TAKUKURU DODOMA YAWEZESHA HALMASHAURI KUKUSANYA MAPATO YA MIL. 308.6

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma Victor Swella akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi zao Jijini Dodoma.

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Katika kuimarisha ukusanyaji mapato ya Halmashauri za mkoa wa Dodoma Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imesema imefanya ufuatiliaji wa ukusanyaji ushuru wa huduma za leseni za biashara na mabango kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jaji ambapo jumla ya Milioni 308.6 zilikusanywa ndani ya siku Kumi katika kata Tatu.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Novemba 13,2024 ofisini kwao Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma Victor Swella kuhusu utendaji kazi wao katika kipindi cha Mwezi Julai mwaka huu ambapo ametaja kata hizo kuwa ni Madukani, Uhuru na Majengo na makusanyo hayo yanatokana na leseni za biashara Milioni 107.5, Ushuru wa huduma Milioni 194.8 na ushuru wa mabango Milioni 6.

Akizungumzia kuhusu suala la kuzuia Rushwa Bw. Swella amesema wamefanya chambuzi za mifumo 11 ili kupata tija ya mifumo imara isiyokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na utendaji kazi za Serikali kwa ujumla.

“Uchambuzi wa mifumo uliofanyika ni udhibiti wa mapato ya uvuvi katika Wilaya ya Bahi, Uchambuzi wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano na utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu katika Wilaya ya Mpwapwa, usimamizi wa uingiaji mikataba kati ya mafundi ujenzi na kamati za ujenzi Wilaya ya Mpwapwa, Uchambuzi wa mfumo kuhusu mianya ya rushwa katika mchakato wa uunganishaji wa umeme kwa wananchi wilaya ya Bahi na Uchambuzi wa mfumo katika utoaji msamaha wa matibabu kwa wazee na makundi maalum katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, “amesema.

Pia amesema kuwa katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 TAKUKURU imetoa elimu ya athari za vitendo vya rushwa katika uchaguzi na wajibu wa mwananchi katika kuzuia vitendo hivyo.

“Kwenye elimu hiyo tuliyoitoa ilikwenda kwa viongozi wa dini 78, viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali 356, Waandishi wa Habari 55, wadau mchanganyiko wapatao 420, wakuu wa taasisi Dodoma na Wakurugenzi wa utawala na rasilimali wa wizara ya fedha, Wizara ya maji wapatao 50,”amesema.

Amesema katika kipindi kijacho cha kuanzia mwezi Oktoba mpaka Disemba wanatarajia kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya rushwa na ufujaji unaoweza kujitokeza.

Aidha ametoa wito kwa wananchi wote kushiriki vyema katika mapambano dhidi ya Rushwa kwani mapambano hayo ni wajibu wa kikatiba.

“Popote pale mwananchi utakapokwenda kupata huduma ya kijamii timiza wajibu wako kwa kujifunza na kuzifahamu taratibu za upatikanaji wa huduma husika kwa kuhakikisha unazifuata wakati unahudumiwa na usiwe sehemu ya kushawishi kutoa rushwa kwa watendaji, “amesema.

Related Posts