MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI UTOAJI TUZO KWA WASHINDI WA MIRADI YA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI – AZERBAIJAN

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ni muhimu kuhakikisha fedha za ufadhili wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinawafikia jamii ya asili (wazawa) ili waweze kubuni miradi ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuwa wanafahamu zaidi changamoto za maeneo yao.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukabidhi tuzo kwa kwa washindi wa miradi ya ubunifu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa na jamii za asili (wazawa) kutoka sehemu mbalimbali duniani katika shindano linaloratibiwa na Taasisi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi Duniani (GCA). Hafla hiyo imefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.

Amesisistiza umuhimu wa viongozi kuwatambua na kuwawezesha wabunifu wa miradi inayotekelezwa na wanajamii wa asili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa jamii kuendelea kuanzisha miradi ya ubunifu itayosaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa Taasisi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi Duniani (GCA) kuongeza wigo wa mashindano hayo ili kuwafikia wabunifu wengi zaidi ikiwemo wanaofanya shughuli zinazohusiana na uchumi wa buluu.

Amesema Tanzania ina mifano ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutoka kwa wananchi wazawa ambapo wanawake katika ukanda wa bahari Zanzibar wanajishughulisha na kilimo cha mwani ambacho ni matokeo ya kuongezeka kwa kina cha bahari kunakosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Amesema hapo awali wanawake hao walijishughulisha na kilimo cha mpunga kabla ya ujio maji mengi ambayo pia wanatumia katika ufugaji wa samaki wa vizimba.

Amehimiza kufanya ufadhili kwa wananchi hao ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi wa buluu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Tuzo hizo zimetolewa kwa miradi minne ya ubunifu katika vipengele vya usalama wa chakula, ujasiriamali wa ndani, usalama wa maji na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Washindi wa tuzo hizo ni kutoka nchi za Burkina Faso, Indonesia, Argentina na Kiribati.

Rais wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni moja ya majaji walioshiriki katika kuchambua miradi hiyo ili kupata washindi wa jumla duniani.

Related Posts