Kulingana na Cris Kacita, mkuu wa operesheni za programu ya udhibiti wa mpox nchini Kongo, wamesalia na dozi 53,921 za chanjo kwa matumizi katika magereza – ambapo watu wako katika hatari kubwa kutokana na hali duni – lakini wanahitaji zaidi ya dozi 162,000 ili kuzindua mpango wa chanjo katika mji mkuu Kinshasa.
Soma pia: Chanjo ya mpox kuchukuwa muda mrefu zaidi Kongo
Kufikia sasa, mji huo wenye wakazi karibu milioni 20, umeathiriwa kidogo kuliko mikoa mingine ambako mipango ya chanjo inaendelea.
Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika – Africa CDC, imesema wafadhili wamechelewa kutimiza ahadi zao za msaada wa kifedha na chanjo.
Kacita amesema, Ufaransa iliahidi dozi 100,000, pamoja na nyegine kutoka Ujerumani na Umoja wa Afrika. Lakini kufikia sasa haijulikani ni lini zitafika. Ameongeza kusema kwamba kuwasili kwa chanjo pia kucheleweshwa na mchakato wa kiutawala, unaojumuisha kutuma ombi rasmi, utengenezaji, utayarishaji wa hati na kupata idhini ya uagizaji.
Ripoti ya wizara ya Afya ya Kongo imeonyesha kuwepo na jumla ya visa vipya 1,017 vinavyoshukiwa, kuanzia Oktoba 28 hadi Novemba 2, ikijumuisha visa 45 vilivyothibitishwa na vifo 16.
Watoto katika athari zaidi
Shirika la hisabu la Save the Children, lilisema chanjo zinahitajika kuzuwia kasi ya kusambaa kwa virusi vya Mpoxmiongoni mwa watoto, ambao wana uwezekano wa kufa karibu mara nne zaidi kutokana na aina mpya ya virusi hivyo kuliko watu wazima.
Takwimu za shirika hilo zinaashiria kuwa, visa vya maambukizi vinavyoshukiwa miongoni mwa watoto nchini Kongo vimeongezeka kwa zaidi ya 130% tangu Agosti 14, kutoka 11,300 hadi 25,600 kufikia Novemba 3.
Haya yanajiri huku Kamati ya Dhaura ya Shirika la Afya Duniani ikitarajia kufanya kikao ili kuamua iwapo mpox inasalia kuwa dharura ya kiafya ulimwenguni.
Soma pia: Chanjo za ugonjwa wa Mpox zaanza kutolewa Afrika
Mnamo Agosti, ugonjwa huo ambao unaendelea kuenea barani Afrika uliainishwa na Shirika la afya Duniani kuwa dharura ya kiafya kimataifa. Nchi zilizoathirika zaidi ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Uganda.