Dar es Salaam. Kampuni maarufu ya gesi ya kupikia ya Oryx Energies Tanzania, imejikuta katika changamoto baada ya kutakiwa kulipa karibu Sh500 bilioni baada ya kuamuriwa na jukwaa la usuluhishi.
Fedha hizo zinazotajwa kufikia Sh468 bilioni zinatokana na madai ya awali, gharama za usuluhishi na riba kuanzia mwaka 2016. Deni hilo linakuwa linaongezeka kila mwaka kwa wastani wa asilimia 8, ikijumuisha riba za kibiashara na mfumuko wa bei.
Kampuni hiyo inayotawala soko la gesi ya majumbani (LPG) la ndani kwa zaidi ya asilimia 40 hapa nchini imejikuta ikitakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha kwa Kampuni ya Oilcom katika uamuzi ambao uliibua mjadala mzito.
Madai hayo yaliyopelekwa kwenye usuluhishi na Oilcom dhidi ya Oryx Energies Tanzania Limited, yalitokana na mikataba ya usafirishaji mafuta na kukodishwa kwa vituo vya petroli tangu mwaka 2016.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mgogoro au tofauti baina yao ilikuwa utawasilishwa katika jukwaa la usuluhishi linaloundwa na wasuluhishi watatu, huku kila upande ukiwa na haki ya kuchagua msuluhishi wake na yule anayechaguliwa na pande zote kuwa mwenyekiti.
Hata hivyo, kinachoonekana sasa ni kama Oryx haijaridhishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu iliyomuidhinisha mjumbe mmojawapo wa jukwaa hilo ambapo inadaiwa alikuwa na maslahi na upande wa Oilcom, sasa kampuni inafanya jitihada zaidi za kumaliza mgogoro huo baada ya kukwama katika rufaa zake mbili.
“Kampuni imejizatiti kujitetea kwa kutumia njia zote za kisheria zinazowezekana,” alisema Msemaji wa Oryx, ambayo imeshindwa rufaa mbili katika Mahakama Kuu, ikipinga uhalali wa mjumbe mmojawapo wa jukwaa hilo tangu mwaka 2022.
Aidha, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Oryx Energies Tanzania kilidokeza kuwa pamoja na changamoto zinazotokana na mgogoro huo uliopo, bado kampuni hiyo inafanya kila jitihada kuhakikisha mwafaka unapatikana na inaendelea na uwekezaji wake hapa nchini.
Pamoja na vikwazo vya kisheria, ikiwemo kufilisiwa kwa mali zake na hisa katika miradi muhimu, Oryx bado inaendelea kushirikiana na wadau wake kwa kutafuta namna ya kulinda maslahi ya biashara zake na kuendeleza wajibu wake kwa sekta ya nishati nchini Tanzania.
“Msimamo wa ndani unaonyesha kuwa kampuni hii imedhamiria na kuamini katika njia bora za kumaliza mgogoro kwa kushirikiana na vyombo husika vya usimamizi,” kilieleza chanzo hicho.
Mtoa taarifa ambaye hakupenda jina lake litajwe alidokeza kuwa endapo biashara hiyo itaathirika kiasi cha kulazimika kufunga, wafanyakazi zaidi ya 700 watakosa ajira za moja kwa moja.
Mbali na ajira za moja kwa moja, hatua hiyo inaweza kuathiri vibarua na mnyororo mzima wa usambazaji wa nishati nchini, ikizingatiwa nafasi yake katika bidhaa ya LPG na wingi wa vituo vya mafuta vinavyomilikiwa na kampuni hiyo.
Kadhalika taasisi za ukopeshaji zinaweza zikajikuta zikipoteza fedha kutokana na kuwa na mikopo isiyolipika, hivyo kuathiri uchumi wa watu wengi kwa namna tofauti.
Mchambuzi wa uchumi, Edward Chalo alisema mgogoro huo wa kisheria unaoendelea kati ya Oryx Energies na Oilcom unaonyesha masuala yaliyopo ya mazingira ya biashara Tanzania na kuleta wasiwasi kuhusu suala zima la uwekezaji nchini na kwa jumuiya ya kimataifa.
“Kwa kuwa na madai makubwa ya kukiukwa kwa taratibu, kumeifanya kesi hii kuwa na mvuto kwa wawekezaji wa ndani na kimataifa,” alieleza Edward Chalo, mchumi aliyewahi kufanya kazi katika Benki ya Dunia.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.