Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amesema endapo timu hiyo ya Tabora United ikiifuga Simba kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, basi zawadi ya matokeo hayo itakuwa Sh50 milioni.
Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Tabora United kuifunga Yanga kwa mabao 3-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Novemba 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambapo leo wanatarajiwa kukabidhiwa Sh20 milioni ikiwa ni motisha waliyoahidiwa endapo wangepata ushindi huo.
Akizungumza na Mwanaspoti katika shughuli ya kuchangia damu iliyofanyika leo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete, kiongozi huyo amesema timu hiyo inatakiwa kulindwa kwa nguvu zote.
“Hivi karibuni timu yetu imefanikiwa kuifunga Yanga ambayo ni timu bora kabisa hapa nchini na lazima tujivunie uwepo wa timu yetu, na natangaza rasmi kwamba endapo wakipata matokeo ya ushindi mbele ya Simba kwenye mchezo wa marudiano zawadi yao itakuwa shilingi milioni 50 na huo ndio msimamo wangu,” alisema na kuongeza.
“Awali tulitangaza kwamba kokote watakaposhinda mchezo wa nje ya mkoa huu tutatoa zawadi ya shilingi milioni 10 lakini sasa wakaishinda dhidi ya Yanga ndio maana tukasema tuongeze motisha lakini siku tukimuangusha yule mnyama mkubwa kabisa (Simba) motisha yangu itakuwa milioni 50.”
Kwa upande wa mashabiki wa Tabora United waliozungumza na Mwanaspoti, walisema wanaiunga mkono kauli hiyo ya mkuu wa mkoa huku wakiahidi kuendelea kusapoti timu yao.
“Hiki anachokisema mkuu wetu wa mkoa kuongeza motisha kwa wachezaji wa timu yetu ni jambo jema na sisi tunajivunia uwepo wa timu hii, kwenye mechi ya Yanga hatukutegemea kushinda ila wachezaji wakajitoa tukapata matokeo mazuri, hivyo motisha hii iendelee kwani tunajenga timu imara zaidi,” alisema Mussa Simon mmoja wa mashabiki wa timu hiyo.
Ikumbukwe kwamba, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Simba iliifunga Tabora United mabao 3-0 huku timu hizo zikitarajiwa kurudiana Desemba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.