Msikie Awesu kuhusu Maxi Zengeli

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Awesu Awesu amemtaja Maxi Nzengeli wa Yanga ni mchezaji mzalendo ndani ya timu yake ambaye anapambana kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Kauli ya Awesu imekuja baada ya hivi karibuni Maxi kumtaja kiungo huyo kuwa miongoni mwa wachezaji anaowakubali na kutamani kucheza naye timu moja.

Maxi alisema: “Awesu kipaji chake ni kikubwa, anajua mpira, napenda anavyoisaidia timu yake.”

Ubora wa Maxi na kile anachokisema Awesu unajidhihirisha namna ilivyokuwa msimu uliopita na alicheza mechi 23 kwa dakika 2090 ndani ya Ligi Kuu Bara akifunga mabao 11 na asisti mbili, huku msimu huu akimiliki mabao matatu aliyofunga dhidi ya Kagera Sugar, Pamba Jiji na KMC.

Akizungumzia ubora wa Maxi, Awesu amesema: “Kwanza napenda aina ya uchezaji wake, mtulivu, mzalendo kwa klabu yake, unamuona anavyopambana kwa muda wote anaokuwepo uwanjani, nidhamu yake ipo juu.

“Nzengeli ni kati ya viungo wenye vipaji vikubwa na anatunza kiwango chake kwani msimu uliopita mchango wake ulikuwa mkubwa katika timu yake na amekuwa na muendelezo mzuri msimu huu.”

Rekodi zinaonyesha, Awesu katika mechi tisa alizocheza Simba msimu huu amefunga mabao mawili na asisti moja, hivyo kauli ya Maxi aliichukulia kama chachu ya kujituma zaidi kuhakikisha timu inafaidi huduma yake.

“Unapoona kuna watu wanakubali unachokifanya, inakupa nguvu ya kupambana kwa ajili ya kuisaidia timu, msimu huu kwangu naamini utakuwa wa mafanikio makubwa,” alisema.

Related Posts