Rasimu hiyo iliyotolewa leo Jumatano haijaleta suluhu za hoja za muda mrefu ambazo zimechelewesha makubaliano ya ongezeko la fedha zaidi kwa mataifa masikini yanayoathirika na mabadiliko ya tabianchi.
Kufikia makubaliano mapya ya kuongeza fedha kwa ajili ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi masikini ni kipaumbele muhimu kwa wapatanishi takriban 200 katika mkutano wa kelele wa Umoja wa mataifa kuhusu mazingira COP29.
Kulingana na rasimu hiyo ya mkataba wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, nchi zote masikini zimekuwa zikisubiri ahadi ya kila mwaka kutoka nchi tahjiri ya angalau dola trilioni 1.3.
Soma pia:Azerbaijan yashtumu mataifa ya Magharibi kwa kuiharibia sifa
Idadi hii ni zaidi ya mara 10 ya dola bilioni 100 kila mwaka ambazo kundi dogo la nchi zilizoendelea ikiwemo miongoni mwao Marekani, Umoja wa Ulaya na Japan wanalipa hivi sasa.
Baadhi ya wafadhili wanasuasua kuahidi kiasi kikubwa kipya cha fedha za umma kutoka kwenye bajeti zao wakati ambapo wanakabiliwa na shinikizo la kiuchumi na kisiasa katika mataifa yao.
Ikumbukwe kwamba toleo la awali la rasimu hiyo lilikataliwa moja kwa moja na nchi zinazoendelea, ambazo zilizingatia masharti yaliyopendekezwa kuelemea kwa kiasi kikubwa kwa mataifa tajiri.
Mataifa ya Afrika yataka mabadiliko ya kimfumo
Wanajopo kutoka mataifa ya Kiafrika katika mkutano huo wa mazingira kwa mwaka huu wanasema wanataka kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kufanya marekebisho kwenye vipaumbele na kutetea mageuzi ya usanifu wa kifedha.
Musalia Mudavadi Waziri Kiongozi kutoka Kenya aliitaja changamoto “ya kutisha lakini inayoweza kuzuilika” ambayo itahitaji kushughulikiwa ili kuzuia mataifa yanayoendelea barani Afrika kukabiliana na limbikizo la madeni yanayoongezeka katikati ya changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa.
“Tunahimiza mageuzi sanifu ya mfumo wa fedha kwa sasa duniani, ikiwa ni pamoja na kuanzisha deni la mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema mbele ya jopo kwenye mkutano huo unaovuta nadhari ya kimataifa hasa kwa wadau wa mazingira.
Soma pia:Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu kasi ya mabadiliko ya tabianchi
Aliongeza kuwa “fedha maalum za hali ya hewa na masharti ya ukopeshaji yaliyorekebishwa ili kuwezesha Afrika kukabiliana ipasavyo na dharura za hali ya hewa.”
Mataifa ya Kiafrika yanatumai kutumia fedha hizo kuboresha uwezo wao wa kustahimili hali mbaya ya hewa, kama vile ukame au mafuriko, kupanda miti na kulinda bayoanuwai, na pia kupanua uwezo wao wa nishati mbadala.
Guterres: COP29 itoke na majibu
Hapo Jana Jumanne Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres aliyarai mataifa tajiri kuongeza ufadhili wake maradufu kwa ajili ya kukabiliana na madiliko ya hali ya hewa hadi dola za Marekani bilioni 40 kwa mwaka ifikapo 2025.
Soma pia:Guterres: Tuendelee kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Cop29 lazima itoke na jawabu juu ya ufadhili wa mabadiliko ya hali ya hewa.” Alisema nchi zinazoendelea hazipaswi kuondoka Baku mikono mitupu lazima mchakato huo ufanikiwe
“Nina imani litafanikiwa. Tunahitaji kuwa na malengo mapya ya kifedha ambayo yanakidhi kwa wakati huu.”
Mkutano wa mwaka huu wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa COP29 unakusanya takriban mataifa 200 mjini Baku lengo likiwa ni kukusanya mabilioni ya dola ili kufadhili mpito wa kimataifa kwa vyanzo vya nishati safi na kupunguza uharibifu wa hali ya hewa unaosababishwa na utoaji wa hewa ya kaboni.