezesha vijana na wanawake.
Sambamba na hilo, pia taarifa hiyo inasema ushiriki wa Tanzania unadhihirisha juhudi za nchi katika kushughulikia changamoto za mabadiliko ya nishati, umaskini, njaa, ukosefu wa ajira kwa vijana, athari za mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula.
“Haya pia ni mambo ambayo yamepewa kipaumbele katika mkutano wa G20 wa mwaka 2024,” inaeleza taarifa hiyo.
Inasema kupitia mkutano huo, Tanzania inatanua hadhi yake kimataifa na kuongeza kasi ya kufikia malengo yake ya maendeleo, kwa kupata ufadhili na ubia wa kimkakati kwa miradi mbalimbali, ikiwamo nishati safi ya kupikia.
“Aidha, ushiriki huo unatarajiwa kuvutia wawekezaji katika miradi ya usalama wa chakula kwa kuhimiza kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, kushughulikia athari za tabianchi katika mifumo ya chakula, na kuimarisha uimara wa kikanda,”inaeleza taarifa hiyo.
G20 inajumuisha nchi 19 ambazo ni Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japani, Jamhuri ya Korea, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani, pamoja na mashirika mawili ya kikanda, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika.