Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki ameuawa kwa madai ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Jumatano Novemba 13, 2024.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa, tukio hilo lilitokea Kijiji cha Njiapanda ya Tosa, Wilaya ya Iringa alipokuwa akiishi. Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tosamaganga, ambako alifariki dunia.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilolo, John Kiteve, akizungumza na Mwananchi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema limewasikitisha.
Kiteve amefafanua kuwa, tukio hilo lilitokea kati ya saa 4:30 na 5:00 usiku wa kuamkia leo.
“Sisi kama chama tumepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa sana. Tunatarajia kufanya mazishi keshokutwa na Katibu Mkuu wa CCM Taifa Emmanuel Nchimbi anatarajia kuhudhuria,” amesema Kiteve.
Mwananchi inaendelea kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi ili kupata taarifa zaidi kuhusu tukio hilo.