KONA YA MALOTO: Trump aionyesha dunia Marekani inavyoishi kwa dhana za Hollywood

Saa 8:24 usiku, Florida, Marekani, ni saa 4:24 asubuhi Dar es Salaam, Tanzania. Ilikuwa Novemba 6, 2024. Siku imebadilika kutoka Novemba 5, 2024, ambayo Marekani ilifanya uchaguzi wa Rais, Seneti na Baraza la Wawakilishi.

Muda huo, Donald Trump, alikuwa anatembea kwa mikogo yenye kuonesha jeuri kubwa, akipanda jukwaani kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mar-a-Lago, West Palm Beach, Florida. Alizungukwa na washauri, viongozi wa chama, familia yake na marafiki.

Namba zilishatoa uelekeo kuwa Trump atakuwa Rais wa 47 wa Marekani. Republicans wamepata ushindi mkubwa. Democrats, yamekuwa matokeo mabaya kwao. Mgombea wa Democratic, Kamala Harris, dhahiri kawa mwepesi dhidi ya Trump.

Kwa Democrats, kushindwa kwa Kamala siyo anguko la kawaida kwa chama. Kupoteza kiti dhidi ya Trump ni zaidi ya pigo la uchaguzi. Ni kawaida Democratic kushindana na Republican (GOP). Ni ushindani wa sera na ahadi kuhusu ndoto ya Marekani.

Republican ambayo mgombea wake ni Trump, inakuwa zaidi ya chama cha siasa. Waliberali (Democrats), hasa wale vindakindaki, wanaamini Trump hawi Rais ambaye atazibeba sera za wahafidhina (Republicans) dhidi ya zile za Democrats, bali anaweza kuipeleka nchi nje ya misingi inayojenga ndoto ya Marekani.

Trump, baada ya kupanda jukwaani, Mar-a-Lago, aliwatazama wafuasi wake waliovaa kofia nyekundu zenye maandishi, MAGA, kifupi cha “Make America Great Again”, ambayo ni sera ya Trump akitamba kuifanya Marekani kuwa bora tena.

Jinsi alivyokuwa akitazama watu, ilithibitisha kiburi chenye tambo za kishujaa. Taswira kama kumtazama mhusika mkuu wa sinema ya Hollywood, baada ya kukamilisha misheni ya kuua watu kwenye mtandao wa majambazi.

Mhusika mkuu wa kwenye filamu za Hollywood, anaweza kuua kijiji kizima au hata kukata vichwa watu wote katikati ya jiji, lakini mwishoni anakuwa shujaa. Hata akikamatwa, ataachiwa tu. Marekani imekuwa filamu ya Hollywood, na mhusika mkuu ni Trump.

Hatia ya makosa 34 ya uhalifu mkubwa, matumizi mabaya ya fedha na rushwa. Novemba 26, 2024, anatarajiwa kusomewa adhabu. Ana kesi nyingine mbili zinamsubiri, ikiwemo ya kujaribu kupindua matokeo ya Uchaguzi wa Rais 2020. Alipokuwa Rais, alinusurika mara mbili kung’olewa madarakani. Amewahi kufilisika mara sita. Wamarekani wamempa miaka mingine minne awaongoze.

Wasifu huo ndio ambao unathibitisha jinsi Wamarekani walivyotekwa na dhana zinazozipamba filamu za Hollywood. Mtu anayekutana na misukosuko mingi na kuishinda ni shujaa. Anakuwa mhusika mkuu wa sinema hata kama ni muuaji.

Unaweza kuelewa kwa nini Trump ameshinda urais.
Trump alishinda urais uchaguzi wa 2016. Rekodi yake akiwa Rais ipo wazi, jinsi alivyoonesha kuwa adui wa demokrasia, alivyogombana na wataalamu katika mambo ya kitaalamu.

Hulka zake zilifanya aanzishiwe mchakato wa kuondolewa madarakani mara mbili. Ikahojiwa hadi utimamu wa akili yake. Ukaanzishwa muswada wa mgombea urais apimwe kwanza akili. Bado Wamarekani wameona Trump ndiye chaguo sahihi.

Mwaka 2016, Trump alishinda urais kupitia kura za majimbo (electoral college), alishindwa na Hillary Clinton (Democrat) katika kura za wananchi (popular votes). Uchaguzi 2024, Trump amemshinda Kamala kuanzia kwenye electoral college hadi popular votes. Ni ushindi wa uhakika.

