Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amewaonya wagombea katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho, kujiepusha na vitendo vya rushwa, huku akiwataka wanachama kuwapima wagombea kama watafaa na vita vinavyokuja vya uchaguzi mkuu wa 2025.
Lissu amesema hayo leo Jumatano Novemba 13, 2024 alipokuwa akihutubia mkutano wa uchaguzi wa chama hicho mkoani Singida, akisema kuna mambo makubwa yanayokikabili chama hicho, hivyo viongozi watakaopatikana lazima wawe na sifa ya kukabiliana nayo.
“Kuna mambo makubwa yanayotukabili mbele yetu. Tuangalie changamoto zilizopo mbele yetu, halafu tujiulize, hizi changamoto zinahitaji watu wa aina gani? Vita iliyoko mbele inahitaji majemedari wa aina gani. Mbele yetu ni vita, mbele yetu ni matatizo makubwa sana, yanahitaji viuongozi wanaoweza kuongoza mapambano ya hiyo vita,” amesema.
Amesema kwa bahati mbaya au nzuri chama hicho kinafanya uchaguzi wa viongozi katikati ya vita, vita ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Mtu anayekwambia njoo chukua hela, anayekurushia hela uje kwenye mkutano, anayekuweka kwenye nyumba ya kulala wageni ili umpe kura anakusaidia ni kweli, anayekupa hela ya chakula anakusaidia ni kweli, anayekupa chochote akwambie hivi nipigie kura, mkono mtupu haulambwi, huyo anayekwambia umpigie kura, sisemi usilambe, lamba lakini jiulize, hii asali ameipata wapi?” amehoji.
Amesema wakati chama hicho kikiwa kwenye hali ngumu kifedha katika kutafuta wagombea wa vijiji, mitaa vitongozji, pesa hakuna, kufanya mikutano ya hadhara, kukodi vyombo usafiri, lakini kumekuwa na dalili za rushwa katika chaguzi za ndani.
“Kwenye uchaguzi mapesa yapo kila mahali. Naomba ujiulize, hayo mapesa ni ya kwetu kweli? Hiyo asali ni ya kwetu, kama sio ya kwetu, jiulize ni ya nani na tunalambishwa kwa manufaa ya nani? Ukishajiuliza hivyo kapige kura.
“Rushwa ni adui wa haki. Biblia imeandika, rushwa hupofusha macho ya wenye haki. Huyo anayekwambia mkono njoo ulambe asali mkononi mwangu, hiyo ni rushwa hata uite majina matamu namna gani, hiyo ni rushwa. Jiulize, anaitakia nchi hii mema, natutakia mema? Kwenye mapambano yajayo atakuwepo? Atasimama upande gani au atasimama upande wa waliokulambisha asali. Ukiridhika naye umpe kura halafu usubiri matokeo,” amesema.
Huku akisoma mwongozo wa chama dhidi ya rushwa toleo la 2012, Lissu amesema Chadema imejipambanua kupinga rushwa hadharani.
“Mtu anayekupa rushwa, kwenye vita ya mwaka ujao hutamwona, wanatengeneza vitega uchumi vya sasa. Wakati wagombea wetu wakienguliwa, hamtawaona, mtakapovurugiwa uchaguzi hamtawaona, mkikamatwa hamtawaona,” amesema.
Amewataka wajumbe wa mkutano huo kuwapima wagombea kwa kazi walizofanya hasa kwa uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa.
“Yeyote anayegombea nafasi yoyote ile, wewe mpiga kura jiulize, katikati ya vita hii, huyo anayeomba kura amefanya nini? Aliweka wagombea wangapi kwenye maeneo yake? Wakati wagombea wanaenguliwa kulia na kushoto, juu chini amesaidiaje kurudishwa?”
“Hii vita ya sasa ni maandalizi ya vita ya vita ya mwaka ujao. Jiulize kama kwenye mapambano ya sasa hajaonekana kwenye uwanja wa mapambano, mwaka ujao akiwa kiongozi mtamwona? Kwa hiyo kipimo cha kiongozi anayetaka kuchaguliwa leo ni haya ya mapambano yanayoendelea,” amesema.
Awali, akizungumza wakati wa kumkaribisha Lissu, Kamanda wa Operesheni wa Kanda ya Kati, Patrick Ole Sosopi amesema baadhi ya viongozi wa chama hicho wameshindwa kuwajibika.
“Wapo viongozi wameshindwa, wanaishi katika kitongoji kinakosa mgombea, kijiji kinakosa mgombea na wewe ni kiongozi wa wilaya au mkoa, unasababu gani za kuendelea kuwa kiongozi wakati unashindwa kusimamisha mgombea? Hili hatutakubali.
“Kwa hiyo baada ya uchaguzi huu, lazima tutatafakari na kuona, kila mtu atakula alikopeleka mboga,” amesema.