Dar es Salaam. Vilio vya vyama vya upinzani juu ya wagombea wao kutoteuliwa ama kuenguliwa vimesikika baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa kutoa maagizo kwa kamati za rufaa.
Miongoni mwa maagizo hayo kwa kamati za rufaa zinazoongozwa na Makatibu Tawala wa Wilaya ni kuziongezea siku mbili kamati hizo za rufaa kupitia rufaa za wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za vijiji, vitongoji na mitaa utakaofanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024.
Muda wa awali wa rufaa hizo zilianza kusikilizwa Novemba 10 na ulitarajia kukamilika leo Jumatano, 13, 2024 lakini kwa uamuzi wa Wiziri Mchengerwa sasa utahitimishwa saa 12:00 jioni ya Ijumaa Novemba 15, 2024.
Mchengerwa amesema hayo kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa usiku wa leo Jumatano ikiwa ni saa chache kupita tangu, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alipotoa maombi kwa Tamisemi juu ya kinachoendelea kwenye mchakato wa uchaguzi huo.
“Ninazielekeza kamati za rufani za Wilaya kuitisha fomu za wagombea wote walioenguliwa/hawakuteuliwa ili kufanya mapitio na kujiridhisha na sababu zilizopelekea wagombea hao kutoteuliwa ili haki iweze kutendeka kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi,” amesema na kuongeza:
“Ofisi ya Rais – Tamisemi itaendelea kuhakikisha inasimamia misingi ya utawala bora ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka na kuchaguliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi.”
Wagombea wengi wa upinzani walienguliwa kwa kutojaza kwa ufasaha fomu, mihuri, wadhamini kutokuandika majina matatu, tarehe ya kuzaliwa, fomu kuchezewa kwa kuongeza herufi ama tarakimu pamoja na sifa ya mgombea hususan kazi halali ambapo waliojaza ujasiriamali walienguliwa.
Jana Jumanne jioni, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk Emmanuel Nchimbi alikutana na wahariri na waandishi wa habari ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam ambapo alisema kuwa Tamisemi inapaswa kuyapuuza makosa madogomadogo yaliyowafanya wagombea wengi hususan wa upinzani. Mbali na hilo alishauri warejeshwe.
Dk Nchimbi katika mkutano huo alitoa maombi kwa Tamisemi akisema yana baraka zote za Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.
“Nitoe wito kwa Waziri wa Tamisemi tunajua watendaji wamefuata sheria lakini ni muhimu kukumbuka demokrasia yetu bado changa, wanahitaji kukua, tutachukua muda kujifunza, lakini watu wetu hawajazoea vitu hivi na tutachukua muda kujifunza kidogo katika uchaguzi huu.
“Tunaziomba mamlaka zinazohusika hasa Tamisemi katika hatua za mwisho za rufaa kuyapuuza makosa madogomadogo ili watu wengi wapate nafasi ya kugombea,”ameshauri Dk Nchimbi.
Serikali itazame makosa madogo yasipewe uzito kwenye rufaa japo ya kisheria, kwa sababu sheria imewekwa kwa ajili ya kuwasaidia watu, sio kuleta tafrani kwenye jamii,” amesema Dk Nchimbi.
Katika taarifa yake kwa umma, Waziri Mchengerwa amesema, “ninawaelekeza wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri zote kuwarejesha wagombea wa vyama vyote ambao walienguliwa kwa sababu ya kutodhaminiwa na vyama vyao.
Katika ngazi ya kijiji/mtaa pamoja na kuwa vyama hivyo viliwasilisha barua za kuainisha ngazi ya chini ya udhamini kuwa ni kata ikiwemo ACT-Wazalendo kilichowasilisha ngazi yake ya udhamini kuwa ni ngazi ya kata.
ACT-Wazalendo kilieleza wagombea wake zaidi ya 50,000 nchi nzima wameenguliwa kwa sababu hiyo.
“Ninavihimiza vyama vya siasa ambavyo wagombea wao wameenguliwa kutumia vizuri muda huu wa siku mbili ulioongezwa endapo hawakuridhika na uamuzi wa wasimamizi wasaidizi kuhakikisha wanasimamia wagombea wao waweze kuwasilisha rufaa zao kwa kamati za rufani zilizopo katika kila wilaya husika,” amesema.