Stars kuifuata Ethiopia kimkakati | Mwanaspoti

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inatarajia kuondoka nchini kesho kwa ajili ya mchezo wa tano wa kusaka tiketi ya kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, dhidi ya Ethiopia, mechi itakayopigwa keshokutwa Jumamosi.

Stars inaingia katika mchezo huo wa tano wa kundi ‘H’ ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa suluhu mechi ya mwisho dhidi ya Ethiopia iliyopigwa Septemba 4, mwaka huu, huku kwa upande wa Wahabeshi hao wakipoteza kwa mabao 3-0, mbele ya Guinea.

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla, kaimu kocha mkuu wa Stars, Hemed Suleimani ‘Morocco’ alisema, licha tu ya ugumu wa mchezo huo ila wao kama benchi la ufundi na wachezaji kiujumla wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo chanya ugenini.

“Kila mmoja wetu yupo tayari kwa changamoto nyingine, tunatambua wapinzani wetu wamekuwa na matokeo yasiyoridhisha sana ila tutacheza kwa tahadhari ya kuhakikisha tunashinda, mchezo huu utatoa taswira yetu ya kufuzu AFCON mwakani Morocco.”

Kocha huyo aliongeza, ni ushindi pekee ndio utawaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu huku akiweka wazi wanahitaji kuutumia mchezo huo vizuri bila kuangalia matokeo ya wapinzani wao Guinea watakaocheza na DR Congo ili kutengeneza mazingira mazuri mechi ya mwisho.

“Wenzetu DR Congo walishafuzu hivyo presha ipo kwetu na Guinea ambayo iko juu yetu kwenye msimamo, mchezo na Ethiopia tunauangalia kwa jicho la tatu kwa sababu ndio utakaotupa matumaini makubwa kuelekea mechi ya mwisho hapa Dar es Salaam.”

Stars itacheza mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa des Martyrs huko Congo na baada ya hapo itacheza na Guinea jijini Dar es Salaam Novemba 19, huku mara ya mwisho zilipokutana Stars ilishinda mabao 2-1, Septemba 10, mwaka huu.

Kundi la ‘H’ linaongozwa na DR Congo iliyofuzu tayari ikiwa na pointi 12, ikifuatiwa na Guinea yenye sita huku Stars ikiwa ya tatu na pointi zake nne, wakati Ethiopia inaburuza mkiani na pointi yake moja baada ya timu zote kucheza michezo minne.

Timu hiyo imeshiriki AFCON tatu tofauti ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa ya Nigeria mwaka 1980, kisha ikapata nafasi hiyo tena baada ya miaka 39, ya kushiriki ilipofanya hivyo mwaka 2019, Misri chini ya Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike.

Mara ya tatu ilikuwa mwaka huu wa 2024 kule Ivory Coast ikiwa na Kocha Mkuu, Adel Amrouche ambapo ilipangwa kundi ‘F’ lililokuwa na timu za taifa za Morocco, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuishia hatua ya makundi.

Related Posts