Polisi yachunguza tukio la mfanyabiashara aliyenusurika ‘kutekwa’ Kiluvya

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inayowaonyesha watu wawili wakijaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari mfanyabiashara, eneo la Kiluvya jijini Dar es Salaam.

Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi leo Jumatano Novemba 13, 2024 imesema kijana aliyekuwa akiingizwa kwa nguvu kwenye gari  anafahamika kwa jina la Deogratius Tarimo.

“Jeshi la Polisi linachunguza picha mjongeo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha watu ambao wanajaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari, Deogratius Tarimo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha, mkoani Pwani. Tukio hili liliripotiwa na yeye mwenyewe katika kituo cha Polisi Gogoni Jijini Dar es Salaam Novemba 11, 2024,”imesema taarifa hiyo.

Polisi kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, David Misime limesema kijana huyo alikwenda kwenye  Hoteli ya Rovenpic lilipofanyiwa tukio hilo ni kufanya mazungumzo ya kibiashara ambayo alianza kuyafanya na watu hao tangu Oktoba 25, 2024.

Picha za CCTV zikionyesha Deogratius Tarimo akichukuliwa kwa nguvu na watu watatu kutoka katika hoteli

“Jeshi la Polisi linahakikisha litawakamata watu waliokuwa wakijaribu kumkamata na kumwingiza kwenye gari kama inavyoonekana katika picha mjongeo hiyo, kulingana na ushahidi ambao umeshakusanywa na unaoendelea kukusanywa ili hatua nyingine zichukuliwe kwa mujibu wa sheria, kwani hakuna aliye juu ya sheria,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika video yenye sekunde 49 iliyoanza kusambaa jana Novemba 12, 2024 usiku katika mitandao ya kijamii ilimuonyesha kijana huyo (aliyetambuliwa kama Deogratius Tarimo) akiwa analazimishwa kuingia ndani ya gari aina ya Toyota Raumu na vijana wawili.

Wakati tukio hilo likiendelea, Tarimo alikuwa akipiga mayowe ya kuomba msaada huku akisema “Naenda kuuawa..nisaidienii” hata hivyo, miongoni mwa waliomkamata alisema “Sisi ni maaskari…twende Gogoni”

Hata hivyo, hadi mwisho wa video hiyo inaonyesha, Tarimo alifanikiwa kujichoropoa mikononi mwa watu hao.

Related Posts