Morogoro wapokea vifaatiba kupunguza maambukizi mapya ya VVU

Morogoro. Shirika la Kimataifa la Afya ya Familia (FHI 360) kupitia mradi wa kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) wa Epic, unaofadhiliwa na PEPFAR, limekabidhi vifaa tiba kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matumizi katika vituo 15 vya afya.

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh52 milioni, Meneja wa Mradi wa Epic Morogoro, Aziz Haka amesema utoaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya afya kwa ajili ya kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kuwahamasisha watu kujitokeza kwa ajili ya upimaji na kuanza dawa za ARV.

“Pamoja na kutoa vifaa tiba, FHI kupitia mradi wa Epic imekuwa ikitoa elimu kuhusu Ukimwi kwa vijana na jamii kwa jumla na kuhakikisha huduma za matibabu zinawafikia watu hadi ngazi ya jamii,” amesema Haka.

Msimamizi wa Mfumo wa Ugavi wa Mradi wa Epic-FHI 360, Anneth Masawe amevitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na vya kupima na kutunza sampuli, makabati ya kuhifadhi kumbukumbu, glovu, makoti na buti za mvua, mabegi ya kubebea vitabu na nyaraka za kumbukumbu, pamoja na vifaa vingine vya kuendeleza kazi ya  upimaji wa VVU.

Amesema vifaa hivyo vitapelekwa kwenye vituo 15 vya afya na vitatumiwa na watoa huduma wa Ukimwi ngazi ya jamii, ili waweze kufika kwa urahisi kwa jamii na kutoa huduma za elimu na upimaji.

Hadi kufikia Septemba mwaka huu, Mkoa wa Morogoro umefikia asilimia 93.8 ya watu wanaotambua hali yao ya maambukizi ya VVU, huku asilimia 98.2 ya wale waliogundulika kuwa na maambukizi hayo wakiwa wanaendelea kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Best Magoma amesema mkoa huo una jumla ya vituo 516 vinavyotoa huduma za VVU na Ukimwi pamoja na vituo 383 vya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha.

Amesema kati ya Januari na Septemba 2024, watu 406,045 walijitokeza kupima VVU katika vituo hivyo na kati yao, 6,464 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU na wameanza huduma ya dawa za ARV.

“Mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Ukimwi, umejikita katika upimaji wa malengo, upimaji wa wenza na watoto na upimaji wa mtandao ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ifikapo 2030,” amesema Dk Magoma.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya VVU kwa sababu mwanzoni, watu walikuwa na hofu ya kujitokeza kupima na unyanyapaa ulikuwa mkubwa.

Hata hivyo, amesema kwa sasa Serikali kwa kushirikiana na wadau, ina matumaini kuwa maambukizi yatafikia sifuri siku zijazo.

Related Posts