Tafsiri ni kuwa watu wanampenda sana Trump. Kwa mapenzi yao, kila kinachosemwa juu yake, wanachukulia kuwa anasingiziwa, kama ambavyo mhusika mkuu wa filamu za Hollywood, hukamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya kusingiziwa, hufungwa hata jela, lakini baadaye hutoka na kuua wabaya wake wote.

Ushindi wa Trump unabeba mantiki hiyo ya dhana ya filamu za Hollywood. Rais Joe Biden, Kamala, Rais wa 44 wa nchi hiyo, Barack Obama, wanaonekana kuwa maadui wa mhusika mkuu wa sinema, kwa hiyo ni muda wao kukiona cha moto.

Trump, hata kampeni zake zilijaa maneno makali ya kukamia watu. Alisema, Biden, Kamala na Obama, wanastahili kuwa jela. Na kwa vile Januari 20, 2025, atakula kiapo kuiongoza Marekani kwa mara nyingine, inatarajiwa itakuwa zamu yake kuwawinda na kuwalipa kisasi wabaya wake wote.
 

Trump, mwanasiasa anayejijenga kwa agenda za umaarufu (populist), huzungumza kama wanasiasa wengi wa dunia ya tatu. Mathalan, aliposhindwa Uchaguzi 2020 na Biden, alilalamika kuibiwa kura, kama wanasiasa wa upinzani Afrika.
Ushindi wa Trump, unadhihirisha umahiri wa kucheza na maneno.

Aliweza kuwafanya wanaume wengi kumwamini, akawavuruga wanawake. Alihakikisha anajenga hoja kwa msisitizo kuhusu uhamiaji haramu na uchumi. Alifanya watu wasijadili masuala ya utoaji mimba, demokrasia na ghasia alizosababisha makao makuu ya bunge, The Capitol, Januari 6, 2021.

Trump, anarejea Ikulu, White House, akiweka rekodi ya kuyashinda mara mbili majaribio ya wanawake, kuongoza dola kubwa, United States of America. Hakudhaniwa angemshinda Hillary mwaka 2016, lakini alimshinda katika upinzani mkali. Amefanikiwa pia kwa Kamala, Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke Marekani. Halafu ni mwanamke mweusi, mwenye asili ya India na Afrika.

Kiasili, Democratic ngome yake ni mijini, hasa kwenye majiji makubwa. Hiyo ndiyo sababu siku zote New York na California ni majimbo ya Democrats (blue states). Maeneo ya vijiji ndiyo maskani ya Republicans. Shida kubwa ya Marekani ni kuwa wapigakura wa vijijini hawana ufahamu wa kutosha kuhusu siasa za dunia.

Marekani, nchi ambayo inapokea wageni wengi kutoka mabara yote, kikazi, kiutalii na hata wenye kuhamia jumla, lakini ina raia wengi ambao hawajawahi kusafiri japo mara moja nje ya majimbo waliyozaliwa. Utafiti uliofanywa na taasisi ya OnePoll, kisha kuchapishwa na jarida la Forbes mwaka 2019, unaonesha kuwa asilimia 11 ya Wamarekani hawajawahi kutoka kwenye majimbo yao tangu walipozaliwa.

Asilimia 54 ya Wamarekani wamewahi kutembelea majimbo chini ya 10, kati ya 50 yanayounda dola hiyo. Hivyo, zaidi ya nusu ya Wamarekani, wanaijua nchi yao kwa asilimia 20 tu. Zaidi ya nusu ya Wamarekani hawajawahi kumiliki hati ya kusafiria (pasipoti). Asilimia 13 ya Wamarekani hawajawahi kusafiri kwa ndege.

Watu wa aina hiyo, nyakati za mapumziko wanatazama habari na makala kwenye redio na televisheni, wanaona nchi yao ndiyo inaisaidia Ukraine dhidi ya Urusi. Wanaona nchi yao inafanya hisani, hawajui wala hawaoni faida ya Marekani katika vita ya Ukraine. Wanapomsikiliza Trump na sera za MAGA, wanamwona ndiye mtu sahihi.

Trump, huzungumza lugha ya kwenye meza ya chakula cha jioni (dinner table language), katika nyumba za wahafidhina wengi. Hawaijui dunia na hawatambui dhana ya hegemony, inayohusu dola moja kuwa kiranja wa ulimwengu. Wanapomsikiliza Trump anazungumza kuilinda nchi yao dhidi ya wahamiaji haramu na kubana matumizi kwa kuwarudisha nyumbani wanajeshi waliopo vitani Ukraine, wanamwelewa zaidi.

