Morogoro. Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kimejipanga kuwatumia wataalamu wa ndani kutumia bayoteknolojia ili kusaidia kupata majibu ya kisayansi katika uzalishaji wa mazao nchini.
Kauli hiyo imetolewa mwanzoni mwa wiki hii na Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda mjini Morogoro baada ya kutoka kwenye mkutano wa Chama cha Wataalamu wa Sayansi za Mazao Tanzania (CROSAT) uliofanyika Dodoma.
Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu ya: “Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia teknolojia za uzalishaji wa mazao,” umeshirikisha jopo la watafiti wabobevu wa teknolojia hiyo kutoka Tanzania, Ubelgiji na Kenya.
Profesa Kibunda amesema SUA wameshapeleka maombi serikalini ili iwe moja ya vituo vya umahiri vitatu vinavyoanzishwa na Serikali kwa ajili ya kufanya tafiti za bayoteknolojia ili kusaidia nchi kubaini ukweli kuhusu teknolojia hiyo kwa.
“Ni maombi ya wanasayansi kwamba, muda umefika sasa wa nchi zetu za Afrika na Tanzania kuangalia upya tunawezaje kushiriki kwenye hii teknolojia kama ambavyo tumeambiwa na wenzetu wa Ubelgiji kuwa nchi za Marekani, China, India wanavyoshiriki.
“Pia, tumeona nchi za Ulaya japo hawalimi sana mazao yatokanayo na teknolojia ya uhandisi jeni lakini ni watumiaji wakubwa kwa kuwa wanaagiza kutoka katika nchi zinazolima na wanatumia kwa manufaa ya nchi zao,” amesema.
Profesa Chibunda amesema chuo hicho kitakuwa mstari wa mbele katika kuanza kufanya utafiti ili kuona hata kama kuna madhara basi madhara hayo yadhihirike kwa kazi ambayo imefanywa na watu wao wenyewe badala ya kutegemea maneno ya kuambiwa au kutegemea tafiti zinazofanywa nje ya mazingira yeo.
Awali, Profesa Marc Heidje kutoka Taasisi ya Flemish ya Bayoteknolojia (VIB) ya Ubelgiji amesema kufuatia ongezeko kubwa la watu duniani, kupungua kwa maeneo ya kilimo kutokana na makazi, mabadiliko ya tabianchi na uhitaji mkubwa wa chakula kulisha watu hao nchi nyingi duniani zinatumia teknolojia hiyo na kusaidia kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo.
“Teknolojia hii sio risasi ya shaba kwenye kutatua changamoto zote za kilimo, bali ni teknolojia nzuri inayorahisisha uzalishaji wa mbegu kwa kupata sifa zinazohitajika kwa haraka ukilinganisha na njia za kawaida,” amesema Profesa Marc.
Ameongeza kuwa, kumekuwa na maneno mengi ya uzushi wa kutisha watu kuwa, nchi za Ulaya hazilimi wala kula mazao yatokanayo na teknolojia ya uhandisi jeni, lakini niwathibitishie kuwa ubelgiji tunalima na tunaingiza mazao hayo kwa wingi kutoka nchi zinazolima na nchi nyingi za Ulaya zinalima na kuagiza kwa wingi sana mazao hayo kwa ajili ya chakula cha binadamu na mifugo,” amesema.