Vyombo vya habari vya ndani vinaonyesha wapiga kura wakisubiri kwenye foleni kupiga kura zao, huku wengi wao wakisema wanataka uchumi imara na ajira zaidi, miongoni mahitaji mengine ya ndani.
Zaidi ya watu milioni 1 wanatarajiwa kupiga kura katika vituo 2,000 vya kupigia kura, huku waangalizi 28 wa kimataifa wakifuatilia zoezi hilo kwa ukaribu kote nchini.
Soma pia: Kiongozi wa upinzani ashinda Somaliland
Katika kinyanganyiro hicho Rais Muse Bihi Abdi wa Chama tawala cha Kulmiye anatafuta muhula wa pili baada ya miaka saba madarakani, ambapo ameisukuma Somaliland kutambulika kimataifa, akipambana na Abdirahman Mohamed Abdullahi wa chama kikuu cha upinzani cha Waddani.
Soma pia: Waziri wa ulinzi wa Somaliland ajiuzulu
Abdullahi, ni mwanadiplomasia wa zamani na Spika wa muda mrefu wa Bunge la Somaliland akiwa na sera ya kuleta mageuzi ya kidemokrasia na uwiano wa kijamii.
Mgombea mwengine ni Faisal Ali Warabe kupitia chama cha Haki na Ustawi akishinikiza sera ya serikali ya umoja wa kitaifa.
Wakosoaji, wanamshutumu Bihi kwa utawala wa kiimla uliochochea mgawanyiko wa kikabila.
“Hatutaki kumuongezea muda tena Muse Bihi. Tumesubiri kwa muda mrefu uchaguzi huu. Hatuwezi kukubali kuongezwa tena muhula.”
“Muda wa Muse umekwisha. Ameiharibu Somaliland. Akaifanya wilaya ya Oog kuwa mpaka wetu, akaanzisha vita huko Eneo la Sool, ameharibu jeshi, amerudisha nyuma uwepo wa Somaliland.”
Uhuru na uthabiti
Somaliland, ambayo ilitangaza uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991, licha ya kukabiliana na migogoro, imedumisha serikali yake, sarafu na miundo ya usalama licha ya kukosa kutambuliwa kimataifa.
Kwa miaka mingi, eneo hilo limejenga mazingira thabiti ya kisiasa, tofauti kabisa na mapambano yanayoendelea ya Somalia na ukosefu wa usalama.
Matatizo ya kiuchumi ya eneo hilo ni miongoni mwa sababu zilizotajwa na serikali wakati ilipotangaza kucheleweshwa kwa uchaguzi wa urais mwaka 2022.
Soma pia:Somalia yasema vitendo vya Ethiopia vinakiuka uadilifu wake
Uchaguzi huu unafanyika wakati eneo hilo likimulikwa kimataifa kufuatia mzozo mkubwa kati ya Somalia na Ethiopia, baada ya makubaliano ya ukodishaji wa bandari baina ya Addis Ababa na Somaliland, ambapo Somalia inaishutumu Ethiopia kwa kudhoofisha uadilifu wa eneo lake.