Dunia hutoa macho na kufuatilia uchaguzi wa Marekani kwa dhana kuwa anayeshinda hutoa picha ya uelekeo wa dunia. Wamarekani wenyewe, hawajali dunia. Mwaka 2016 Hillary, na 2024 Kamala, walipigiwa chapuo kama chaguo la dunia. Wamarekani hawaichagulii dunia rais, wanajichagulia kiongozi wao.

Trump, anawajua Wamarekani kwa wingi wao wanatamani nini na siyo dunia inataka Marekani ifanye nini. Huwakuna mno anapozungumza lugha yao. Covid-19 iliipigisha magoti Marekani na dunia. Wamarekani wengi kwa kutoijua nchi yao vema, wanapomsikia Bernie Sanders anasema kuwa watu wengi walipoteza maisha kwa uongozi mbaya wa Trump, wanaona anasingiziwa. Wao hawakushuhudia vifo hivyo.
 

Agosti 21, 2024, Hillary akihutubia Kongamano la Kitaifa la Democratic (DNC), alisema kuwa Trump alitaka urais kwa ajili yake binafsi ili ajiokoe na hatia 34 za uhalifu, alizokutwa nazo mahakamani. Hillary pia alitaka Wamarekani wamchague Kamala ili wabaki kitu kimoja, kwani sera za Trump zinabeba mgawanyiko.

Trump ni populist. Uchaguzi kwake ni vita. Hivyo, huzungumza kinachoweza kufanya apendwe na akubalike, hata kama kina gharama kwa nchi. Hiyo ndiyo sababu Trump amekuwa hatari kwa mshikamano wa Wamarekani. Hata hivyo, watu wengi hawajui madhara ya sera za makundi ya kijamii. Wanamwona Trump ni mtetezi wao.

Marekani imefika hapa. Trump, binadamu mwenye hatia ya makosa 34 ya uhalifu mkubwa, siyo tu aliruhusiwa kugombea urais, bali pia ndiye mshindi. Anasubiri muda ufike aapishwe. Yupo Mmarekani alisema, ushindi wa Trump unaifanya dunia ione Marekani inafanya maigizo ya televisheni (reality show), kwenye mambo ya msingi.

Trump alipoiongoza Marekani kati ya Januari 20, 2017 mpaka Januari 20, 2021, matendo aliyokuwa anayafanya kama rais, yalisababisha Obama wakati fulani aseme: “Trump anaongoza nchi kama vile anacheza reality show.” Lugha za hivyo ni za mjini. Wapigakura wengi vijijini Marekani, waliona Obama alimwonea wivu Trump.

Jaji Juan Merchan wa Mahakama ya New York, aliahirisha kutoa adhabu dhidi ya Trump hadi Novemba 26, 2024. Baada ya kushinda kesi, bado Jaji Merchan anaweza kumpa kifungo rais huyo mteule. Hata hivyo, matarajio ni wanasheria wa Trump kukata rufaa na kuomba adhabu isitekelezwe mpaka rufaa isikilizwe ili kumruhusu Trump atekeleze majukumu aliyochaguliwa kuyatekeleza.

Mwendesha mashitaka wa Brooklyn, New York, Julie Rendelman, anasema kuwa Trump hawezi kutumikia kifungo kutokana na mazingira yaliyopo. Na mchakato wa rufaa inaweza kuchukua miaka, kipindi hicho Trump akiendelea kutekeleza majukumu yake ya urais.

Kuhusu kesi nyingine zinazomkabili, ikiwemo ya jaribio lake la kupindua matokeo ya urais Uchaguzi 2020, Katiba ya Marekani inasema wazi rais madarakani hashitakiwi. Zaidi, Trump ameshaahidi kuwa akishakula kiapo, atamfuta kazi mara moja Wakili Maalumu Wizara ya Haki Marekani, Jack Smith, kwa kuwa ndiye amevalia njuga mashitaka dhidi yake.

Upande wa siasa, hakuna anayeweza kutabiri Trump atakapoapishwa ataamua nini. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanajiandaa kwa lolote kuhusu usalama na jeshi la nchi za Magharibi (Nato). China, wao wanaona ni fursa kwao kujenga ushawishi Asia na Afrika, maana Trump atayaweka mbali mabara hayo.

Ukraine inaweza kubaki pweke, wakati Urusi wakijihakikishia usalama hadi kwa nchi jirani. Inasubiriwa tamthiliya nyingine ya Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un. Kwa Israel, ujio wa Trump ni neema.

Related Posts