KATIKA kikosi cha Simba, kuna washambuliaji wa mwisho wawili raia wa kigeni, Leonel Ateba na Steven Mukwala. Nyota hao hadi sasa wamehusika kwenye mabao saba kati ya 21 yaliyofungwa na timu hiyo ambayo imeruhusu nyavu zake kutikisika mara tatu kwenye mechi 10 ilizocheza ndani ya Ligi Kuu Bara.
Usajili wa Ateba ni pendekezo la kocha Fadlu Davids baada ya kuona kuna upungufu eneo hilo wakati wa maandalizi ya msimu ‘pre season’ ndipo alipouomba uongozi kumuongezea nguvu eneo la ushambuliaji.
Ujio wa Ateba dakika za jioni kabla ya dirisha kubwa la usajili kufungwa ulibeba matumaini makubwa ya kufanya vizuri zaidi ya Willy Onana aliyeuzwa siku chache kabla ya usajili kufungwa sambamba na kuondoka kwa Freddy Michael ambaye alihudumu kikosini hapo kuanzia dirisha dogo la msimu uliopita na kufunga mabao tisa yakiwamo sita ya ligi, mawili ya Kombe la Shirikisho na moja Kombe la Muungano.
Maswali ambayo washambuliaji hao wanapaswa kuyajibu kwa haraka hivi sasa wakati Simba ikiwa imecheza mechi 14 za mashindano tofauti msimu huu ni kuhakikisha namba zinaongea.
Ukiangalia Ateba bado hajaonyesha makali kama ambavyo wengi walimtarajia, ingawa tayari ameifungia Simba mabao matatu kwenye mechi nane za michuano tofauti. Mabao mawili ligi kuu na moja Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika ligi, Ateba aliyecheza mechi saba kwa dakika 488, alianza kuifunga Azam FC, timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini, kisha akafunga tena kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa nyumbani, lakini baada ya hapo hajafanya maajabu yoyote zaidi ya kutoa asisti dhidi ya Namungo.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika aliwafunga Al Ahli Tripoli wakati Simba ikishinda 3-1 nyumbani na kufuzu hatua ya makundi.
Kwa mechi alizocheza Ateba, ameonyesha uwezo wa kushambulia na kushuka chini kutafuta mpira ikiwa ni sambamba na kusaidiana na mabeki kuzuia mashambulizi.
Nyota huyo aliyewahi kuzichezea klabu mbalimbali zikiwemo za Cotonsport na PWD Bamenda, mwaka 2023, alipoibuka mfungaji Bora wa Ligi ya Cameroon baada ya kufunga mabao 21, akajumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon kilichoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) zilizofanyika mapema mwaka huu Ivory Coast.
Ateba alijiunga na USM Alger, Januari, mwaka huu akitokea Dynamo Douala ya kwao Cameroon ambapo msimu uliopita alicheza michezo 23 katika mashindano tofauti, akafunga mabao matatu na kuasisti mara saba, hivyo ni wazi kuwa asipokufunga anaweza kutengeneza nafasi.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Ateba, upande wa Mukwala kapachika mabao mawili katika ligi hadi sasa na kutoa asisti mbili akicheza mechi zote kumi kwa dakika 418.
Lakini pia mshambuliaji huyo raia wa Uganda amecheza mechi mbili za Ngao ya Jamii na mbili Kombe la Shirikisho Afrika bila ya kufunga.
Kinachomgharimu zaidi Mukwala mpaka sasa ni kwamba hana utulivu ndani ya eneo la hatari licha ya kuacha rekodi nzuri Asante Kotoko ya Ghana alikotoka.
Hata hivyo, mpaka sasa ameonyesha ana kitu na anatakiwa kuendelea kuaminiwa kwa kupewa muda zaidi kama ambacho Kocha Fadlu anafanya, huku jukumu likibaki kwake kujitathimini kama anatosha kuendelea kubaki kikosini hapo.
Kazi aliyo nayo Mukwala ni kuhakikisha anawajibu mashabiki, viongozi na benchi la ufundi kwa kuzitumia vizuri nafasi zinazotengenezwa kwa kufunga au kutoa pasi za mwisho kwa wenzake wafunge.
Licha ya kocha kuamini kuwa mchezaji huyo anateswa na presha ya mashabiki, bado hatakuwa na nafasi ya kutetewa litakapokuja suala la nani aachwe ili aongezwe mchezaji mwingine ambaye atafanya kazi kwa usahihi.
Mchezaji huyo umri unambeba kutokana na sasa ana miaka 25 sawa na Ateba, lakini namba bado zinamkataa ndani ya kikosi cha kocha Fadlu, ingawa kama akiongeza utulivu na kujitenga kwenye maeneo sahihi ataweza kuifungia Simba mabao mengi msimu huu.
Simba kwa miaka mitatu mfululizo imekuwa ikipambana kusaka mshambuliaji wa kimataifa ambaye ataweza kufanya makubwa kama ilivyokuwa kipindi cha Emmanuel Okwi.
Mbali na Okwi, Simba pia imewahi kuwa na Meddie Kagere ambaye alitwaa Tuzo ya Ufungaji Bora katika Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo msimu wa 2018-2019 na 20190-2020 akiwa na timu hiyo rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa.
Mukwala ametua Simba akikumbukwa zaidi msimu uliopita ambapo alifunga mabao 14 akiwa na kikosi cha Asante Kotoko nyuma ya kinara mshambuliaji wa Berekum Chelsea, Stephen Amankonah aliyefunga 16.
Pia aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Ghana, Desemba, mwaka jana, akiwa na kikosi hicho alichojiunga nacho Agosti 2022 akitokea URA ya Uganda. Katika msimu wa kwanza alifunga mabao 11 na kutoa asisti tano.
Akiwa URA, Mukwala alicheza kwa misimu mitatu kuanzia 2019-2020 alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda akifunga mabao 13 na 2020-2021 akafunga 14, kisha 2021-2022 akatupia tena kambani mabao 13. Hii ni kuonyesha kuwa sio mchezaji wa kubezwa kwani namba zinambeba.