SIMBA Queens leo imetoa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga Princess na kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Wanawake ikiwa na pointi 12.
Ikiwa kwenye harakati za kutetea taji la ligi hiyo, dakika ya 48 ya mchezo huo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Vivian Corazone alilipa presha lango la Yanga Princess na Danai Bhobho akajifunga likiwa ni bao pekee lililoipa ushindi Simba Queens.
Baada ya kupata bao hilo, Simba Queens iliendelea kulishambulia lango la Yanga Princess kupitia kwa Elizabeth Wambui na Corazone waliokuwa mwiba mchungu kwa Wananchi lakini hakukuwa na mabadiliko ya ubao wa matokeo.
Kipindi cha kwanza timu zote mbili hazikufungana lakini Simba Queens ikionekana kusogea zaidi langoni mwa Yanga Princess ingawa mashambulizi hayakuwa na matokeo chanya.
Simba Queens ilitengeneza nafasi nyingi lakini utulivu kidogo wa nyota wake uliwanyima kuandika bao ndani ya dakika 45 za kwanza.
Simba Queens ambayo leo ilikuwa mgeni wa Yanga Princess, pointi tatu ilizoondoka nazo imeifanya kuwa ndio timu pekee kwenye ligi hiyo msimu huu hadi sasa imeshinda mechi zote baada ya kila timu kucheza mechi nne.
Mchezo wa kwanza Simba Queens ilitoa kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Mlandizi Queens, kisha ikaichapa Fountain Gate Princess 3-0 na Ceasiaa Queens 4-1.
Yanga Princess kwenye mechi nne ilizocheza, imetoka sare tatu dhidi ya Bunda Queens 0-0, Alliance Girls 0-0 na Mashujaa Queens 1-1 kabla ya kufungwa na Simba Queens 1-0.
Hii inakuwa mara ya pili msimu huu timu hizo zinakutana baada ya awali kupambana Oktoba 2 kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii na Yanga Princess ilishinda kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare 1-1.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Simba Queens imeendelea kuwa wababe wa Yanga Princess kwani tangu mwaka 2018, Yanga Princess imeshinda mechi moja pekee, ilikuwa Aprili 4, 2022 kwa bao 1-0 lililofungwa na Clara Luvanga, wakati Simba Queens ikifikisha ushindi wa tisa huku sare zikiwa tatu kwenye mechi 13 za ligi.