Dar es Salaam. Umewahi kusikia dhana ya ‘unsung hero’? yaani shujaa asiyeimbwa?
Dhana hii inamgusa Susie Wiles moja kwa moja mwanamama aliyepambana katika ushindi wa Rais Donald Trump nchini Marekani akiwa meneja wa kampeni huku akiwa nyuma ya jukwaa mara nyingi.
“Baada ya dhiki, faraja,” hatimaye Susie amechaguliwa na Rais Mteule Trump kuwa Katibu Mkuu wa Ikulu ya White House katika uongozi wa awamu ya 47.
Kwa uteuzi huo, Susie anakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, Trump amekuwa akimtaja kama mtu mwerevu na mbunifu.
Kama hufahamu mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 67 amehusika katika ushindi wa Trump katika chaguzi zote mbili, kuanzia ule wa 2016 hadi huu wa 2024.
Kwa mujibu wa tovuti ya Cbsnews, Susie anajulikana kama mtaalamu wa siasa anayependelea kufanya kazi kimya kimya yaani nyuma ya pazia na mara nyingi hapendi kusimama wala kuonekana jukwaani au mbele ya kamera.
Hili limedhihirika baada ya Trump mapema asubuhi ya Jumatano Novemba 6, 2024 kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya urais, alimuita aje jukwaani kwenye kipaza lakini alikataa.
Susie anatajwa kupendwa zaidi na washirika wa karibu wa kampeni za Trump, hili linathibitishwa na Mshauri Mkuu wa Trump, Danielle Alvarez aliyenukuliwa siku chache zilizopita akisema: “Susie Wiles ni mtetezi mkubwa wa Rais Trump na kiongozi mwenye maono.”
Pia, Brian Hughes mshauri mwingine wa Trump amesema kwake yeye na wengine wengi, kuwa pamoja na Susie kuwa kama mshauri na rafiki lakini pia kwao ni zawadi kubwa.
Baada ya Trump kushinda nafasi hiyo, Novemba 7, 2024 alimteua Susie katika nafasi hiyo nyeti Ikulu ya Marekani.
Susie Wiles alizaliwa Mei 14, 1957, alisoma Chuo Kikuu cha Maryland, College Park (BA) akipata Shahada ya Sanaa katika lugha ya Kiingereza. Susie ni mzaliwa wa New Jersey.
Ni mmoja wa watoto watatu wa Pat Summerall ambaye alikuwa mcheza mpira katika Ligi ya Kitaifa ya Mpira wa Miguu (NFL).
Baada ya kuhitimu alifanya kazi katika kampeni ya urais wa Ronald Reagan na baadaye akaendelea kufanya kazi mbalimbali za kisiasa Jimbo la Florida.
Mwaka 2010, alimsaidia Seneta Rick Scott kushinda uchaguzi wake dhidi ya Bill McCollum wa Democratic, na pia amekuwa mshauri wa kisiasa katika mambo mbalimbali huko Florida.
Mbali na siasa, Susie ni kiongozi wa kampuni kubwa ya ushawishi na mikakati ya Mercury, ambayo wateja wake ni pamoja na SpaceX, AT&T, na Ubalozi wa Qatar.