Geita. Sh422.6 milioni zimetengwa ili kukamilisha miradi 34 ya maendeleo iliyokuwa ikijengwa kwa fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR), kwa kipindi cha 2018/2021 na kuachwa ‘viporo.’
Miradi hiyo mingi ni ile ya ujenzi kwa sekta ya elimu na afya iliyojengwa kwa ushirikiano baina ya Halmashauri ya Mji wa Geita na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kupitia fedha za CSR.
Akitoa taarifa kwa baraza la madiwani leo Jumatano Novemba 13, 2024, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Yefred Myenzi amesema timu ya wataalamu wa halmashauri na wale wa GGML wamekaa na kupitia miradi yote 38 na kubaini kati ya hiyo, iliyokamilika ni minne pekee.
Amesema ili kuikamilisha miradi 34, Sh422.6 milioni zinahitajika na tayari wametoa ombi kwa GGML kuhamisha fedha na kuziweka kwenye akaunti ya halmashauri ili wazisimamie na kuanza ukamilishaji kuanzia sasa hadi Desemba, mwaka huu.
“Mheshimiwa mwenyekiti tumezungumza na GGML, badala ya kazi hii kupewa mkandarasi mmoja ambaye atazunguka kwenye miradi yote, tumeomba fedha zihamishiwe halmashauri nasi tuwatume mafundi kwenye kila mradi ili hadi mwisho wa mwaka huu, iwe imekamilika,” amesema Myenzi.
Kuhusu miradi ya mwaka 2022/23, Myenzi amesema utekelezaji wake unaendelea ipo miradi ambayo tayari imekamilika na ile ya kimkakati ukiwamo uwanja wa mpira, shule maalumu ya msingi Bombambili na ujenzi katika eneo la soko la dhahabu ambayo usanifu wake unafanywa upya kutokana na bei ya awali kuwa kubwa.
Wakati huohuo, Baraza la Madiwani limepitisha azimio la hoja binafsi ya mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu ya kuitaka halmashauri kutafuta fedha za dharura za kukarabati kituo cha mabasi cha Geita mjini kilichoharibiwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni.
Akizungumza kwenye baraza hilo, Kanyasu amesema licha ya halmashauri kuwa na mpango wa kujenga kituo kipya cha mabasi eneo la Usindakwe Magogo, mpaka sasa hawajaingia mkataba na mkandarasi yeyote kutokana na mchakato wa ununuzi kuendelea.
“Kipindi cha mvua wananchi wanateseka na stendi iliyopo na inatia aibu Halmashauri ya Mji wa Geita, niiombe halmashauri ione namna na ipange bajeti ya dharura kukarabati stendi hii inayotia aibu kwa kila anayepita eneo hili,”amesema Kanyasu.
Akichangia hoja hiyo, Makamu mwenyekiti wa baraza hilo, Elias Ngole amesema wakati halmashauri inakarabati kituo hicho cha mabasi, ni vema wakala wa barabara wakarekebisha mitaro kwa kuweka matoleo ya maji, kwa sababu yaliyopo yana mdomo mdogo usioendana na mapokeo ya maji.
“Mwenyekiti mafuriko yaliyotokea stendi hayakutokana na mvua, yalisababishwa na mtaro kuwa na matoleo madogo ya kutolea maji, kwa hiyo wakati sisi tunatafuta fedha za kukarabati ni vizuri wenzetu Tanroads waboreshe miundombinu yao kwa kupanua mitaro au kuweka matoleo makubwa ya maji,”amesema Ngole.
Kupitia ombi hilo, baraza kwa pamoja limeazimia halmashauri kupitia ia upya bajeti yake na kuona vifungu na miradi itakayoweza kuahirishwa ili fedha zitakazopatikana zielekezwe kwenye ukarabati wa stendi kwa haraka.